Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Gairo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kwa kuwa mmoja wa wachangiaji katika hoja ya Waziri Mkuu, lakini leo mimi nitachangia kwa upole sana na kwa ushauri tu angalau kidogo.
Mheshimiwa Spika, labda watu wengi hawajazungumzia au Wabunge wengi wapya lakini hawajaiona athari ya TARURA na RUWASA kwenye Wilaya zetu.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia muundo wa uliounda RUWASA na TARURA mimi sina shida nao sana na wala sina matatizo na Mameneja wangu wa Mkoa, mimi natoka Mkoa wa Morogoro wala wa Wilaya ya Gairo, wapo vizuri kabisa. Lakini ukiuangalia ule muundo unapishana kabisa na Katiba, Ibara ya 145 na 146 iliyoweka mamlaka kwa umma katika kuamua mambo yao katika Sheria za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia leo wakati inaundwa TARURA ilikuwa kama technical agency, lakini sasa hivi yenyewe ndio imekuwa na mamlaka ya kila kitu. Utakuta Meneja wa TARURA wa Wilaya hawajibiki kwa chochote katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo linapokuja sasa, kwa hiyo, Diwani amechaguliwa na wananchi kama mwakilishi kwneye Kata yake, na yeye naye ana maswali ya kuulizwa habari ya RUWASA kuhusu maji na ana maswali ya kuulizwa kuhusu barabara za TARURA, lakini anakuwa hana majibu ya aina yoyote. Na watu wa TARURA kwa mamlaka waliyopewa wao wanaamua barabara watengeneza ipi bila kushirikisha Baraza la Madiwani wala Mbunge na ukiona Mbunge kashirikishwa basi ujue hiyo ni hisani tu, umekaa naye vizuri Meneja wako, mnashirikiana, lakini akija Meneja kichaa na wewe ataamua kupeleka barabara kwa hawara wake na ya kwako ya kimkakati isipelekwe. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ipo sehemu hata kwa Mheshimiwa Kakunda pale Meneja wa TARURA kapeleka barabara guest kwake.
Mheshimiwa Spika, nilizungumza nyuma kidogo lakini sikupata nafasi ya kuichambua zaidi. Mama Samia juzi amesema kabisa sasa TARURA mtashirikiana na TAMISEMI, lazima sasa TARURA na RUWASA wa maji kwenye menejimenti zao sina shaka nazo, fedha zao wanavyokaa nazo na technical zao sina shaka nao, waendelee hivyo hivyo, lakini mipango mikakati yote ya bajeti ianzie kwenye Halmashauri za Wilaya. Barabara za kutengeneza zitoke pale kwenye Baraza la Madiwani, visima vya maji au maji yanatoka na kwenda wapi na kwenda wapi yaanzie kwenye Baraza la Madiwani, wao wawe watekelezaji, watoa fedha na mambo mengien yote. Lakini utakuta bajeti wanapanga, wanarudishiwa, hawasemi zimekuja shilingi ngapi, wanaanza wao, wewe una barabara ya kimkakati huku ina watu 10,000 wao wanaenda kutengeneza barabara ya watu 500.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili jambo tusipoliangalia kwa kweli hawa TARURA na RUWASA wanakuwa sasa ni Mungu mtu kwenye Halmashauri, na ukiangalia na jiulize huyu Mkurugenzi wa Maendeleo sasa anafanya kazi gani kama anashindwa kumdhibiti Meneja wa TARURA au Meneja wa RUWASA Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya ni ni sasa, si mkitoe tu hicho cheo na mtupe sisi Wabunge tuwe Wabunge na Wakurugenzi wa Maendeleo.
SPIKA: Kwanza nikuongezee Mheshimiwa Shabiby, hao Mameneja wa TARURA na RUWASA wana mshahara kuliko huyo Mkurugenzi wa Maendeleo, yalivyo mambo ya ajabu.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Sawa kabisa na nalifahamu hilo.
SPIKA: Kamkurugenzi tu ka-TARURA yaani, tayari.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aliangalie hili, hawa watu warudi na wawajibike, hivi leo TARURA anatengeneza barabara, RUWASA anatengeneza maji, halafu Diwani kupitia Baraza la Madiwani haruhusiwi kwenda kukagua, yaani anatengeneza yeye, anakagua yeye na yeye ndio kaamua, sasa Diwani anafanya kazi gani, Diwani leo kabakia na madarasa na zahanati. Sasa Diwani ana kazi gani na Mkurugenzi wa Maendeleo ana kazi gani kama anashindwa kumdhibiti TARURA na RUWASA? Tunaomba lirudi hili suala, menejimenti na fedha zibaki kwao kama mnasema Madiwani wanafuja fedha, lakini lazima wawajibike pale na akifanya vibaya baada ya ukaguzi wa Madiwani; Madiwani wawe na amri ya kusema huyu hafai. Nataka niseme na sisi Wabunge tukiwa kule kwenye Wilaya zetu na sisi ni Madiwani.
Mheshimiwa Spika, cha pili tunatafuta hela kila siku za TARURA, lakini wewe ni shahidi na Waziri Mkuu ni shahidi, aliyekuwa zamani Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kabla hajawa Waziri Madini Mheshimiwa Doto Biteko ni shahidi. EWURA kila lita moja ya mafuta tunayoweka wanachukua shilingi 17 mpaka 16 kila lita moja ya Mtanzania, hata jenereta ukiweka wanachukua fedha, kisingizio wanasema tunaweka vinasaba kwenye mafuta. Vinasaba kwenye mafuta zimeleta mzozo, wewe umevunja Kamati ya Nishati na Madini, na walikuja hata kwako wakusomeshe ukawafukuza. Ndio mjue kule kuna wezi, kuna baadhi ya Wabunge hapa walikuwa wanakula rushwa nje, nje, tena mkinikera nitataja, ila basi acha leo ninyamaze, kwa sababu ya kutetea huu wizi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, sasa leo mkataba kwa yule mwekezaji kwa mwezi anachukua zaidi ya shilingi bilioni tano, ambapo kila mwezi tungejenga hospitali moja.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nadhani allegation aliyotoa kwamba Bunge limekula rushwa ni allegation kubwa, mimi ningeomba tu kama wapo waliokula rushwa wawataje ili wengine tubaki na heshima zetu. (Kicheko)
SPIKA: Hilo nalikataa. Mheshimiwa Shabiby endelea. (Kicheko)
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, hiyo nimetoa onyo, sasa hivi wapya hamjala. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, lazima tuliangalie, tunao TBS ambao ndio kazi yao, kwa nini wasipewe hii tender na TBS wanachukua fedha kutoka sehemu tofauti. Hii fedha shilingi 17 tuipeleke TARURA ili TARURA wafanye kazi vizuri zaidi. Profesa Muhongo pamoja na kuchambuliwa na Mheshimiwa Musukuma hapa lakini alishawaita, wakati ule ulitoa amri kwamba wafanyabiashara tukutane na Profesa Muhongo, EWURA walishindwa kujibu. Kwa sababu waliitwa watu wa TRA, watu wa TRA wakasema sisi tunadhibiti mafuta yetu, tunajitosheleza kwa asilimia 100. Kwa sababu kama gari ya transit inaenda Rwanda au Burundi tunaweka king’amuzi, tunaiona gari kila kona mpaka inafika.
Mheshimiwa Spika, nakumbuka mimi wakati ule EWURA inaanzishwa ilikuwa watu wasichanganye mafuta ya taa na dizeli na mafuta ya taa na petroli ndio lilikuwa lengo. Mimi ndio nilikuwa Mbunge pekee niliyeongea miaka mitatu hapa mpaka mafuta ya taa yakapanda bei, niliyechakachua nikashinda wao wakahama, wakaona ulaji huku umeisha, wakahamia sasa tunadhibiti transit na mafuta ya kawaida, ilimradi tu ulaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na yule jamaa anachukua five to seven billion per month. Huyo agent/mkandarasi aliyepewa kuweka hiyo.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, huyu GFI anachukua shilingi 14 kwa lita, halafu kuna tozo zingine zote zilizopo pale sasa hivi zinafika shilingi 90; fedha inayotumika kwa siku kwa lita milioni 12 zinazouzwa ni shilingi bilioni moja na elfu themanini kila siku ya Mungu, kwa mwezi ni shilingi bilioni 32.4.
Mheshimiwa Shabiby endelea, tunapigwa vya kutosha. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yake ni nzuri sana.
Sasa hizo fedha zote zikichukuliwa na kupelekwa TARURA hatujapata mtaji? Na tukiongeza....
SPIKA: Yaani ni kutumbukiza tu hicho kinasaba tu hivi halafu ndiyo mabilioni yote hayo?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
SPIKA: Na taasisi ya Serikali hiyo TBS hawezi kuwa unanyunyiza hiyo? Endelea Mheshimiwa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, nataka nikuambie kwanza mimi namiliki vituo vya mafuta.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri afadhali, Mheshimiwa Kalemani.
T A A R I F A
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge lakini pia nimpongeze kwa hoja hii na tumeshatoa taarifa katika Kamati yetu kuwa ile kampuni inayofanya vinasaba tumeshasitisha mkataba wake na wala haifanyi kazi hiyo. (Makofi)
Kwa hiyo yale maeneo mengine nadhani yanaweza kuendelea kujadiliwa lakini la vinasaba tumeshasitisha na nimetoa maelekezo kuwa kazi hiyo ifanywe na Taasisi ya Serikali ya TBS. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa hiyo.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri ahsante sana, tungekuwa na taarifa hiyo mapema ingetuokolea muda. Tunakushukuru sana na tunaishukuru sana Serikali.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Taarifa yake siipokei kwa sababu bado ipo na huyu niliyekaa naye hapa ana kampuni ya mafuta na leo wameweka. Sasa umesitisha mkataba huku unaendelea? Kwa naomba ukasitishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nililalamika kipindi fulani hapa Bungeni wakaniandika kwenye gazeti, walikuwa wahonga mpaka baadhi ya magazeti, wakaandika Mbunge wa Gairo ni mwizi wa mafuta tunamdhibiti wakaja hawakuweka vinasaba kwenye mafuta yangu na mimi nikawafanyia timing gari sikushusha nikaenda kuchongea kwa Waziri Mkuu, ndio wakakimbia, Waziri Mkuu akanambia andika na nikaandika, kwa hiyo wizi wote unafahamika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba hawa watoke kwa sababu wameshakula fedha ya nchi siku nyingi, huyu Mheshimiwa Doto aitwe hapa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye sasa ni Waziri wa Madini alikuja kutishwa na mtu mkubwa kwa sababu wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Madini alishikilia kidedea, akaja kutishwa mtu wa juu kabisa, akaambiwa wewe dogo tunakupoteza sisi ukiendelea kufuatilia hii kitu. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Waziri nimekaa na wewe zaidi ya mara tatu lakini kila nikikueleza nilikuwa naona hunielewi, sasa nikaona napoteza muda wangu, kila nikimwelewesha. Hivi wewe unawekewa kitu, kwa mfano mimi nakodisha gari ya Mheshimiwa Shangazi, Mheshimiwa Shangazi anamtuma dereva wake aende depot anapakia mafuta ya Shabiby halafu dereva anawekewa mkojo wa punda anaambiwa hii ndio kinasaba hata haujui, halafu wewe unakuja kupima kwangu mimi, hapo uhalali upo wapi? Halafu hainekani kwenye rangi, wala haionekani kwenye chochote, wote ni upigaji tu, shilingi bilioni saba, bilioni sita na mpaka bilioni 30 alizosema Mheshimiwa Mbunge pale.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Utaratibu umeshaisha. Nimeshamaliza. (Makofi/Kicheko)