Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Naomba nianze kwa pongezi. Wapo Mawaziri wanne ambao wamegusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ngara na ninapenda nitumie nafasi hii kuweza kuwapongeza. Naomba kumpongeza Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda na Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kugusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ngara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipomwomba Mheshimiwa Prof. Mkenda miche ya michikichi ndani ya siku saba, alituma watu wa TARI, walifika Ngara na kuotesha vitalu vya miche ya mchikichi. Ahsante sana. Nilipoomba miche ya kahawa, Mheshimiwa Hussein Bashe ndani ya mwezi mmoja amenipatia miche 300,000 na wananchi wangu wa Jimbo la Ngara wameshaipanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, speed hii ya Wizara ya Kilimo ni speed ya dream-liner naomba muweze kuindeleza. Vile vile, naomba nimpongeze Mheshimiwa Dorothy Gwajima pamoja na Mheshimiwa Godwin Mollel kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya na hasa kwa kufika kwenye jimbo langu la Ngara na kuhakikisha kwamba changamoto zile za ukosefu wa madawa wamezifanyia kazi na sasa zile simu nilikuwa ninapigiwa kwamba hakuna madawa kabisa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, zimepungua. Ahsanteni sana kwa kuja Ngara, naomba kazi mnayoifanya ya kuboresha huduma za afya muweze kuendelea nayo na mtu yeyote asiwakatishe tamaa, mimi na wananchi wa Jimbo la Ngara nipo pamoja nanyi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kumpongeza Mheshimiwa Maryprisca na Mheshimiwa Aweso kwa kuja Ngara pia kugusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ngara. Walikuja Ngara na wakati Mheshimiwa Maryprisca anafika pale, alikuja na barua mkononi ambayo ilikuwa na taarifa za kupewa kibali cha kuruhusiwa kujenga mradi wa maji mpya ambao unaenda kutatua matatizo ya maji kwenye Mji wa Ngara Mjini pamoja na viunga vyake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri hao waliogusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ngara, naomba niseme kwamba Wizara yote itakayotugusa kabla sijaendelea na mchango, nitakuwa nawapongeza hapa hivyo, nikija kuwaomba msaada kutokea Ngara Waheshimiwa Mawaziri, basi ujue kabisa kwamba ukinisikiliza haraka haraka utakula pongezi ndani ya hili Bunge. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye eneo la kilimo na ninaomba nichangie kwenye upande wa kilimo cha zao la alizeti. Mahitaji ya mafuta ya kula Tanzania kwa mwaka mmoja tunaitaji metric tani 400,000 mpaka 500,000 za mafuta ya kula. Uwezo wa kuzalisha mafuta ya kula kama Taifa ukijumlisha michikichi, alizeti na kadhalika, tunazaliza metric tani 200,000 mpaka 250,000 kwa mwaka. Hii inafanya tuweze kuagiza mafuta nje ya nchi kwa kutumia fedha za Kitanzania zenye dhamani ya Dola za Kimarekani milioni 80. Tunatumia fedha hii wakati Watanzania wapo na wana uwezo wa kulima alizeti na hayo mazao mengine tukazalisha mafuta ya kula hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania tuko tayari kuzalisha mafuta ya kutosheleza mahitaji ya Taifa. Wapo wakulima wa kutosha, wako wasindikaji wa mafuta ambao kwa Mkoa wa Manyara peke yake, nikitolea mfano, kuna viwanda vya kukamua na kusindika mafuta ya alizeti 234; na kwenye Jimbo la Ngara kipo kiwanda kimoja ambacho ni changu mwenyewe na chenyewe kina uwezo wa kuzalisha mafuta ya kula ya alizeti yanayotosheleza wakazi wa Jimbo la Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, changamoto kubwa inayofanya tushindwe kuzalisha mafuta ya kula ya kutosha, ipo kwenye upatikanaji wa mbegu bora ya kisasa. Taasisi za utafiti za Tanzania tulizonazo hazijawahi na sijui kama wana mpango wa kuanza uzalishaji wa mbegu bora ya alizeti aina ya high breed. Teknolojia wanayoitumia kwa sasa kuzalisha mbegu ya alizeti inaitwa Open Pollinated Varieties (OPV), maana yake wanazalisha mbegu yenye daraja la kati ambayo haiwezi kuzalisha mafuta ya kutosha kutosheleza mahitaji ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo, naomba nitumie nafasi hii kuweza kumwomba Waziri wa Fedha kufanya mambo yafuatayo; kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, mwana wa Nchemba, naomba utusaidie mambo yafuatayo: moja, Wizara yako isaidie kulinda viwanda vya ndani hususani vile vinavyomilikiwa na wasindikaji wadogo, viwanda vya kati na vile vidogo hususani kwa kuzielekeza mamlaka, hasa TRA kujitafakari inapokwenda kwenye viwanda hivi na kuviathiri kupitia makusanyo ya kodi kwenye usajili, lakini pia na kodi za ukaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia zipo mamlaka nyingine zinazoathiri viwanda hivi vidogo vidogo. NEMC, hitaji la kufanya Environment Impact Assessment ambalo linataka ukiwa na kiwanda uweze kutoa shilingi milioni 10, hiyo una- depots benki, umekopa huku kuanzisha kiwanda; hii nayo inatuathiri kwenye viwanda vidogo vidogo. Hivi vitu Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango viangaliwe ili athari inayopatikana kutokana na vitu hivyo ipunguzwe ili viwanda hivi viweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ni muhimu, ninaomba Vituo vya Utafiti vya Serikali vya Mbegu viwezeshwe ili vianze kuzalisha mbegu bora za kisasa. Narudia tena kwa msisitizo na herufi kubwa, VITUO VYA UTAFITI VYA SERIKALI VIWEZESHWE KUZALISHA MBEGU BORA ZA ZAO LA ALIZETI ZA KISASA MBEGU ZA HIGH BREED.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye soko, mbegu la zao la alizeti inanunuliwa shilingi 35,000/=. ukienda Mbeya Vijijini, ni mwananchi gani ana uwezo wa kumudu gharama hii ya mbegu shilingi 35,000/= kwa kilo moja? Hayupo! Ndiyo maana mimi kule kwenye Jimbo langu la Ngara nimenunua mbegu na nikatoa mikopo nikawagawia wakulima. Ninaomba watu wa kilimo waje wajifunze, tume-pilot na inaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ni muhimu sana ninaiomba Wizara ya Fedha iweze kusaidia Pamoja na Wizara ya Kilimo ni utolewaji wa mikopo ya mbegu kwa wakulima. Wakulima wawezeshwe kununua mbegu ili waweze kupanda zao la alizeti kwenye mashamba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya kawaida, mwananchi ana shamba lake amelilima, mbegu sokoni inauzwa shilingi 35,000/=, hata kama tukiwezesha kwenye Taasisi zetu za Utafiti, sidhani kama itashuka shilingi 10,000/=. Bila kumwezesha mkulima huyu kwa kumpatia mkopo aweze kununua ile mbegu na kupata nguvu ya kupalilia shamba zima na baadaye kuvuna, hawezi kulima mashamba makubwa kibishara. Hivyo wakulima wawezeshwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hayo mambo matatu tutakuwa tumepata faida zifuatazo: moja, tutawezesha Watanzania kupata mbegu za kutosha tena mbegu bora za zao la alizeti, ambapo endapo tutawezesha Taasisi zetu za Utafiti kuzalisha; na hii haina chenga chenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hatuwezi kutenga fedha za kuwezesha taasisi zetu zizalishe mbegu ya kisasa na badala yake tukawa tunasubiria Mataifa ya nje ambayo yana kampuni zao zinazozalisha mbegu za kisasa, wao ndio waje watuuzie, tena wanatupiga kweli kweli, kilo moja shilingi 35,000/=; bila hivyo tutakuwa hatujawatendea haki wananchi wangu wa Jimbo la Ngara, Shubi pamoja na Wahangaza na Wasukuma wa Nyamagoma pamoja na Wahaya wa Benagu. Tutakuwa hatujawatendea haki wananchi wa Dodoma wanaolima alizeti, Wagogo pamoja na wengine wa Singida, Wanyiramba na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, tutapunguza gharama ya kununua mbegu ya zao la alizeti sokoni iliyopo kwa sasa. Kama tutawekeza kwenye viwanda vyetu vya kuzalisha mbegu, tutawezesha upatikanaji wa chakula cha mifugo cha kutosha. Yale mashudu yanatumika kwa ajili ya kulishia mifugo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia.
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kabisa sekunde tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwekeza hivi kwa kuwezesha taasisi zetu tunaenda kuondoa tatizo la mafuta kwenye nchi yetu ndani ya kipindi cha miaka miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)