Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyenijalia afya njema hata siku ya leo nikawa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja zote mbili, kwa maana ya maazimio yote mawili; lakini pili nijielekeze kwenye azimio la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hayati aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli sisi, ulimwengu wa kimwili tunaona ametangulia mbele za haki lakini bado yu hai. Bado yu hai kwasababu matendo yake, aliyotutendea watanzania yatadumu milele. Na watu wenye vitendo vya namna hii, wenzetu waingereza wanasema immortality ni mtu ambaye anaweza kuishi angali amekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kazi kubwa ambayo mimi naomba nilishauri Bunge letu Tukufu; amefanya mambo makubwa ndani ya nchi yetu lakini kukumbukwa kwake kutakuwa ni jambo la msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda South Africa pale Johannesburg, utaona kuna mnara pale lakini pia kuna sanamu nzuri sana ya Mandela, wanapaita Mandela Square. Kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhamisha Makao Makuu yetu ya Nchi kuja Dodoma. Hapa Dodoma kuna eneo tengwa la Serikali na lina haki miliki maeneo ya Chimwaga; na Chimwaga tunafahamu kihistoria. Zaidi ya heka 100 zimetengwa pale kwa ajili ya recreational park, eneo la mapumziko. Niombe kushauri Serikali, ingefaa tujenge monument pale ambayo wajukuu, watoto wetu na kizazi kijacho kitakuwa kikisema Magufuli ni nani? Wanakwenda pale, na hii itatusaidia kumjengea heshima kubwa aliyotutendea Watanzania. Eneo lipo, zaidi ya heka 100 na lina hati ya Serikali na ni mali ya Jiji la Dodoma, kwahiyo hakuna mashaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kuzungumza haya nijikite kwenye eneo hili la Rais tuliyenaye Mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan. Waingereza wanasema, all starts well ends well, all starts well ends well, mama ameanza vizuri, ametuonesha Watanzania kwamba kazi anaiweza. Mfano mzuri leo hii tumeona jina hapa la Makamu wa Rais. Ukitazama unaona matarajio yetu Watanzania, kwamba sasa yale yote yalioachwa na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli yatakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema haya. Ukiangalia makamu wa Rais yeye amekuwa Waziri wa Fedha, lakini haitoshi, ni bigwa na mbobezi wa kukusanya mapato ya nchi haitoshi pia kubana matumizi. Kwahiyo hii chemistry ya Mheshimiwa Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Makamu wa Rais ni sawa na oxygen; yaani hydrogen mbili ukijumlisha, wale wana kemia ukichukuwa, ukichukuwa hydrogen mbili ukijumlisha na oxygen moja unapata maji. Kwa hiyo chemical reaction hii hatuna mashaka nayo, lazima maji yatapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nisichukue muda mrefu, itoshe tu kusema kwamba aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametubadilishia fikra Watanzania. Kuna watu tulikuwa tunaamini bila rushwa huwezi kupata huduma ya afya, lakini leo hii Watanzania tunaamini utapata huduma ya afya bila rushwa. Kuna watu tulioamini hakuna uwajibikaji ndani ya Taifa hili, lakini leo hii tunaona Taifa letu uwajibikaji umekuwa wa kutukuka na utawala bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nisiseme sana lakini itoshe tu kusema nionge mkono maazimio yote mawili. Ahsante sana.