Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Fedha na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa uwasilishaji wao mzuri leo asubuhi, kwa kweli mbinu waliyotumia kuwasilisha imefanya mpango wetu uweze kueleweka sio kwetu sisi Wabunge bali hata kwa wananchi, kwa hiyo, kwa niaba ya watu wa Sikonge nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu kwamba kwa niaba ya watu wa Sikonge nimeupokea Mpango uliowasilishwa leo asubuhi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa mikono miwili na kwa matumaini makubwa. Thatimini ambayo ameitoa hapa ya utekelezaji wa mpango uliopita unatoa matumaini kwamba Mpango huu wa Tatu utakuwa na mafanikio makubwa zaidi na nina sababu mbili za kusema hivyo. Sababu yangu ya kwanza ni kwamba utekelezaji wa mpango uliopita katika maeneo mawili hasa makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza, eneo la huduma za jamii, elimu, afya, maji kwa kweli tunahitaji kuipongeza sana Serikali na kuipa heko kubwa kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye eneo la huduma za jamii. Eneo la pili ambalo limetengezwa vizuri sana ni eneo la miundombinu kwa ajili ya kuhudumia uchumi, eneo la barabara, madaraja makubwa, vivuko, reli, umeme hasa umeme vijijini, maji, viwanja vya ndege na bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo hayo yalionesha mfano mkubwa, safi kabisa na ni mfano wa kuigwa kwa Serikali nyingi katika Bara la Afrika kuhusu matumizi mazuri ya fedha za umma. Maendeleo tuliyoyapata kwenye eneo la miundombinu, kwenye maeneo hayo niliyoyataja yamefanya Tanzania iwe sehemu muhimu, nzuri ambayo inawavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Mazingira ni mazuri, kwa hiyo kutokana na mafanikio ya hivyo nashauri Serikali ni vema tuendelee kusimamia vizuri utekelezaji kwenye maeneo yote hayo ili tuendelee kuwa bora zaidi na hayo ni maeneo ya vipaumbele vya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya CAG ya juzi kwa kweli inanifanya niiombe Serikali kupitia Waziri Mkuu na viongozi wote wa Serikali kwenye Wizara mbalimbali naomba sana taarifa ya CAG muipitie kwa kina ninyi ndugu zetu mliopo Serikalini ili muweze kuchukua hatua stahiki, sio hatua za kukurupuka hapana, hatua stahiki kwa kila aliyehusika na ubadhirifu ili tunapoenda kwenye kutekeleza mpango mpya tupate mafanikio makubwa kwa niaba ya wananchi wetu na kila mwananchi aweze kufurahi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mimi natangaza rasmi kwamba Halmashauri yangu ya Wilaya ya Sikonge ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zimepata Hati Chafu, hili mimi binafsi kama Mbunge wa Sikonge nawaambia wananchi wa Sikonge sijalifurahia na niomba mamlaka zinazohusika ziweze kufuatilia ili tusiwe na mambo kama hayo katika siku za usoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni na maeneo matano ya kushauri; eneo la kwanza, kwenye viashiria vya Taifa vya Uchumi kuna kitu kinaitwa mfumuko wa bei au inflation. Mimi ni mtaalam wa uchumi tena sio mtalaam wa hivi hivi, ni mbobezi kabisa kwenye eneo hilo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha anafahamu, hii habari ya kukaa tunatamba kama Taifa hapa unajua inflation yetu ni 3.5% sio kitu cha kujivunia sana, tunatakiwa kweli kuwa single digit, lakini ni single digit ambayo inasogelea 10% ili kuweza kuchochea faida za muda mfupi na faida za muda wa kati za wawekezaji na kwenye eneo la biashara, hii kuweka 3.5% na chini ya hapo ni kuufanya uchumi uwe dormant, sawa bei hazitabadilika sana, lakini je, uwekezaji? Je, biashara faida kwenye biashara itakuwaje? Kwa hiyo namshauri Waziri wa Fedha awaambie watalaam wasiwe waoga sana kwenye inflation hasa hii inflation ambayo iko chini ya 5% sio nzuri sana kwa Taifa ambalo tumeshatengeneza mfumo mzuri wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili; tunapozungumzia viwanda unataja maelfu ya viwanda, kweli na mimi nilikuwa Waziri wa Viwanda wakati fulani, nataja mafanikio, tumeanzisha viwanda 50,000; mimi kwangu binafsi mafanikio ni kwenye eneo la ajira, tume-create ajira kiasi kwenye sekta ya viwanda, sio kutaja viwanda 50,000 hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa viashiaria muhimu kabisa kwenye dira yetu ya Maendeleo ya Taifa tulisema kwamba ifikapo mwaka 2020 asilimia 40 ya ajira itatoka kwenye eneo la uzalishaji viwandani, kwa hiyo tunapotoa taarifa ya viwanda tulivyoanzisha lazima tuseme tumefikia hatua gani kwenye kufikia lengo la 40% ya ajira kwenye sekta ya viwanda, hilo ni la muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo na ningependa kulishauri maeneo ya utawala bora. Dira ya Maendeleo ya Taifa ina nguzo nne; nguzo ya kwanza huduma za jamii, nguzo ya pili umoja wa kitaifa, amani na usalama, eneo la nguzo ya tatu ni nguzo ya utawala bora halafu nguzo ya nne ni eneo la kukuza uchumi ambapo tunakuta na mambo ya infrastructure na nini. Hiyo ni kengele ya kwanza. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote hayo manne lazima eneo la umoja wa kitaifa, eneo la usalama na amani ya nchi lazima tulihudumie vizuri, lakini vilevile eneo la utawala bora lazima nalo tulihudumie vizuri, kwenye eneo la utawala bora kuna vi-section kumi ambavyo nilikuwa nafikiria kwamba niwashauri wenzetu waweze kuviangalia na kuviongezea umuhimu katika bajeti na katika kuisimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni ukaguzi na urakibu wa polisi. Tunazungumzia hapo utekelezaji wa Sheria Kuu ya Jinai na hii ni muhimu sana katika kulinda mali na usalama wa wananchi. Polisi naamini katika eneo hilo hawana bajeti ya kutosha. Lakini eneo la pili ni Ukaguzi wa, Ukaguzi wa ndio risk manager wa fedha tunazopeleka kule kwenye Halmashauri na kwenye Wizara. Kwa hiyo, Ukaguzi wa Ndani unatakiwa upawe kipaumbele cha juu sana. Halafu cha tatu ni Ukaguzi wa Nje naye CAG wakati mwingine anakuwa na hela kidogo, eneo la nne, Tume ya Kudumu ya Uchunguzi, eneo la tano, Tume na Sekretariat ya Maadili ya Viongozi, eneo la sita Usalama wa Taifa, hawa watu wa Usalama wa Taifa wakati mwingine wanakuwa na informers wengi kuliko hata wao wenyewe ambao wameajiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nashauri wale informers ambao wana uzoefu wawachukue waajiri ili kusudi Idara ya Usalama wa Taifa iweze kufanya kazi zake vizuri zaidi in a formalized manner.
Mheshimiwa Naibu Spika, la saba ni TAKUKURU hata Mheshimiwa Rais juzi aliwaambia TAKUKURU zingatieni sheria iliyoanzishwa TAKUKURU katika kufanya kazi zenu, sasa walikuwa wanaingilia na maeneo mengine ambayo wao hawahusiki. Lazima tuwajengee uwezo, tuwape watumishi wa kutosha ili waendelee kupambana na ufisadi na mambo mengine ya ubadhirifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la nane Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu hii inafahamika. Eneo la tisa vyombo vya kusimamia utoaji wa haki na eneo la mwisho kujenga umahiri wa viongozi kwenye ngazi za chini. Naomba nimalizie kwamba eneo hili la kujenga umahiri wa viongozi wa ngazi za chini kwa mfano Maafisa Watendaji wa Vijiji na Maafisa Watendaji wa Kata ni la muhimu zaidi kama tunataka tuendelee na vilevile kuwapa fedha TARURA nyingi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuunga mkono. (Makofi)