Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami kama wenzangu wote nianze kwa kutoa pole kwa Watanzania wote na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondokewa na Rais wetu kipenzi, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii nimpongeze Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kuwa mwanamke wa kwanza kuvunja na kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Nchi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Mwigulu kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kupewa Wizara nyeti; Wizara ya Fedha na Mipango. Hongera sana. Vile vile nampongeza kwa Mpango ambao ameuwasilisha leo yeye na timu yake yote ya waatalam pamoja na Mwenyekiti wake wa Bajeti. Kwa kweli inatoa matumaini ya Taifa letu, tunaenda wapi kiuchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita katika sehemu ya uvuvi na kilimo. Nikianza na uvuvi, Tanzania ni nchi iliyobahatika sana. Tuna maziwa ya kutosha, mito na bahari, lakini bahati hii bado hatujaitumia. Tumeenda na kudra ya Mwenyezi Mungu tu kuvua samaki walio ziwani na baharini; lakini kama tukijikita kwenye vizimba kufuga kitaalam Mheshimiwa Waziri atapata mapato ya kutosha na ugomvi kati ya Serikali na wananchi kwa uvuvi haramu utakuwa umekoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sehemu hii Serikali ijikite kutoa hela za kutosha, Wizara husika ndiyo itafute maeneo na kujenga vizimba. Vizimba hivyo wananchi wakodishwe kufuga. Nilikuwa napiga mahesabu, lakini mimi sio mtaalamu wa hesabu; ila tukiweka vizimba hivyo kila baada ya miezi sita tunavua Samaki, tena ambao siyo wa kupima na rula, kwa sababu amefikia kiwango kinachotakiwa. Vile vile hapa tutapata kodi, hapa tunawainua akina mama na vijana, watapata ajira kutokea pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi Jirani, Uganda nimetembelea mwenyewe vizimba vya akina mama. Mwanamama anakwambia kwa mwaka ana uwezo wa kutengeneza shilingi milioni 200 au shilingi milioni 15, lakini sisi Tanzania tumekaa tu. Naiomba Serikali, nakuamini Mheshimiwa Mwigulu na Waziri wa Uvuvi, tuchukue hatua, wakati ni sasa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba tunaukalia uchumi, nasi tumeukalia uchumi kwenye hili la uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wenyewe, ukiamua wewe mwenyewe kutafuta vizimba, kuna idara inaitwa ya Idara ya Mazingira; unaambiwa hapa mazingira hayafai, hapa hayafai, lakini kwa Waganda inafaa vipi? Tunakosea wapi hapa? Sasa sisi tunaiomba Wizara husika, yenyewe ndiyo ishirikiane na Idara ya Mazingira, wote ni Serikali moja, watuambie kwamba maeneo kama haya hamtaharibu mazingira, weka vizimba, fuga Samaki. Mheshimiwa Waziri utapata mapato ya kutosha pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri, kwenye bajeti ijayo Mheshimiwa Waziri tenga ruzuku, tupe akina mama na vijana tukaweke vizimba kule tukutengenezee mapato na tuinue uchumi wa Tanzania. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo, toka uhuru mpaka leo bado tuko kwenye kilimo cha jembe, hatujawahi kutoka hapo, lakini tunasema kilimo ndiyo uti wa mgongo, kilimo ndiyo asilimia 70 ya Watanzania tuko pale, kilimo ndiyo kinagusa kila Mtanzania, ndiyo tumekiweka mbali na Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri niko kwenye Kamati ya Kilimo. Tumetembelea miradi kama Kilosa, lakini ukiangalia kidogo kwenye sehemu ya umwagiliaji waliyoijenga pale na mazao yanayotoka pale na tumebahatika maziwa na mito ya kutosha, lakini bado hatujaingia kwenye kilimo cha umwangiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kilimo hicho tukiingia, mbegu hakuna. Kilio cha mbegu kimekuwa kikubwa sana. Hakuna mbegu za kutosha, hakuna wataalam wa kutosha, kwa hiyo, kwenye kilimo tunakwama hapo. Ushauri wangu tu, niishauri Serikali sasa ijikite kwenye kilimo cha umwangiliaji, lakini ijikite kabisa kwenye uzalishaji wa mbegu, tena ambazo ni za kiwango kwa kutumia utafiti, tutenge bajeti ya kutosha ya utafiti wa mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuhakikishe tunaajiri Wagani wa kutosha, hawapo. Leo hii kuna Kata nyingine zina vijiji 15 na mgani ni mmoja; lakini kwa sababu yuko TAMISEMI, wanamwambia utakaimu Utendaji wa Kata. Tumeyaona haya. Sasa Ugani anaufanya saa ngapi? Akishaenda kwenye Utendaji wa Kata, kule kuna kusimamia kuuza mashamba na kadhalika, Ugani anaacha, anaomba recategorization akawe Mtendaji wa Kata, tunawakosa Wagani namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado hata yule ambaye amejitahidi kulima yeye mwenyewe, masoko hakuna. Kuna kipindi ilitangazwa hapa zikalimwa mbaazi Tanzania kwamba zitaenda India, lakini matokeo zilipelekwa mpaka kwenye vituo vya shule kuwapikia wanafunzi, India hazikuwahi kwenda. Sasa tunakwama wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo na uvuvi, vitu hivi tukivishika, tukaviwekea mkakati kama tulivyoweka kwenye miundombinu ya barabara, Tanzania tutafika mbali. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)