Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami pia napenda niungane na Watanzania wenzangu kutoa pole kwa kumpoteza kiongozi wetu Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Pia nichukue nafasi hii kusema pamoja na kwamba tuko kwenye majonzi makubwa lakini tutaendelea kumuenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameifanya na ametuachia. Pia najua kazi sasa inaendelezwa na Mheshimiwa Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa hiyo, nichukue nafasi hii pia kumpongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee masuala matatu. Kwanza, nitaanza na vitambulisho vya wazee wetu ambavyo tumewapa kwamba wanapofika hospitalini waweze kuhudumiwa kwa sababu wenyewe ni wazee na wana miaka 60. Hivi vitambulisho kwa sasa havifanyi kazi, wazee wengi wamekuwa wakienda katika hospitali mbalimbali, siyo tu kwenye Mkoa wangu au Jimbo langu, sehemu mbalimbali wanaambiwa kwamba dawa hakuna.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niiombe Serikali kwa sababu hii imekuwa ni changamoto sisi Wabunge tunapoenda kufanya mikutano sehemu mbalimbali tunakutana na changamoto hizi, wazee wanalalamika kwamba wana vitambulisho lakini hawahudumiwi. Kwa hiyo, naomba niiombe Serikali kwamba kama inaweza kusitisha hivi vitambulisho au inaweza kuwapa hivi vitambulisho na ikawapa waweze kupewa dawa basi ifanye hivyo kwa sababu hivi vitambulisho vimekuwa tu kama picha yaani hawawezi kuvitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linafanana na hilo ni kuhusiana na akina mama wajawazito wanapokuwa wanaenda hospitalini kwa ajili ya kupimwa au kufanyiwa huduma mbalimbali hawapati zile huduma, wengi wao wanaambiwa watoe pesa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kuliangalia suala hili ni kwa nini jambo hili linatokea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka niongelee, ni kuhusiana na issue ya fidia mbalimbali kwenye Majimbo yetu ambapo wananchi wametoa maeneo yao kwa sababu ya kuiachia Serikali ili iweze kupitisha miradi. Katika miaka yangu mitano kuanzia 2015 mpaka 2020, nimekuwa ninaongelea jambo moja la fidia ya wakazi wa Kipunguni, Kata ya Kipawa ambao wameiachia Serikali Uwanja wa Airport. Leo ni miaka 24 wakazi hao hawajalipwa pesa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 wakati Mheshimiwa Naibu Waziri akiwa Mheshimiwa Kwandikwa aliongea hapo kwamba kuna bajeti imepangwa kwa ajili ya kuwapa wale wananchi fidia yao lakini haijawahi kutoka mpaka leo. Hawa wananchi wametoa maeneo yao kwa miaka 24 na mpaka sasa hivi maeneo yao mengine yapo tu hawawezi kuyaendeleza, hawawezi kufanya kitu chochote cha wenyewe kujipatia kipato, nyumba zao tayari Airport wameshakuja kuweka mawe yakisemekana kwamba hilo ni eneo la Airport, hawa wakazi kwa kipindi cha miaka 24 wako tu wamekaa hawaelewi kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naiomba Serikali itoe tamko kama hawa wakatizi waendelee na shughuli zao katika hizo nyumba au katika hilo eneo, hiyo fidia haitalipwa ili wajue waendelee na mambo yao. Kwa sababu katika kipindi cha miaka 24, ukipita hilo eneo kwanza huduma za kijamii zenyewe, hazipo. Barabara ni mbovu, halafu wengine hawawezi kuziendeleza nyumba zao.

Mheshimiwa Spika, kama unavyojua, mtu akiwa na eneo lake; shamba lake au nyumba, kama hana pesa, anaweza akachukua leseni yake ya makazi au hati akaenda kukopa, lakini wale hawawezi. Wakienda benki yoyote wanaambiwa kwamba hilo eneo ni la Airport, lakini pia Serikali kwa muda wa kipindi cha miaka mitano ambayo mimi nimo humu Bungeni na kila mwaka nilikuwa nauliza maswali na katika kuchangia naulizia, hawajawahi kusema watawalipa au hawawalipi; watalichukua hilo eneo au hawalichukui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa naomba jibu la Serikali ili wajue kwamba wenyewe wapo pale au wanaondoka? Watalipwa au hawalipwi; ili masuala mengine yaendelee? Kwa sababu sisi Wabunge tunapokwenda huko, tunapata malalamiko mengi sana kutoka kwa hawa wananchi; na kweli kulalamika ni haki yao kwa sababu kama fidia ilifanyika 1997, mpaka leo ina maana hata hiyo kama watalipwa, watatumia sheria gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kuhusiana na mradi wa umeme ambao unapita Kinyerezi unakwenda Chalinze. Hawa watu wa Kata ya Kinyelezi Kifuru pia wamechukuliwa eneo lao sasa ni miaka minne, mpaka leo hawajalipwa. Siku zote wamekukwa wakija hapa kumwona Waziri, wamekuja kumwona Katibu, lakini pesa hazilipwi na mpaka sasa hivi tayari nimeona TANESCO wameshaanza kuweka nguzo zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iwalipe wananchi kwa sababu wanapotoa maeneo yao, nasi tunasema Serikali inawasaidia wananchi kiuchumi, maeneo yao hayo ndiyo yanawategemea. Kwa hiyo, Serikali iweze kuwalipa hao watu wa Kipunguni kama inawalipa. Kama haiwalipi, iseme. Serikali iwalipe watu wa Kinyerezi kwa sababu Kinyerezi nimeona tayari wameshaanza mradi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nililotaka kuongelea ni kuhusiana na issue nzima ya Mkoa wa Dar es Salaam kuhusiana na miundombinu. Sisi watu wa Dar es Salaam hatuwezi kusimama hapa tukaomba mbolea, sijui vitu gani; sisi hatulimi kitu chochote. Sisi uchumi wetu sana sana ni kuhusiana na miundombinu. Yaani wananchi wetu wakiweza kupita vizuri kwenye maeneo yao ili kwenda kwenye kazi zao na biashara zao, kwanza inawaongezea Serikali mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukubaliane, Dar es Salaam haiwezi ikalingana na mkoa wowote hata kama siyo Makao Makuu. Kwanza ndiyo inachangia pato kubwa katika nchi yet una ndiyo ina wakazi wengi. Kwa sasa hivi Dar es Salaam ina wakazi karibu milioni sita. Sasa tuna mradi unaitwa DMDP; huu mradi Hayati Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliahidi kwamba utaanza kutekelezwa mwezi wa Tatu, lakini mpaka sasa hivi hakuna chochote kinachoendelea, tunavyofuatilia, mradi wa DMDP II bado haujatekelezwa na wala hakuna matayarisho yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nilitaka niseme, sisi wakazi wa Dar es Salaam tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ametuwekea miradi mikubwa sana ya miundombinu, lakini bado kutokana na wingi wetu na kutokana na umuhimu wa Jiji la Dar es Salaam, bado tunahitaji huo mradi wa DMDP. Tunaiomba sana Serikali iweze kuamua, kama umekwama mahali iweze kuukwamua ili huu mradi uweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi Dar es Salaam mvua inanyesha. Kwa Wabunge wote wa Dar es Salaam; wa Majimbo pamoja na wa Viti Maalum hakuna mtu anaweza kurudi Dar es Salaam sasa hivi kutokana na mambo yanayoendelea. Barabara ni mbovu, zimejaa maji, mafuriko yanaendelea na wananchi wanadhani kwamba labda sisi tumekaa huku hatufuatilii kitu chochote wala hatusemei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba na kwa sababu tuliahidi, tuliahidi katika kampeni na lilikuwa ndiyo jambo kubwa, wananchi waliomba kwa kusema kwamba, sisi tunaomba miundombinu. Tukaahidi kwamba tutakapopata tu nafasi, miundombinu itaanza kutekelezwa; na tulikuwa na mradi wa DMDP ambao ulianza, lakini sasa hivi haupo tena.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, haya ambayo nimeyasema kuhusiana na fidia pamoja na mradi, naomba sana sana uweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)