Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Geoffrey Idelphonce Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

WAZIRI NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia ningependa kukukumbusha kwamba siku mbili/tatu zilizopita kulikuwa na mechi kule Egypt na hujatuambia matokeo yake. Labda utatupa taarifa ukipata nafasi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwanza ningependa sana kushukuru michango ya Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli ni michango ambayo imesaidia sana kutengeneza Mpango wetu wa Miaka Mitatu ambao ni Mpango wa Tatu wa Maendeleo; na kwa kweli michango yenu tumeichukua na tutahakikisha kwamba tunaifanyia kazi kwenye maeneo yetu ya kisekta, lakini pia kuboresha huu mpango.

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba uniruhusu niwataje baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia kwenye eneo la uwekezaji. Kulikuwa na Mheshimiwa Zuberi Kuchauka (Mbunge wa Liwale), Mheshimiwa Tarimba Abbas (Mbunge wa Kinondoni); Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa (Mbunge wa Biharamulo) pamoja na Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani (Mbunge wa Viti Maalum Ruvuma). Pia kuna Mheshimiwa Hassan Mtenga (Mbunge wa Mtwara Mjini); Mheshimiwa Simon Songe na Mheshimiwa Yahya Mhata, huyu wa Nanyumbu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kushukuru kwa michango yao lakini naomba nijielekeze kwenye kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge lakini pia na wananchi kwa ujumla, kwamba Serikali wakati wote imekuwa ikifanyakazi ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kwenye nchi yetu. Kama ambavyo mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge mwaka 1999 tulikubaliana kwamba tuunde Dira ya Maendeleo ya miaka 25 (2000 – 2025), tunaiita Tanzania Development Division 2025 ambayo ilianza mwaka 2000, mwaka uliofuatia. Tukawa na mipango midogo midogo ya kimkakati sasa kutekeleza ile Dira ya Maendeleo; na ni kwenye ile dira tulijipangia kwamba mpaka kufika mwaka 2025 tuingie kwenye uchumi wa kati, lakini pia tukiongozwa na sekta binafsi, lakini pia na tukiongeza uzalishaji wetu wa mazao kwa ajili ya kupeleka fedha nje, tuwe na fedha za kigeni nyingi. Pia shilingi yetu iweze kuwa imara, tuwe na mfumuko (inflation) ya single digit, ikiwezekana twende kwenye chini ya wenzetu kwenye eneo la Afrika Mashariki na SADC na tukajipangia mipango mingi ikiwemo kukuza ajira kwa vijana; sasa tunakuwa na mkakati midogo midogo ya kuweza kutekeleza hivyo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna reforms ambayo ndiyo nilitaka iwe hoja yangu kubwa. Kwamba tunafanya maboresho kila wakati kama Serikali kwa kupokea mawazo kutoka kwa wadau, lakini pia watekelezaji wa programu mbalimbali za kisekta. Kama mtakumbuka tulikuwa na Public Sector Reform Program ambayo iliunda Idara yetu ya Utumishi kipindi kile, lakini pia kuna Public Finance Reform Program, pia tulikuwa na Local Government Reform Program ambayo tumetengeneza hizi halmashauri kupitia hizo programu. Pia hata Legal Sector Reform Program tuliifanya wakati huo ili kuboresha sheria zetu ziendane na mahitaji yetu sisi ya kuwa na uchumi wa kisasa kuendana na malengo ya kwenye Dira ya Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye kuyafanya hayo tukatengeneza mikakati. Tulikuwa na mkakati mdogo wa miaka mitatu wa kupunguza umaskini lakini tukasema huu mkakati baada ya kupata maoni ya wadau tuupanue zaidi kwa kukuza uchumi na kuupunguza umaskini. Tulikuwa na MKUKUTA, MKUKUTA I na MKUKUTA II wa miaka mitano, mitano kama mtakumbuka. Kwenye MKUKUTA II tukaona sasa tuje na mpango tofauti kidogo, ndipo tukawa na huu Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano ambao Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete alizindua mwaka 2011/2012 mpaka 2015/2016 mpango wa kwanza ukilenga kuibua fursa za kiuwekezaji lakini pia kujenga miundombinu ili tuhakikishe kwamba tunajenga msingi mpana wa kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutekeleza huo mpango tukaja na mpango wa pili sasa wa miaka mitano mingine ambayo ni 2016/2017, 2020/2021 ambao ndiyo umekamilika, huu tukasema tujikite kwenye ujenzi wa viwanda, na ndiyo maana Serikali inaripoti mara kwa mara kwamba tumejenga viwanda zaidi ya 8,477 ambako vikubwa ambavyo tunaviona ni 210 kwenye nchi yetu, ambavyo vimetoa ajira za kutosha kwa vijana wetu, lakini kutengeneza mafungamano kati ya sekta ya kilimo na masoko kwa kuwa na viwanda katikati ili tuweze kuchakata bidhaa za wakulima, lakini pia kutengeneza immediate market (soko la karibu) la mkulima na kumuhakikishia mkulima soko la mazao yake.

Mheshimiwa Spika, lakini pia sisi kama nchi tukasema baada ya kupata mafanikio kwenye Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Mipango ya Maendeleo kupitia Long Term Perspective Plan sasa twende kwenye Mpango wa Tatu ambao unaishia 2025/2026 na huu mpango umejikita kwenye ku-consolidate na kuchukua yote yale ya nyuma, lakini pia na kuchukua yale ambayo hatukuweza kuyatekeleza au kuyaboresha ili tuweze kwenda mbele. Sasa kwa upande wa uwekezaji kuna mengi ambayo tumeyaona kuna mafanikio makubwa sana ambayo sana tumeyapata kipindi hiki cha miaka iliyopita kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano wa Kwanza na wa Pili.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye Mpango wa Tatu tumelenga kuongeza; moja, utekelezaji wa mipango ya kuboresha mahusiano yetu sisi na sekta binafsi na tutaongea hizi PPDs (Public Private Sector Dialogue) kwa kuwasikiliza zaidi wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kuweza kuboresha complaints handling; zile kero za wafanyabiashara zile tuwe na masikio mapana zaidi ili tuweze kuzisikia na kuhakikisha kwamba tunatekeleza yale ambayo wafanyabiashara wangetamani, kwa sababu wao ndio wazalishaji na wasambazaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kipindi hiki tunasema blue print ambayo imezungumzwa hapa tunaenda kuitekeleza kwa uhakika labda niseme hivyo. Tangu mwezi Mei, 2018 baada ya Baraza la Mawaziri kuridhia na pia ndani ya Serikali kuweza kuhamasisha wananchi uwepo wa blue print na wafanyabiashara tumeweza kutekeleza mambo mengi ikiwemo kupunguza tozo 273 kwenye eneo letu la kujenga mazingira ya biashara na uchumi. Lakini pia kama mnakumbuka tulikuwa na TFDA ambayo ilikuwa inafanyakazi ambazo zinagongana kidogo na TBS. Kwa hiyo, Serikali baada ya kupata ushauri kutoka kwa wadau ikiwemo Waheshimiwa Wabunge hapa Serikali ikaamua kuchukua eneo la chakula na vipodozi ikapeleka TBS na kuiacha TFDA kushughulika na madawa na vifaa tiba ndiyo maana inaitwa TMDA kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunatekeleza mipango yetu ambayo tumejiwekea kupitia blue print, lakini pia na maboresho mbalimbali ambayo tulianza tangu mwaka 2010 kupitia ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunaita maboresho, ambayo imetokana na kufuatilia na kutafiti juu ya ripoti ya IFC ya Benki ya Dunia ya Easy of Doing Business, kuna indicators kumi na moja ambazo zinatuonesha hatufanyi vizuri kulinganisha na nchi zingine duniani. Kila nchi inapigana na kukimbia kwahiyo tutajitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba tunatekeleza hiyo yale maboresho na kuwa na mazingira wezeshi zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nipende kusema tui le miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo imelengwa kufanywa na Serikali itafanywa ikiwemo Mradi wa Bagamoyo ambao Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa ameulizia. Serikali iko wazi kwenye hilo kwamba tulichokataa ni yale masharti tu ambayo hayakuwa mazuri sana kwa nchi yetu, lakini kwa kweli wakija tena wale wawekezaji au wakitokea wengine tukakaa chini tukaongea tukaja na masharti ambayo yana interest kwa nchi, Serikali haitapinga kwa sababu ule mradi ni wa kwetu Serikali, wala si wa wawekezaji ni wa kwetu sisi. Na kwa kweli hayo maeneo mbalimbali tumeshalipia fidia sehemu ya viwanda, sehemu ya logistics lakini pia na sehemu ya bandari tumelipia fidia kabisa yako chini ya mikono ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningependa kuwahakikishia Wabunge na kuwahakikishia wafanyabiashara jumuiya ya wawekezaji kwenye nchi yetu, kwamba Serikali itaongeza usikivu na kuhakikisha kwamba tunafanya kazi pamoja kuweza kuboresha mazingira ya biashara.

Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru sana na naunga mkono hoja.