Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kutumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujaalia afya njema na uzima. Pia tuwe pole katika mzigo uliotufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutambua michango iliyotolewa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Mwenyekiti wake Mheshimiwa Sillo Daniel Baran pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika mjadala huu wa hoja kwa kuzungumza na kwa maandishi hapa Bungeni. Tunawashukuru wote kwa maoni yao na ushauri wao waliotupa kwa ajili ya kuboresha Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026) pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/2022; ushauri wao tumeupokea tunawashukuru sana wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Kiongozi wa Shughuli za Bunge hapa Bungeni Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia na kuwakilisha Serikali hapa Bungeni. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Phillip Mpango Waziri wa Fedha na Mipango kwa ushirikiano na maelekezo mazuri anayoendelea kunipa katika kutimiza majukumu yangu kama Naibu Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kumshukuru Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuwasilisha hoja hii kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango na kuniongoza vyema katika kufuatilia michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, napenda niwashukuru watendaji wote wa Wizara ya Fedha wakiwemo Makatibu, Wakuu wa Idara, watumishi wote wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya ya utangulizi, napenda kuchangia hoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza, Serikali iongeze juhudi katika upatikanaji wa fedha za ziada na ugharamiaji wa miradi ya maendeleona izingatie upande wa Sekta Binafsi, kiwango kimeshuka kiasi cha trilioni nne kwa Serikali na kimeongezeka kwa trilioni 15.2. Kwa hivyo ni vyema Mpango huu wa Taifa kuendelea kutatua changamoto za upatikanaji wa fedha za ugharamiaji Mpango ili kufikia malengo na shabaha tuliyojiwekea. Ufafanuzi, Serikali itahakikisha kuwa rasilimali zote za utekelezaji wa Mpango zinapatikana kama ilivyopangwa ili kuhakikisha malengo ya utekelezaji wa Mpango yanafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vya fedha vya ugharamiaji ni pamoja na Mapato ya Ndani na yasiyo ya ndani, misaada, mikopo nafuu, hati fungani na amana za Serikali; Mikopo ya kibiashara, ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi; Utekelezaji wa moja kwa moja wa taasisi na mashirika ya umma (Joint venture) na utekelezaji wa moja kwa moja wa Sekta Binafsi. Katika kuhakikisha hilo vyombo mbalimbali vya ugharamiaji mapato, vimeambatanishwa katika sehemu ya sita ya kitabu cha Mpango kulingana na eneo la ugharamiaji na aina kubwa za miradi au programu, fursa za kiuchumi, kijamii zilizopo na vihatarishi vya Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja namba mbili; Serikali ihakikishe kuwepo na upatikanaji wa taarifa endelevu za utekelezaji miradi na bajeti, dhidi ya hatua na malengo ya Mpango. Ufafanuzi, katika kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa uchambuzi wa kina wa Taarifa za utekelezaji miradi, Serikali imeandaa Mifumo mbalimbali ya Kielektroniki (GEPG); Mfumo wa Msaada na Ununuzi wa Serikali (TANEBS); Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSTE); Mfumo wa Uandaaji wa Usimamizi wa Bajeti (CBMCS).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mifumo hii Wizara na Idara na Taasisi na Serikali zitaendelea kutoa takwimu sahihi za utekelezaji wa miradi ili kusaidia ufanyaji na tathmini za ufanisi. Aidha, Serikali imeanza maandalizi ya kuandaa mwongozo wa Kitaifa na ufuatiliaji wa tathmini za miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuweka miongozo rasmi katika shughuli za ufuatiliaji na tathmini na kuwezesha mchakato shiriki katika ubia na uandaaji wa taratibu na usimamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja namba tatu, Serikali ihakikishe inaelekeza Mpango Mkuu kulingana na sheria, kanuni na taratibu. Ufafanuzi, ushauri umepokelewa Serikali itaendelea kutekeleza Mipango ya Maendeleo kwa kutimiza sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika Sheria ya Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa ufafanuzi huo, naomba kuunga mkono hoja na kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Ahsanteni sana. (Makofi)