Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo ipo mbele yetu.
Kwanza, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutujalia uzima na kuweza kuwepo hapa leo asubuhi kwa ajili ya kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa letu. Pili, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuanza vizuri na kutoa mwelekeo wa Taifa letu ambalo, hivi karibuni tumeondokewa na Rais wetu mpendwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, mwanamapinduzi wa kweli, mzalendo na anayeipenda nchi yake. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.
WABUNGE FULANI: Amina.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa wasilisho lake aliotoa jana, lakini nimpongeze yeye pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuratibu shughuli za Serikali. Kama ambavyo tunajua wao ndio waratibu wa shughuli za Serikali, kwa ujumla wake Wizara zote wanazisimamia wao. Nimpongeze sana mama yangu Jenista Mhagama pamoja na Manaibu Waziri ambao wako katika ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo nichukue nafasi hii kupongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kipindi kilichopita. Taarifa tuliyosomewa hapa na Mheshimiwa Waziri Mkuu inaonyesha wazi kwamba Serikali ina dhamira ya dhati katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. Tumeona huduma za kijamii ambazo zimetajwa hapa zimefanyika katika kipindi kilichopita. Tumeona pia barabara kwa maana ya miundombinu lakini pia tumeona katika maeneo ya elimu, umeme, pamoja na usafirishaji ikiwemo na utalii kazi imefanyika kubwa katika kuhakikisha kwamba Tanzania inasonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya ni pamoja na miradi ya kielelezo, miradi mikubwa ambayo imeanzishwa katika kipindi kilichopita ikiwemo SGR, ununuzi wa ndege, uboreshaji wa shirika letu pamoja na umeme wa Mto Rufiji. Kwa hakika hii ni misingi mikubwa ya kuleta maendeleo katika nchi yetu. Uchumi wetu lazima uimarishwe kupitia mambo kama hayo makubwa.
Kwa hiyo, leo hii ukisikia mtu anabeza juhudi zilizofanya na Serikali katika muda huu, mtu huyo hajui maana ya maendeleo. Watu hao sometimes utakuta wanalalamika kwamba Serikali haijaweka mipango mizuri, tukija kutekeleza wao wanarudi wanageuka kuanza kuilaumu Serikali. Naomba nimwombe Waziri Mkuu tusonge mbele na kama alivyotuambia jana miradi yote itekelezwe iliyoanzishwa na Serikali ambayo inaweza kuleta matumaini makubwa katika maendeleo ya nchi yetu, tusirudi nyumba kwa sababu tumejipanga vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunajivunia tumefikia uchumi wa kati au kufika uchumi wa kati bila kuweka mipango kama hii. Leo hii tunapunguza gharama za usafirishaji kwa kujenga barabara nzuri. Leo tunahakikisha tuna shirika letu wenyewe la ndege, tunaambiwa sasa zitafika kumi na mbili ni shirika au nchi itakuwa na uwezo wa kuwa na usafirishaji na kuvutia watalii katika nchi yetu, mwisho wa siku tutaweza kuongeza fedha za kigeni na kuweza kuongeza uwezo wa Serikali kuhudumia wananchi wake. Kwenye hili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na naomba niseme sisi Wabunge tuunge mkono Serikali yetu katika kazi nzuri inayofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikieleza hivi hayo ni maono ya viongozi wetu, lakini maoni ya viongozi wetu pia yanasimamiwa na Ilani bora kabisa ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imepanga mipango na imetafsiriwa vizuri sana katika Dira ya Maendeleo pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Kwa hiyo, niseme tu kwamba maendeleo haya yanayofanyika yanaenda kulenga kumkomboa Mtanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maendeleo haya yaliyofanyika huwezi kuondoa viongozi walioshiriki kwa muda wao katika kuhakikisha kwamba wanaisaidia nchi hii. Legacy ambayo imewekwa katika nchi hii, Mwenyezi Mungu amemtanguliza mbele ya haki Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, hatutamsahau kwa kazi kubwa aliyofanya katika nchi yetu. Ndio maana kama Bunge tuliazimia kwa pamoja kumpongeza na kutambua juhudi zake. Kutambua juhudi za Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ni kuwafanya akina Dkt. John Pombe Maguguli wengine waendelee kufanya kazi kama aliyofanya yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tuwe na wivu wa kuona mtu aliyefanya kazi vizuri; mapungufu madogo madogo kila mmoja hapa ana yake, inawezekana, lakini kwa yale mengi aliyofanya mazuri lazima tumuenzi na kumpongeza sana na kumuunga mkono katika mambo haya. Mfano mdogo, alikuwa ni jasiri katika kupambana na vita ya majangili wa tembo, wote tuajua, miaka ya nyuma tulikuwa na tatizo kubwa la majangili wa tembo. Tulifikia tulikuwa na tembo karibu 100,009 miaka ya nyuma ya 2014, lakini leo tembo walipungua mpaka kufika 43,000, lakini leo kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa na wenzetu wa maliasili, tunafikisha tembo 60,000 katika nchi yetu. Maana yake nini? Maana yake ni kwamba tumeweza kusimamia vizuri kazi ambayo tumeachiwa rasilimali au maliasili tuliyoachiwa katika nchi yetu. Kwa hiyo, niwaombe sana twende kifua mbele, kazi inayofanyika ni nzuri, tusibabaishwe na kelele za pembeni, sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha Tanzania inakwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili la utalii mafanikio yake yameonekana, leo hii tunavyoongea hapa tumeongeza kuvutia watalii. Mwaka 2015 watalii 1,137,000 mpaka kufikia 2019 tumeongeza watalii, wamefika 1,527,000; maana yake ni kwamba kupitia hivi vituo vyetu tumeongeza watalii kiasi hicho, kuja katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo tumeongeza fedha kama ambavyo ametuambia Mheshimiwa Waziri Mkuu, kufikia mwaka 2015 tuliongeza fedha dola bilioni 1.9 ziliongezwa katika utalii, lakini kufikia mwaka 2019 tuliongeza fedha za kigeni bilioni 2.6 ambazo zinakwenda kuongeza uwezo wa Serikali wa kutoa huduma za kijamii katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii ni kubwa ni nzuri, niwaombe sana wenzetu wa maliasili, Tanzania lazima tuongeze nguvu katika maliasili kwa sababu ndipo tunapopata fedha nyingi za kigeni. Leo hii Simba wamesema visit Tanzania, naomba niongeze tena, niseme visit Tanzania, the land of Kilimanjaro, Serengeti and Zanzibar ili iweze kuvutia zaidi tunapokwenda kwenye ile robo fainali ili dunia nzima ione kwamba tuna vivutio vikubwa vya Serengeti na Zanzibar ni sehemu nzuri ya kupumzika pamoja na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kupongeza kazi nzuri iliyofanyika, lakini naomba nikuhakikishie kwamba Watanzania wanajua kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya CCM pamoja na viongozi wake. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)