Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujaalia uhai wake ambao leo umewezesha kukutana hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imepita katika mtihani mkubwa sana katika kipindi hiki. Umauti uliowakuta viongozi wetu wakuu wawili katika nchi hii, kwakweli ni pigo kubwa sana. Kuondokewa na Dkt. John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Seif Sharif Hamad, Makamu wa Rais wa Zanzibar. Kwa kweli ni msiba mkubwa ambao katika historia ya nchi hii haujawahi kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema kwamba naungana na Watanzania wote na Wabunge wenzangu kuyasifu, kuyaadhimisha na kuyapongeza mema yote waliyoyatenda viongozi wetu. Nataka niseme kwamba kwa imani yangu tunapaswa kumsema Marehemu kwa mema yake na sisi tunatimiza ibada kwa kuyasema mema ya Dkt. Pombe Magufuli kwa yale aliyoyafanya katika uhai wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua Dkt. Pombe Magufuli ni binadamu na hakuwa mkamilifu lakini hatupaswi kuyasema sasa kwani nafasi ya kujitetea hana tena. Kwa hivyo, nijielekeze katika kumpongeza kwa yale mema ambayo ametuachia na sisi tuko tayari kushirikiana na uongozi mpya uliopo kuyatekeleza kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata Rais wetu mpya mama Samia Suluhu Hassan. Binafsi niseme nina imani na mama Samia Suluhu Hassan kama walivyo na Imani Watanzania wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mola wetu Mtukufu alipoiumba dunia alimuumba Adam, kwa mujibu wa vitabu vitakatifu vinavyosema lakini akaiona dunia siyo mpaka alipomtoa mama Hawa ubavuni kwa Adam. Kwa hivyo, Hawa ana nafasi kubwa sana na ndiyo maana leo akina mama tunawapa nafasi kubwa hata kama sisi tumewatangulia katika uumbaji wake Mola wetu Mtukufu. Hebu leo tujiulize bila akina mama hii dunia ingekalikaje? Ingekuwa ni mtihani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mama Samia ameshika madaraka ya nchi hii ilianza kuonesha jinsi ambavyo atayadumisha yale mema ya mtangulizi wake. Pia tunaridhika na alivyotuonesha kwamba ni mama anayejiamini kweli kweli. Kwa hiyo, hatuna shaka hata kidogo na uongozi wa mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka niseme kwamba tumepata pia Makamu wa Rais miongoni mwetu kwa maana ametoka hapa ndani. Nimevutiwa sana na aliyoyaongea hapa, ameongea mambo mengi jinsi watakavyosimamia yale maendeleo waliyoyaanzisha pamoja na mtangulizi aliyekuwepo. Amezungumzia habari ya kuimarisha barabara, reli, maji, elimu na afya. Hayo ni mambo mema ambayo kila Mtanzania anatakiwa ayapongeze yalivyofanyika na walivyopanga kuendelea kuyatekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nataka nimuombe Mheshimiwa Makamu wa Rais huko aliko kama ananisikia, katika hotuba yake amegusia maendeleo ambayo wanatarajia kuyafanya. Nataka aweke highlight katika dondoo chache ambazo nitampa sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imeingia katika uchumi wa kati kwa jitihada zao na zetu. Sasa nataka kuiona Tanzania chini ya uongozi wao ikiingia katika demokrasia ya kati. Tutoke demokrasia tuliyonayo twende demokrasia ya kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namaanisha nini? Tunataka kuona uhuru wa vyama vya siasa unatekelezwa kwa vitendo. Tunataka kuona vyama vya siasa vinafanya kazi zake pasipo kubughudhiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka Makamu wa Rais aweke highlight Katiba mpya ni mahitaji ya Watanzania, sisi na wenzetu wa CCM. Siyo mahitaji ya wapinzani kama inavyodhaniwa na baadhi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ada ya mja kunena, muungwana ni vitendo, sisi waja tunapozungumza, waungwana onesheni vitendo. Katiba mpya haikuwa mahitaji ya Upinzani, Katiba mpya kwa mujibu wa ilipofikia tayari ilipitishwa, kilichobakia ni umaliziaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona fedheha sana kama mimi nilikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na tulipiga kura kuipitisha leo akitokea mwingine akisema kwamba si kipaumbele cha nchi hii, ni ahadi na zilitumika pesa za Watanzania ili ipatikane Katiba mpya kwenye nchi hii. Kwa hivyo namuomba Mheshimiwa Makamu wa Rais aweke highlight juu ya jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana uhuru wa vyombo vya habari. Najua upo na tunaposema haya si kwamba hayakuwepo unapodai leo barabara nzuri, siyo kwamba tulikuwa tukipita kwenye mapori, barabara zilikuwepo lakini tunataka barabara zilizoimarika Zaidi. Tunapozungumza tunataka uhuru wa vyombo vya habari siyo kwamba haukuwepo kabisa lakini tunataka uhuru uliomarika kweli kweli. Hatutaki uhuru ambao mwandishi akiandika jambo anafikiria usiku mzima…

T A A R I F A

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatibu, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah.

MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimpe Taarifa kaka yangu Mheshimiwa Khatib kwamba wakati tunapitisha Katiba Mpya Wabunge wa Upinzani waliikataa na wakatoka nje. Nashangaa leo wanavyong’ang’ania Katiba Mpya. Hawa watu wakoje, wanataka nini? Tulikuwa tunaipitisha wakaikataa, leo tumekubaliana, wanaitaka tena. Yote hiyo wanataka kutuvuruga, hatutoki kwenye reli ya maendeleo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khatib unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu dada yangu Munde. Mahitaji ya Katiba Mpya hayakuwa mahitaji ya Wabunge wa Upinzani, yalikuwa ni mahitaji ya Watanzania. Ninyi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa kuona yale ni mahitaji ya Watanzania ndiyo maana mliipigia kura ikapita kwa kishondo na mkacheza ngoma zote ndani ya Bunge hili. Kwa hivyo, kila tunalolikataa sisi kama na ninyi mnalikataa tuambiane kuanzia leo tujue hayo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuendelea. Katiba Mpya ni ahadi na tayari imepitishwa. Namuomba Mheshimiwa Rais ambaye naye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba aliangalie kwa jicho pana jambo hili kwa manufaa ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niligusia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari siyo kwamba haukuwepo, tunapoomba mambo kuboreka ni kwamba tunataka twende mbele. Uhuru wa vyama vya siasa sio kwamba haukuwepo, lakini tunataka zaidi uimarike. Leo tunakuwa marafiki wakati tunazungumza hapa ukifika wakati wa uchaguzi mnabadilika, mnakuwa sura nyingine, tunakwenda wapi? Tunataka mambo haya yaondoke kama alivyosema mama Samia na sasa twende kwenye nchi ya kistaarabu, tufanye siasa kistaarabu, anayeshinda ashinde, anayeshindwa ampe mkono, Tanzania iende mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili natoa wito kwa wale wenzetu wote wanaoisema vibaya nchi hii sasa warudi nyumbani mambo yamenoga. Wasikae huko kuipaka matope, mama Samia yuko. Gwajima amesimama hapa amesema Konki Fire, sasa nasema rudini tujenge nchi yetu, tunaambizana hapa, tunasikilizana hapa, tufanye mambo yetu kama Watanzania. Tuache kubaguana kwa vyama, leo tumepiga kura hapa haijapungua hata moja, kwa nini? Tunapowapa mkono wa aalan wasaalan, mtoe mkono wa aalan marhaba, sawa? Tusiwape mkono mbele mkashika panga nyuma, hatutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)