Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi kuchangia hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nampa pongezi Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayoendelea kuifanya ya Chama chetu cha Mapinduzi akitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kuongea kuhusu afya. Nianze kwa kutoa pongezi kwa Serikali kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi hasa kwa kujenga vituo vingi vya afya kwenye Halmashauri zetu na kuboresha Zahanati zetu, Hospitali zetu zote za Rufaa. Ila natoa ushauri kwa sababu unakuta Vituo vya Afya vimejengwa lakini vingine havina watumishi wa afya.
Mheshimiwa Spika, mfano mmoja ni Kituo cha Afya Kisaki ambacho tulipewa hasa na Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli alipotembelea Bwawa la Nyerere; aliona kuwa kuna umuhimu wa pale Kisaki kuwa na Kituo cha Polisi na Kituo cha Afya. Kituo cha afya kimemalizika, lakini mpaka sasa hivi hakina watumishi. Kwa hiyo, kuna vituo vya namna hiyo. Naomba vituo vya afya vilivyokamilika ambavyo havina watumishi wa afya viweze kupewa watumishi hao.
Mheshimiwa Spika, napongeza sana kuona kuwa bajeti ya dawa imeongezeka. Ni kweli imeongezeka lakini bado wananchi hawajapata dawa. Bado kuna tatizo la dawa. Nilishaongea na Waziri wa Afya, Mheshimiwa Dorothy kuhusu dawa na nilifanya ziara kwenye Mkoa wangu wa Morogoro; na ikiwa ni mojawapo ya mikoa mingine kuwa bado tuna tatizo la madawa. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, ameongelea kuhusu mambo hayo, kwa hiyo, naomba waichukulie kwa undani tuweze kupata dawa, waweze kutibiwa watu ambao tunaumwa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni ushauri kuhusu Bima ya Afya. Viongozi wetu walishatuambia kuhusu Bima ya Afya kwa watu wote, naomba nalo walifanyie kazi kusudi liweze kutekelezwa. Jambo lingine ni watumishi wa afya kama nilivyosema.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba kuongelea ni dirisha la wazee. Ni kweli tulisema kuwe na dirisha la wazee, lakini inategemea na Halmashauri na Halmashauri. Wazee wengine wanatibiwa vizuri, wengine bado wanahangaika, wanaambiwa mkanunue dawa na unakuta wazee wengine hawana uwezo. Kwa hiyo, nashauri kuwa nalo liweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nashauri ni kuwa na maboma hasa kwenye Zahanati. Kwa ile miradi ambayo haijakamilika hasa maboma ya Zahanati naomba yaweze kukamilika na Vituo vya Afya kusudi tuweze kuendelea na miradi mpya kwa kukamilisha miradi ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nimekumbana nalo ni chanjo ya watoto wachanga. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Afya aifanyie kazi. Bado kuna matatizo; akina mama wengine wanalalamika kuwa watoto wao hawapati chanjo kadiri inavyostahili ambalo ni tatizo kubwa sana. Kama mtoto hajapata chanjo kadiri inavyostahili, anaweza baadaye akapata ugonjwa ambao ungetibiwa kutokana na chanjo. Hilo ni jambo ambalo nimekutana huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, magonjwa yasiyoambukizwa nayo sasa hivi imekuwa ni tatizo. Naomba ifanyiwe utafiti na jinsi ya kuyatibu tuweze kuepukana na magonjwa haya ikiwepo kisukari, kansa, magonjwa ya ini pamoja na magonjwa ya moyo. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri kuwa elimu iweze kutolewa kwa wananchi pamoja na kuona jinsi ya kuepukana na hili, lakini na utafiti uweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Spika, nikiwa bado kwenye mambo ya afya; tumeingia kwenye Covid tumesahau kuwa bado UKIMWI upo. Naomba suala la UKIMWI, ingawa tuna Kamati ya UKIMWI, ifanyiwe kazi, elimu izidi kutolewa kwa sababu sasa tumekwenda na Covid, tumesahau UKIMWI bado upo. Kwa hiyo, naomba iangaliwe sana kuwa UKIMWI bado upo. Ndiyo sababu uliunda Kamati ya UKIMWI ukijua kuwa UKIMWI bado upo.
Mheshimiwa Spika, wananiambia ni Kamati ya Mambo ya UKIMWI, siyo Kamati ya UKIMWI. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nilindie muda wangu, huyu Shangazi ananisumbua. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, elimu; naishukuru Serikali kuwa kwa kweli imefanya vizuri katika mambo ya elimu.
SPIKA: Mheshimiwa Shangazi usimsumbue Mheshimiwa Ishengoma. (Kicheko)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya vizuri kwenye mambo ya elimu, elimu bila malipo hasa kwa upande wa ada, lakini tatizo bado lipo kwenye chakula hasa kwa shule za msingi na sekondari zile za kutwa ambapo hawapati chakula cha mchana. Naomba hilo lisisitizwe kwa sababu bila ya kupata chakula huwezi kuwa na lishe bora na huwezi kufikiria na huwezi kufanya vizuri darasani, kwa hiyo naomba hilo nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Spika, tumetembea kwenye shule za pembezoni bado kuna tatizo la Walimu, kwa hiyo naomba nalo liangaliwe ingawaje wataajiriwa wengine, lakini awatoshi bado kuna Walimu ambao wapo tu lakini hawajaajiriwa. Kwa hiyo tunaomba utumishi watoe vibali kusudi Walimu waweze kuajiriwa ambao bado hawajaajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, miundombinu bado mingine ni mizuri lakini mingine bado matatizo. Kwa mfano, madawati nashukuru Mheshimiwa Ummy alisema kuwa atanunua madawati, lakini naomba waliangalie watoto wasikao chini waendelee kukaa kwenye madawati. Pia madarasa na nyumba za walimu bado ni matatizo.
Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi kwa ukarabati wa Shule Kongwe kweli shule kongwe zimekarabatiwa hasa za shule za sekondari, lakini nikija kwenye madarasa ya shule za msingi, bado ni matatizo. Kwa hiyo shule za msingi naomba na zenyewe ziangaliwe katika kufanyiwa ukarabati.
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; nashukuru na natoa pongezi ndio, mikopo imeongezeka, lakini bado ni tatizo. Kuna wanafunzi ambao wamefaulu na unakuta wengine ni wasichana ambao hawajapa mikopo, wako vijijini, juzi juzi nimekutana na msichana mmoja analia kabisa, wako wengi vijijini, wako wengi mitaani, wamefaulu lakini wamekosa mikopo. Kwa hiyo, naomba vigezo vya mikopo ya elimu ya juu viangaliwe, hata watoto wa maskini ambao ni hitaji waweze kupata mikopo kwa sababu kweli wengine hawajapata mikopo hiyo. (Makofi)
Mheshimwa Spika, sekta ya utafiti hasa Vyuo Vikuu; naomba uangaliwe, uweze kutengewa fedha za kutosha na hiyo asilimia moja inayotengewa iweze kutolewa kwa wakati. Mafao ya Walimu wakiwemo Wahadhiri naomba yaangaliwe na hapa naongea kwa pia kwa ajili ya wafanyakazi wote. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake amesema pension inatolewa, nashukuru sana, lakini kuna wengine ambao wanasota hawapati pension kwa muda mrefu, naomba waangaliwe, waweze kupata pension zao. Wengine wanatuambia tuwaombee na ndiyo hivyo hapa nawaombea kuwa waweze kupewa pensions zao kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, siwezi kumaliza bila kuongelea miradi ya kimkakati. Namshukuru sana Hayati Dkt. Magufuli, Rais wetu mpendwa, alale mahali pema peponi. Mheshimiwa mama Samia ambaye ni Rais wetu waliungana kwa pamoja na Serikali yetu wakaona miradi ya kimkakati ambayo ilikuwa imekaa kwa muda kabla ya kufanya kazi, sasa imefufuliwa, reli ya mwendokasi ambayo ni SGR, inaendelea kujengwa vizuri. Mpaka sasa hivi tumeambiwa ni asilimia 90.3 Dar es Salaam mpaka Morogoro.
Mheshimiwa Spika, sasa nauliza ni lini itaanza kazi hasa hiki kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro au tutasubiri reli nzima imalizike? Wananchi wa Morogoro wanaisubiri kwa hamu. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aniambie kwa sababu inaenda vizuri na nashukuru sana kwa sababu hiyo reli ya mwendokasi ikiisha ambayo ni mradi mkubwa, ambaye haoni aje angalie pale inavyopendeza. Watanzania tunajivunia hii reli ambavyo itapunguza mizigo ambayo inaharibu barabara zetu, pamoja na wasafiri na utalii itakuwa ni kivutio kikubwa na itaongeza ajira kwa vijana wetu na wajasiriamali wote pamoja na kipato kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile naomba kuongelea kuhusu bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, bwawa hili ni kubwa kama tulivyoambiwa ambalo litaweza kutoa umeme wa kutosha ambao…
SPIKA: Ahsante
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tunawashukuru, waendelee iweze kukamilika ili tufaidikea kwa hilo. Nashukuru kwa kunipa nafasi.