Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai wa kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Sambamba na hilo, naomba nikushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 hadi 2025/ 2026.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara husika, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote kwa kuandaa Mpango huu. Niwapongeze pia ndugu zetu wa Kamati ya Bajeti kwa kuandaa taarifa yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze moja kwa moja kwenye hoja ambayo ningependa kuizungumzia leo, miongoni mwa hoja hiyo ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji. Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumzia hili suala la kilimo cha umwagiliaji nami pia naomba nichangie kwenye suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kujengwa na kuboreshwa kwa miundombinu ya umwagiliaji kulingana na Taarifa ya Mpango kwamba kutoka hekta 461,372 mwaka 2015 hadi kufikia hekta 694,715 mwaka 2020 bado kilimo cha umwagiliaji kinahitaji kufanyiwa kazi ya ziada. Nilitamani tungepata maelezo kwamba hizi hekta 694,713 zilifikiwa kwa lengo lipi, kwamba je, Serikali ilikuwa imepanga kufikia lengo kiasi gani katika suala zima la kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu ambazo nimezifuatilia inabainisha kwamba tuna zaidi ya hekari milioni 29 ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, hadi sasa ambazo zimeweza kufanyiwa kazi yaani katika kilimo cha umwagiliaji ni hizi hekta 694,715. Leo ni miaka 50 na zaidi ya uhuru, kwa kweli kiwango hiki cha hekta hizi bado tuna safari ndefu sana kama tunahitaji mapinduzi ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomb nitoe rai kwamba tuone jinsi gani Serikali inajipanga vizuri kuhakikisha kwamba kilimo cha umwagiliaji kinawekewa uwekezaji mkubwa ili kusudi tuweze kupata chakula cha ndani ziada, mazao ya biashara na ili kusudi tuweze kuuza katika masoko ya nje. Leo nakumbuka asubuhi wakati Mheshimiwa Bashe akijibu swali la Mheshimiwa Timotheo Mnzava alizungumzia kwamba katika Mpango huu wana-plan kufikia hekta 1,200,000 za umwagiliaji. Maana yake ni kwamba hii labda inawezekana katika miaka mitano, lakini bado ina maana kwamba zitabakia hekta 27,800,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa bado naomba nitoe msisitizo kwamba hatuna budi sasa tuone mipango yetu ya Serikali tunafanyaje ili angalau tufikie hatua nzuri tuweze kujikomboa katika kilimo hasa kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba, Serikali haina budi kuona jinsi gani tunaweza tukaboresha hii miundombinu ya umwagiliaji lakini pia uhamasishaji wa Sekta Binafsi na wadau mbalimbali waweze kushiriki katika hili suala la kilimo cha umwagiliaji ili mwisho wa siku sasa tuweze kuwa na mapinduzi ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa sita wa Taarifa hii imezungumziwa kuhusu maabara ya mbegu katika Makao Makuu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo Morogoro. Hili jambo naipongeza sana Serikali, lakini pamoja na pongezi hizo nina ushauri kwamba, Serikali ione umuhimu kwamba kuna hii maabara ya mbegu lakini kuna kila sababu ya kuwa na maabara ya kupima udongo katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. Kama tutaweza kupima udongo, ina maana kwamba zile mbegu ambazo zitakazosiwa zitaendana na ule udongo kulingana na rutuba yake. Kwa hiyo mwisho wa siku ina maana kwamba mazao yatakayopatikana yatakuwa ni mazao ambayo yataleta tija. Kwa hiyo, naomba nitoe ushauri huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilisoma mahali nikaona kwamba, wenzetu Mkoani Kigoma walikuwa na mradi wa FAO, mradi ule ulikuwa ukiwaelekeza wakulima jinsi ya kupima afya na ubora wa ardhi. Sasa basi hebu Serikali ione itawezaje kuendesha huu mradi katika maeneo mengine ili wakulima waweze kupima ardhi na hatimaye waweze kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijatenda haki kama sitazungumzia suala la zabibu. Sisi katika Mkoa wa Dodoma zao letu ambalo ni mkombozi ni zao la zabibu, lakini katika mpango huu sijaona sehemu yoyote ambayo Serikali, imezungumzia kidogo sana katika taarifa ya kamati, lakini bado sijaona mkakati wa Serikali wa kuendeleza zao la zabibu katika Mkoa wa Dodoma. Jamani zao la zabibu ni utajiri katika Dodoma, zao la zabibu ni siasa katika Dodoma, lakini tatizo ni kwamba, zao la zabibu bado halina pembejeo. Mbegu ambazo zinatumika ni zile za miaka nenda miaka rudi kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali ione jinsi gani itakavyoweza kusaidia kukuza hili zao la zabibu ili ndugu zetu wa Mkoa wa Dodoma waweze kuondokana na suala zima la umasikini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi wamezungumzia kuhusu suala la mafuta. Na hasa wamezungumzia jinsi gani ya kuweza kuboresha mbegu za alizeti, mbegu za mchikichi, na kadhalika. Lakini basi hebu tuone kwamba, Serikali ijaribu kuangalia zaidi; kuna mafuta ya karanga, kuna mafuta ya ufuta, kuna mafuta yanayotokana na mifugo, vyote hivi najaribu kuona ili kusudi tuweze kupunguza utegemezi wa kupata mafuta kutoka nje.
Ninakumbuka miaka ya nyuma tulikuwa tuna mafuta ya pamba. Je, kwa nini Serikali isifikirie kuona umuhimu wa kuanzisha tena zile ginnery za mafuta ya pamba, ili kusudi tuweze kupunguza upungufu wa mafuta? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri sana hebu Wizara ione hilo, lakini jambo jingine kama muda utaniruhusu nilikuwa naomba nizungumzie kuhusu suala la afya. Kwenye suala la afya katika ule mpango wamezungumzia kwamba, vifo vimepungua kutoka 432 kwa vizazi hai laki moja. hadi sasa vifo vimekuwa 321,000 kwa vizazi hai laki moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kwamba, pamoja na kupunguza lakini hii namba bado ni kubwa. Tunatamani, yaani ndoto yangu natamani kama mwanamke nione wanawake hawafi kutokana na uzazi na hili jambo linawezekana. Kwamba, tukiwa na mipango kabambe ya kuhakikisha kwamba, wanawake hawa hawapotezi maisha yao tutapunguza mayatima na tutapunguza na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, wenzetu nchi ya Rwanda wameweza sana kujitahidi kupunguza vifo vya akinamama na watoto kwa kuwafuatilia kuona kuhakikisha kwamba, mwanamke au mama lazima kumfuatilia mpaka mwisho kuona anajifungua na anajifungua salama. Kwa hiyo, kama itawezekana na sisi tungeweza tukaweka program au kwa kufanya field visit, jinsi utakavyoiita, ili kusudi wataalamu wetu waweze kwenda kule, waweze kwenda kujifunza, kuona jinsi gani wenzetu wameweza kufanikiwa. Na naamini kabisa kujifunza ni jambo jema kabisa, mwisho wa siku na sisi inaweza ikawa vifo vya akinamama na watoto ikawa ni historia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa uchache niliona nichangie hayo. Baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, asante sana, nashukuru kwa kunipa fursa. (Makofi)