Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Leo nitajitahidi kidogo nichangie taratibu ili angalau wote kwa ujumla hasa Wabunge ambao tumeingia ndani ya Bunge hili kwa awamu ya kwanza hasa Wabunge vijana, baada ya hapa ni imani yangu tutakwenda wote sambamba.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nichukue nafasi kukushukuru sana wewe binafsi kwa namna unavyoliongoza hili Bunge. Nachelea kusema maneno haya kabla ukiwa ndani ya Bunge hili na ukiwa ni Spika wetu sisi kama Kiongozi wa Bunge. Ukistaafu ukiwa ndani ya Bunge hili ndiyo nipate ridhaa ya kukushukuru kwa namna unavyotuunganisha sisi Wabunge ndani na nje ya Bunge. Pia namna ambavyo unajitahidi angalau kumpa Mbunge mmoja mmoja nafasi ya kusemea yale ambayo anatakiwa ayasemee kwa mustakabali mzima wa wananchi ndani ya Jimbo lake. Mwenyezi Mungu pekee ndiyo anaweza kukulipa hili, muhimu ni kukuombea uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, nichukue nafasi kumshukuru sana Waziri Mkuu kwa namna anavyotuunganisha sisi Wabunge na Serikali kama Mtendaji Mkuu wa Serikali. Pia nichukue nafasi hii kuwashukuru Mawaziri wote kwa namna ambavyo pamoja na changamoto walizozipitia hapa katikati wiki tatu zilizopita, lakini bado wamebaki imara wanatuongoza na sasa tunakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nichukue nafasi kumshukuru Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan. Namshukuru kwa namna ambavyo ameanza, lakini namshukuru kwa namna ambavyo ameanza na anasema kazi iendelee kutekeleza na kulinda yale yaliyokuwa yanafanywa na pacha wake Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Ametuonesha sote kwamba njia bado iko pale pale. Yale waliyokuwa wanayasimamia juu ya wananchi maskini, miradi ya maendeleo, juu ya utendaji mkubwa wa Serikali kwa ujumla wake, bado ameahidi kuyasimamia na sasa tunaona kazi inakwenda vizuri. Ndugu zangu Wabunge tuendelee kumwombea mama yetu ili aendelee kufanya yale mazuri kwa kadri ambavyo Mungu ataweza kumwongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi sasa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa mujibu wa Taarifa ya Shirika la Kifedha la Kimataifa la IMF mwezi Januari, kutokana na ugonjwa wa corona IMF ilikadiria uchumi wa kidunia utashuka kwa asilimia 3.5 kulinganisha na 2.8 ya mwaka 2019, lakini Serikali yetu juu ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakishirikiana na pacha wake, mimi namwita pacha mama yangu, mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu hakuna namna unaweza ukazungumza mazuri yaliyokuwa yanafanywa na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli bila kumgusa mama Samia Suluhu Hassan. Hakuna namna unaweza ukazungumza mazuri yaliyokuwa yanafanywa na hawa watu wawili bila kumtaja Waziri Mkuu kama Mtendaji Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo niseme, kwa namna ambavyo walituongoza pamoja na kushuka na kuyumba uchumi wa kidunia pato letu la Kitaifa la ndani ya nchi liliongezeka kwa asilimia 4.7. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana, Wabunge waliokuwa humu wanajua changamoto ilivyokuwa hasa baada ya tikiso hilo la ugonjwa wa corona, walibaki imara wakawasemea wananchi, sasa haya ndiyo matunda yake ambayo wanayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye hotuba hiyo hiyo ya Waziri Mkuu. Taasisi ya Utafiti wa Kilimo kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, imejipanga sasa kufanya utafiti wa kilimo wa kuangalia namna gani sasa tunaanza kubuni mbegu bora na miche bora kwa mustakabali wa wakulima wa nchi yetu. Nina mambo mawili au matatu ya kushauri.

Mheshimiwa Spika, watakapokuwa wanafanya utafiti huu, waende sasa wakatazame namna gani wanafanya utafiti kwa ngazi ya kimkoa, wilaya na halmashauri, washuke chini ngazi ya kata mpaka vijiji ndani ya nchi nzima, ili mwisho wa siku waje kulingana na jiografia ya kila eneo ni zao gani moja linafaa kulimwa kama zao la kibiashara.

Mheshimiwa Spika, pili, utafiti huo ujikite katika maeneo gani ambayo yanaweza yakalimwa na yakafanyika kilimo cha umwagiliaji na yakawanyanyua wananchi kwa ujumla kwenye kipato chao kwenye maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, tatu, waende wakafanye utafiti warudi kushauri ili angalau sasa kwenye kila wilaya tuwe tuna zao moja la kibiashara ambalo wilaya moja ikisimama inasema ndani ya wilaya yangu, zao fulani ndiyo zao la kibiashara ambalo kimsingi kama Mbunge nikitaka kuwashika mkono kuwasaidia wale wananchi mbegu nawasaidia mbegu ambayo wanajua wakiipanda kama zao la kibiashara itainua uchumi wa wananchi kwenye maeneo yao husika.

Ningetamani sana, tafiti hizi ninaporudi ndani ya Jimbo langu kwenye wilaya nione kwamba kweli hapa kwenye kata fulani ndani ya kijiji Fulani, nikiwashauri wananchi kulima pamba inastahimiliki na isiwe kwa ku-guess au kwa kuchukua yale maoni ya wakulima peke yake, badala yake, niweze kuitoa hata kwenye taarifa za utafiti huu utakaokuwa umefanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, hapo hapo kwenye kilimo ningetamani sana, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Waziri wa Kilimo kwa namna ambavyo amejipanga kupeleka pikipiki kwa Maafisa Kilimo wote ndani ya halmashauri. Wasiishie hapo tu, ningetamani waende moja kwa moja, watengeneze mustakabali mzuri wa kuwasimamia Maafisa Kilimo ili Afisa Kilimo anapoamka asubuhi, ajue ni mashamba mangapi anakagua kwa siku, ametembelea wakulima wangapi, anategemea kupata nini kwa wale wakulima. Mwisho wa siku wampime kwa product inayopatikana kwenye ngazi ya chini kabisa, ngazi ya Kijiji, itakayoleta tija, lakini itaamsha ari mpya ya utendaji wa Maafisa Kilimo kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, natamani sana Wizara ya Kilimo pamoja na kwamba tunawapelekea vitendea kazi, tufike tutengeneze assessment nzuri ya kuwasimamia ili ninaposimama hapa kama Mbunge, yakitajwa maeneo mengine, nami nikitaja kama Rorya nataja mazao fulani ambayo wananchi wangu wameyapata kwa mwaka mmoja kwa kilimo walichokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo nizungumzie kuhusu huduma za kijamii na nitaanza na maji. Nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru sana Waziri wa Maji. Nasema ni katika Wabunge wachache ambao baada ya yeye kupata uteuzi alifanya ziara kwenye jimbo langu. Kulikuwa na Mradi wa pale Shirati, mradi ulikuwa na zaidi ya miaka 10 hautoi maji, lakini alipofika alitoa maneno ndani ya mwezi mmoja, ninavyozungumza chini ya Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi, leo kuna maji yanatoka pale. Unaweza ukaona ni historia gani ndani ya miaka 10, wananchi wale walikuwa wamesahau issue ya maji, leo wanapata maji.

Mheshimiwa Spika, sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri pale imepelea kiasi cha kama milioni 300, najua hili unaliweza, tusaidie ili tuweze sasa isiwe Shirati peke yake badala yake na majirani wote wanaozunguka kata ile waweze kupata maji kwasababu, miundombinu ipo ni kuifufua tu iweze kuwasaidia wananchi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna miradi ya maji ambayo iko ndani ya jimbo. Nichukue nafasi hii kukuomba kuna miradi ya Nyarombo, kuna miradi kwa muge pale Kyang’wame na miradi mingine ambayo kimsingi ukiwekeza fedha pale itawsaidia sana wananchi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri tusiishie mradi mmoja, turudi tuone namna gani ya kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niliwahi kusema na nitarudia tena, ili kutatua changamoto ya maji ndani ya Jimbo ni lazima twende na ule mradi mkubwa wa maji ambao upo kwenye plan ya kutoa maji Rorya kwenda Tarime. Ule mradi tunazungumzia zaidi ya kata 28 zitanufaika na ule mradi na kwa sababu, jimbo langu zaidi ya asilimia 50 changamoto kubwa ni maji ni imani yangu huu mradi ukiingia kwenye pipeline ukaanza kutekelezwa Rorya issue ya maji itakuwa ni historia. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu mkubwa sana na kwa sababu limesemwa na Waziri Mkuu ni imani yangu litafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe, ni imani yangu kipindi mlikuwa mnatunadi sisi Wabunge vijana, Wabunge ambao tumeingia kwa mara ya kwanza, mlikuwa mnazunguka wewe, Spika, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mama yangu Mama Samia Suluhu Hassan. Ulipopita kwenye jimbo langu uliniahidi namna gani tunaweza tukapata ambulance, ili angalau iweze kusaidia wale wananchi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hili tusaidie.

Mheshimiwa Spika, la kumalizia la mwisho nimalizie kuhusiana na issue ya TARURA, tuna daraja pale la Mto Mori, kwa sasa hivi kwasababu nimemuona Waziri wa TAMISEMI amekuja mama na lile daraja tunazungumzia kipenyo ambacho hakizidi hapa na Mheshimiwa Waziri alipo upana wa lile daraja. Ni imani yangu kwasababu limekuwa likizungumzwa zaidi ya miaka 10 huku nyuma sasa amekuja Waziri ambaye ni mama na ninaamini ni mchapakazi mzuri sana wanaoteseka kuvuka kwenda kutafuta huduma za kijamii, huduma za hospitali, huduma za masoko ni akinamama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na niliwahi kusema mto ule watu wamekuwa wakifariki pale. Angalia kipenyo tunachohitaji daraja ambalo tumekuwa tukiliomba kwa miaka 10 ni hapa na pale alipo Mheshimiwa Waziri. Ni imani yangu sasa amekuja mama atawasaidia hawa wamama ili lile daraja sasa badala ya kila mwaka kufanyika upembuzi yakinifu liweze kupata suluhisho la kudumu ili hawa wananchi sasa waweze kuokoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia la mwisho kabisa nizungumzie kwenye sekta ya afya kwenye upande wa Waziri.Ndani ya jimbo langu nina kata 26 ni kata tatu tu ambazo zina vituo vya afya na bahati mbaya sana Kata ya Kinesi ambayo ina Kituo cha Afya cha Kinesi kwa mujibu wa projection ya Wizara ilitakiwa ihudumie vijiji viwili peke yake. Hivi ninavyozungumza kituo kile cha afya kinahudumia zaidi ya vijiji 27 zaidi ya tarafa tatu wanapata huduma tena mpaka Kijiji Jirani cha Butiama, watu wanaokwenda pale projection yake imekuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, na kwasababu kimeshapanuka na Serikali ilitupa fedha tukakipanua zaidi ya milioni 500 hapa kilipofikia nichukue nafasi hii kumuomba sana Waziri tuone namna gani sasa tunakihamisha kwasababu, kimeshatoka kwenye vigezo vya kutoa huduma kama kituo cha afya kiende kiwe hospitali ya wilaya ili angalao tuweze kuwa na hospitali ya wilaya kwa ukanda wa chini upande wa Suba. Na hii hospitali ya wilaya ambayo Serikali ipo kwenye mchakato wa kuifungua upande wa pili maana yake tutakuwa na hospitali mbili, angalau kwa jiografia ya jimbo langu lilivyokaa tunaweza tukawasaidia sana wale wananchi kwenye sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya haya machache nichukue nafasi hii na niseme kwamba, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)