Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii uliyonipatia ili niweze kuchangia kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuongea mbele ya Bunge lako Tukufu, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kuwa kati ya wawakilishi wa wananchi kwenye Bunge hili la Kumi na Mbili. Nafahamu umuhimu na ukubwa wa nafasi hii, hivyo, namuomba Mwenyezi Mungu akapate kunipa busara na hekima hasa kwa hiki kipindi changu cha miaka mitano ili niweze kuwaongoza watu wake kwa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fursa ya kuusoma vizuri Mpango huu lakini kutokana na muda nimeamua ushauri wangu wote wa kitaalam niuweke kwenye maandishi hivyo baada ya hapa nitakabidhi meza yao ushauri wangu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa hizi dakika chache ulizonipatia, naomba niongee mambo machache hasa yanayohusiana na Jimbo langu la Korogwe Mjini. Nafahamu Mpango huu hasa umejikita kuimarisha uchumi kwenye Sekta ya Viwanda na Biashara. Hata hivyo, ili tuweze kufikia malengo hayo, naomba tuzingatie ushiriki wa wanawake katika uchumi wa viwanda na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu umuhimu wa wanawake katika kukuza uchumi. Hii hata kwenye Biblia inadhihirishwa, inasema wanawake ni Jeshi kubwa. Hata hivyo, ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya uchumi umeathiriwa sana na changamoto mbalimbali kwenye jamii zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini, ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uchumi na biashara pamoja na viwanda umeathiriwa sana na tatizo la maji. Wamama wa Korogwe badala ya kujihusisha kwenye shughuli za kiuchumi wamekuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji kwa ajili ya kuhudumia familia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yamekuwa changamoto kubwa ambayo imewapotezea focus wamama wa Korogwe hivyo kupunguza kasi ya uchumi na maendeleo ya Jimbo letu la Korogwe Mjini. Hivyo nimuombe kaka yangu Mheshimiwa Aweso aone namna gani tunatatua tatizo hili ili akina mama wa Korogwe wakape fursa ya kushiriki kwenye uchumi badala ya kuhudumia familia zao kutafuta maji usiku mzima. Kwa wastani kwenye Jimbo langu tunapata maji mara moja kwa wiki, hivyo tunaomba tuangaliwe kwa jicho la kipekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu pasipo afya bora ni vigumu kuweza kufikia haya maendeleo tuliyoyaainisha kwenye Mpango huu. Hivyo, kwenye sekta ya afya kwenye Jimbo langu la Korogwe pia ni changamoto kubwa. Tuna hospitali yetu moja ya wilaya ambayo tunaitegemea kwenye Jimbo letu la Korogwe, lakini sio Korogwe tu pamoja na wilaya nyingine za jirani; hospitali hii ni chakavu sana imejengwa tangu mwaka 1952 hivyo haiwezi kukidhi mahitaji ya huduma za afya kwenye jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba Wizara husika ione namna gani inatutatulia changamoto hii. Aidha, tukarabatiwe hospitali ile kwa viwango vikubwa au kujengewa hospitali nyingine, ili watu wapate afya bora tuweze kukimbizana na shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba niweze kuungana na watu wengine wengi waliochangia, umuhimu wa miundombinu ya barabara katika kukuza uchumi na kuweza kufikia Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini tuna barabara muhimu sana, barabara hiyo inatuunganisha watu wa Korogwe Mjini, watu wa Korogwe Vijijini, pamoja na Mkinga. Barabara ambayo inatokea Korogwe – Kwa Mndolwa – Magoma, tuliahidiwa na Rais pamoja na Waziri Mkuu tutatengenezewa barabara hii, hivyo namwomba Waziri mhusika wa Wizara hii aweze kutujengea barabara hiyo ili kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)