Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza niungane na hoja ya mwisho ambayo amezungumza Mheshimiwa Matiko kuhusiana na Bandari ya Bagamoyo, lazima ifanywe uchunguzi wa kina wa kimkataba ili kama mkataba uliopo huko kwa lugha ambayo hayati Magufuli alizungumza ambaye alikuwa ni Rais highest authority then. Kwa hiyo, niungane na wewe kwamba lazima kama Taifa, tutulie, tuweze kufanya uchambuzi wa kina, tuje na kitu kitakachosogeza Taifa mbele, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa nini, majuzi CAG kazungumza kuhusiana na ATCL, nimesoma hapa kuhusiana na usafiri wa anga, taarifa Mheshimiwa Mwigulu, anasema tulikuwa tuna ndege moja katika utekelezaji huu wa mpango, sasa hivi tuna 11, lakini tulivyokuwa ndege moja miruko ya ndege ndani na nje ilikuwa 225,000 mwaka 2015, maandiko ya Waziri wa Fedha. Tulivyokuwa na ndege 11 miruko imekuwa 292,105 ndani ya miaka mitano. Kwa hiyo tumetoka ndege moja kuja 11 katika kipindi cha miaka mitano tulichofanikiwa ni miruko yaani ndege kuruka ni elfu 67 pekee. Sasa vitu kama hivyi vinakupa swali ama tathmini ndogo tu. Naomba tuangalie abiria waliosafiri walitoka 4,207,000 mpaka 4268,000, ndege moja as against ndege 11, maandiko ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Sasa kama kulikuwa kuna walakini atakuja kuyasema yeye.

Mheshimiwa Spika, wakati tunahoji uwekezaji wa fedha kwenye shirika la ndege sio kwamba tulikuwa hatutaki shirika letu lifufuliwe, tulisema uangaliwe upungufu ambao umezungumzwa na wataalam. Wakati tunatoa fedha mara ya kwanza 2016, mara ya kwanza tumetoka kwenye ripoti ya CAG Utoh wakati huo, ameelezea masuala ya msingi zaidi ya 15 juu ya ubovu wa ATCL, akapendekeza yafanyiwe kazi kwanza, hatukuyafanyia kazi tukaanza ku-inject five hundred billion, miezi mitatu kabla ya taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Msajili wa Hazina akaenda akatoa taarifa PIC, akasema shirika hili hali ni mbaya, halina mpango wa biashara, kama uliandaliwa ulikuwa ni wa kukurupuka, haina mpango wa uwekezaji kama ulikuja kuandaliwa ulikuwa ni wa kukurupuka, halina mahesabu, halijafanyiwa mahesabu; hali ya shirika haijulikani kwa sababu hakuna ukaguzi wa kimahesabu uliofanywa. Tumezungumza hapa kama ndugu zangu kama nyie hapo wakapiga makofi wakasema hewala.

Mheshimiwa Spika, CAG Profesa Assad ripoti yake ya kwanza, huyu wa juzi amesema hasara ya miaka mitano, Profesa Assad ripoti yake ya kwanza baada ya kuteuliwa kuwa CAG alisema shirika limepata hasara kwa miaka kumi mfululizo. Sasa Waheshimiwa Wabunge, tukiwa tunapanga vitu kwa ajili ya Taifa hili, tuangalie namna njema ya kulisaidia. Leo hii ripoti ya juzi…

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa ipo upande gani? Sawa, nimekuona.

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, tunapokuwa tunajaribu kuangalia performance ya shirika la ndege mara nyingi sana huwa hatuangalii number of tourists ambao wamesafiri kutoka sekta moja kwenda sekta nyingine.

Mheshimiwa Spika, tunapojaribu performance ya shirika la ndege mara nyingi tunajaribu kuangalia amount of money which has been spends by the tourists katika sekta moja mpaka sekta nyingine katika kipindi cha mwaka. Kwa mfano, sisi Tanzania tunajua katika kipindi cha mwaka 2015 tuliweza, watu waliweza kuja na kutumia fedha walitumia fedha dola milioni moja, milioni mia tisa na ishirini na nne mwaka 2016 dola bilioni mbili milioni mia moja arobaini na tisa mwaka 2017 dola bilioni mbili, milioni mia mbili na sitini na tano elfu, mwaka 2018…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, sasa nilichotaka kuwa kusema ni kwamba tusije kupoteza Taifa…

SPIKA: Ahsante. Taarifa inakuwa fupi.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, ahsante.

SPIKA: Ahsante sana, nafikiri umeeleweka. Unaipokea taarifa Mheshimiwa Halima.

MHE. HALIMA J. MDEE: Tatizo la hawa manjuka, ndio maana nawaambia watulie, unajua ukiwa form one inabidi utulie kwanza. Nimesema hapa kwamba hakuna anayepinga shirika la ndege kufanyiwa ama kuwekewa fedha, hakuna anayebisha…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Musukuma.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, kuna kauli ameitumia Mbunge mwenzetu ya njuga, sasa sisi wengine tunatoka kijijini, sijui njuga ni nini, hatuelewi labda afafanune.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa…

SPIKA: Haina shida Mheshimiwa Msukuma unajua yeye ni darasa la saba, sasa hii lugha hawezi kuielewa kidogo. Endelea Mheshimiwa Halima.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru njuka ni form one, sasa Msukuma si unajua ameishia darasa la saba mwanangu. Kwa hiyo njuka ni form one, hukufika kule.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunachofanya hapa, ni kujaribu kusaidia yaani huwa nawaambia watu sisi ni Watanzania, tunaishi Tanzania, pasipo kujali umetoka chama gani, yaani vyama ni njia ya kusaidia Taifa, kwa hiyo tukizungumza tusionane maadui.

Mheshimiwa Spika, ninachosema taarifa ya Kichere ambayo watu wanajifanya wanaifanyia rejea na wengine kutoka huko sio mambo mapya. Yalizungumzwa CAG Bwana Utoh aliyazungumza, CAG Profesa Assad, tena Profesa Assad aliyazungumza kipindi ambacho ndio tumekuja hapa na Serikali inatuambia jamani tutenge bilioni mia tano, tunafufua ndege. Kazungumza hapa Mheshimiwa Aida, ni muhimu as a nation tuwe na vipaumbele vinavyo tu-guide ili CCM ikichukua sawa, ACT ikichukua anakuwa guided, CHADEMA ikichukua anakuwa guided. Sasa leo tunapanga kipaumbele kilimo, kesho Alhamdulillah Mheshimiwa Jenista anakuwa Rais, anakuja hapa anasema, mie nadhani nilikuwa napenda sana ndege nilivyokuwa mtoto, hapana. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tuweke kuji-guide, tutafanya mambo na kuweza kuyamaliza ndio hoja waliokuwepo wanajua kama sio wanafiki, suala la ndege halikuwa priority namba moja, you know it, tulikuja tu tukalichomeka, leo tunaambiwa trilion 1.2 zimemwagika, CAG anatuambia shirika lina madeni ya bilioni 412, this is…

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa nilikuwa ninaishauri Serikali na namshauri Waziri wa Fedha…

SPIKA: Mheshimiwa Mpembenwe tena, Mheshimiwa Halima kaa, kuna taarifa.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, pamoja na u-form one uliyepo, nataka kusema tu sisi Wabunge tusijekupoteza wananchi. CAG sisi ndio tumempa kazi na kazi tuliyompa ya kwenda kuangalia mashirika tofauti, hasara iliyokuwa imepatikana, naomba nimpe tu taarifa mzungumzaji ni kwamba, shirika ambalo lina-operate kwa hasara kubwa sana Afrika kwa sasa hivi ni shirika letu ambalo ni majirani zetu hapo karibu wa Kenya, lakini kwa nini hawapigi kelele kuna sababu.

Mheshimiwa Spika, kwenye economics kuna kitu kinaitwa complimentary goods. Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati amechukua maamuzi ya kununua ndege hizi tafsiri yake ni kwamba alikuwa anaenda ku-compliment na sekta nzima ya mambo ya tourism na ndio maana tourism sekta kwetu sisi imepanda sawasawa na watu wa Kenya tourism sekta ilivyokuwa imepanda japokuwa wanapata hasara. Ahsante sana.

SPIKA: Mheshimiwa Halima, pokea taarifa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Nafasi za uteuzi zimejaa. CAG ameambiwa aseme ukweli kulisaidia Taifa, CAG amesema shirika la ndege halifanyi kazi vizuri, lazima tuliangalie, tuangalie watu wameshauri nini, ndege zishakuwa hapa, hatuwezi kusema tukazitupe ama kuzichoma moto, tuangalie kwa makini tujirekebishe pale tulipojikwaa.

Mheshimiwa Spika, tunasema haya kwa nini? Unajua, nilikuwa nasikiliza hapa Wabunge wachanga, tunakaa tunajiaminisha eti miradi tunajenga kwa hela zetu za ndani my friend nchi yenu inakopa, kukopa sio tatizo, lakini kopa wekeza kwenye miradi ambayo…

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Namtafuata anayesema taarifa.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU Nipo hapa, Kingu.

SPIKA: Haya bwana endelea, Mheshimiwa Kingu.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango mzuri wa dada yangu hapa Halima, lakini naomba nimpe taarifa ifuatayo: -

Mheshimiwa Spika, most ya carrier za mataifa mbalimbali hasa kwa Afrika, kazi ya mashirika ya ndege mengi duniani ukisema ripoti za shirika linalosimamia mashirika ya ndege duniani, kazi kubwa ya mashirika ya ndege duniani ni kuchochoa uchumi mwingine, si lazima kutengeneza profit. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukienda na mentality ya kutegemea ATC siku moja itengeneze faida tukataka ku- discourage juhudi zilizofanywa za kufufua shirika la ndege tutakuwa hatulitendei haki Taifa la Tanzania. Natoa mfano, Kenya Airways mwaka 2016 na 2017 ilirekodi loss ya dola millioni 249, mwaka uliofuata wa 2018 wakapata loss kutoka dola milioni 249 kwa asilimia 51 zikaenda dola 97 milioni, hasara. South African Airways…

SPIKA: Malizia taarifa yako.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, South African Airways mwaka 2017 shirika la ndege la South Africa lili-accumulate loss ya dola milioni mia moja hamsini na tatu, lakini uchumi mwingine kwa mashirika haya ulikuwa unachochowewa. Naomba tusibeze juhudi za kufufua ATCL.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Ahsante kwa taarifa, nafikiri ataipokea taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Halima taarifa hiyo.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, ninavyomwona senior naye anaingia humohumo, unakuwa unaona kwamba naye dogo anataka kupotea.

Mheshimiwa Spika, ni hivi ndege tukianza kuzungumza katika zile ndege zilizo-park pale airport tukiuliza tu kati ya hizo nane zilizopo au 11, ngapi zinaruka tutaanza kupotezana. Wamenunua ndege, hawana business plan zina-park pale. Kwa hiyo ndege ziki-park kama hasara kama hii inazungumzwa, lazima mtoe justification kwa nini hasara kama hii inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tusitake kwenda huko wala tusipotezeane muda, wataalam waliochaguliwa na Rais wamesema tumekurupuka kwenda kudandia treni kwa mbele wakati hatujajiandaa, hilo ndilo tatizo. Inawezekana tungejiandaa, sisi tungekuwa ni mifano yaani Kenya ingekuwa inaturejea sisi, South Africa ingekuwa inaturejea sisi, yaani wewe unajivunia vipi kuanza kufanya rejea failures, yaani unajivunia vipi, kwa nini usijivunie kwamba umejipanga vizuri wale failures wanakutumia wewe kama rejea. CAG amezungumza, mama Samia amesema, CAG funguka, maana yake mama Samia kawaambia na nyie fungukeni, acheni unaa, tulisaidie Taifa.

Mheshimiwa Spika, deni la Taifa linakua kwasababu, kwa makusanyo wanayokusanya TRA tunaweza kufanya mambo makubwa matatu; tunaweza tukalipa deni lenyewe, tunapitisha hapa trilioni nane mpaka kumi, tunaweza tukalipa mishahara watumishi kwa mantiki ya wage bill; tunaweza tukalipa OC – matumizi ya kawaida ya ofisi ili watu waweze kwenda ofisini. Ukiacha mambo makubwa hayo matatu, TRA ama sisi kama Taifa kama kuna salio linabaki labda trilioni moja, tukijitutumua sana trilioni mbili. Kwa hiyo mkija kupitisha hapa trilioni 36 mjue kwenye 36, 22 ndiyo tuna uwezo nazo, 12 tunakopa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuzingatia kwamba miradi yetu ya maendeleo tunaendesha kwa mikopo ndiyo maana tunatoa mapovu hapa. Tufanye vitu vyenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninyi mnajua wakati Dkt. Magufuli anaingia mwaka 2015 – Mungu amlaze mahali pema peponi Mheshimiwa Rais – deni la Taifa lilikuwa 41 trillion. Now, Ripoti hii ya BOT ya Februari, 2021 deni la Taifa ni trilioni 71, public and private. Kwa mantiki hiyo – msije mkasimama hapa mkaanza kusema tunajenga kwa hela zetu, hakuna hela, tena tunakopa mikopo ya biashara. Kwa hiyo, kila jambo tukilipitisha hapa tulipitisha kwa wivu mkubwa kwa kuangalia kizazi cha sasa na kijacho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunivumilia. (Makofi)