Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii ili nami niweze kuchangia hoja ya kumpongeza Rais wa Tano aliyepita kwa njia ya kifo na Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwape pole wafiwa wote wa Tanzania na hasa wenzetu wa Chama cha Mapinduzi ambao wamempoteza kiongozi wao wa Chama. Naungana na Watanzania wote wanawake kwamba wanawake wamefurahi sana kwamba wamepata kiongozi mwanamke ambaye atapandisha hadhi ya wanawake; kunyanyaswa kwa wanawake tunajua sasa basi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upole, kwa hekima aliyonayo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na kwa CV ambayo tumeiona, tunaamini kwamba atasimama katika nafasi yake kuifanya Tanzania iheshimike katika Taifa hili na nje ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, Watanzania wengi wanaamini kwamba kwa hekima yake atarudisha demokrasia kwenye vyama vyote vya kisiasa vipate nafasi kama ambavyo Muasisi wa Taifa hili Mwalimu Nyerere alitaka kwamba viwe na uhuru ambao ni kikatiba pia, kufanya mikutano yao bila kubughudhiwa na vyombo vya dola. Pia Watanzania wengi wanajua kuwa kupitia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan uhuru wa Vyombo vya Habari na uhuru wa wananchi kujieleza utapatikana yeye akiwa ni mama mwenye busara na hekima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hata Angela Merkel wa Ujerumani jinsi alivyopeleka ile nchi mpaka ikaheshimika mpaka leo. Tunajua kwamba nchi yetu ili iwe na upendo wa kweli na amani ya kweli ni lazima haki itendeke. Haki ndiyo inayoweza kuzaa amani ya kweli na kuleta upendo na umoja katika nchi yetu. Kwa hiyo, tunaamini kwamba kupitia mama kama ambavyo mmesifu, akinamama ni watu ambao hawana ubaguzi; hatujasikia hata siku moja mama akisema mwanawe akafanye DNA, maana watoto wote ni wake. Kwa hiyo, tunajua kwamba vyama vyote ni vyake, wananchi wote ni wake, wenye vyama na wasio na vyama ni wake. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, atasimama katika nafasi yake kuonyesha akinamama ambavyo tunaweza kuendesha nchi na isiingie kwenye mitafaruku wala vita. Kwa hiyo, tunashukuru na tunaamini kwamba Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan atalitendea Taifa hili kazi kubwa na ataonekana mwanamke wa kwanza siyo Barani Afrika tu na duniani kwamba nchi yetu hii ameipaisha kwa kurudisha demokrasia ya kweli, kurudisha vyama vyote viwe na nafasi sawa na kwamba akinamama wa Tanzania hawanyanyaswi tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwombea Mwenyezi Mungu ambariki aweze kufanya kazi yake hii akiongozwa na Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni. (Makofi)