Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuweze kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya yote nipende kuwatakia Watanzania wote heri na baraka ya Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani ambao tumeuanza leo, Mwenyezi Mungu atujalie tuifunge kwa heri na tumalize kwa heri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru wenzetu ambao si Waislamu lakini wameonesha kutuunga mkono kwa njia zote. Nikiangalia leo Bunge lako hijabu zimeongezeka, si kwa Waislamu peke yake, na mavazi ya staha yameongezeka sana. Na hii ni kutuunga mkono na kutusaidia kutupunguzia majaribu; ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia hotuba hii kwa kusema yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, sisi wote ni Watanzania na tunajenga Tanzania moja. Tuna wajibu wa kuyaenzi yale mema yote ambayo… katika nchi yetu. Binafsi toka imeanza hotuba ya mpango na mpaka tunakwenda hotuba ya bajeti, nimesikiliza sana, nimekaa kimya sana kuyazingatia sana yanayosemwa na naomba niseme tu, hoja hujibiwa kwa hoja, hoja haipigwi rungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotoa hoja ikaonekana hoja zetu wakati mwingine zinakinzana na yale mawazo waliyonayo wenzetu, wajaribu kutujibu kwa hoja zile zile ili mwisho wa siku tufikie mwafaka katika kujenga Taifa letu hili moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitamke bayana, sioni aibu, hata kama ni mpinzani, kusifia lolote jema linalofanywa na Serikali hii. Lakini hali kadhalika, msione soo! Pale tunapolisema lolote baya linalofanywa na Serikali hii kwasababu lengo linarudi palepale, kwamba lengo letu ni kujenga nchi moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia kuhusu miradi ambayo ilianza katika utawala wa Awamu ya Tano. Niseme wazi, wako wasomi, wachumi, walioongelea sana kuhusu miradi lakini nitamke bayana, miradi ambayo imetumia fedha nyingi za Watanzania kwa malengo ya kuliletea tija Taifa hili, hata kama kuna kasoro zinazoonekana katika utekelezaji wa miradi ile, hatuwezi kui-dump miradi ile kwasababu ya kasoro hizo. Na kufikiria kui-dump miradi hii na kuitelekeza kwasababu ya kasoro zilizopo ni kosa moja ambalo kizazi kijacho kitatuhukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia baadhi wakisema kwamba mradi wa bwawa la umeme hauna tija na utupiliwe mbali, nimesikitika sana. Mama mwerevu anapopika chumvi ikazidi kwenye nyungu, watoto wanasubiri chakula, haendi kulitupa lile sufuria watoto wakafa njaa, ataongeza maji ukali wa chumvi upungue na watoto waweze kula; huyo ndio mama mwerevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Watanzania, Wabunge sisi, tuna wajibu wa kuyaona makosa yaliyomo kwenye miradi ile, tusiwe wanafiki wa kusifia kila kitu wakati tunajua yako mapungufu ambayo yanatakiwa kurekebishwa ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono mradi wa bwawa uendelee (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika, naomba kasoro zilizopo katika Mradi wa Bandari ya Bagamoyo tuangalie tena upya, mahitaji ya Bandari mpya ya Bagamoyo bado ni muhimu kwa uchumi wa Taifa letu, ni muhimu kwa ustawi wa viwanda vilivyotarajiwa kujengwa maeneo ya Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wasafiri wa kwenda Zanzibar tunapopanda boti mara kwa mara, hakuna siku utakuta hapana meli chini ya 50 ambazo zinasubiri kufunga geti katika Bandari ya Dar es Salaam, hakuna. Inaaishiria bado kuna mapungufu katika Bandari ya Dar es Salaam. Kupata Bandari ya Bagamoyo ni ukombozi wa eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipofikiria kujenga Bandari ya Bagamoyo wenzetu wa Kenya hawakuwa hata na wazo la kujenga Bandari ya Lamu, walipotusikia tu wao walianza, na tayari Bandari ya Lamu imekamilika. Sisi bado tunakaa tunabishana tukidhani kwamba kuna kasoro; kasoro zirekebishwe na kazi iendelee, hayo ndiyo mawazo yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika hili, kipekee sana nampongeza kiongozi wangu wa chama, Mheshimiwa Zitto Kabwe. Katika maoni yake yote ameonesha kukubaliana na mapungufu lakini akitaka kazi nzuri iliyoanza tufikirie namna ya kuifanya, kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie katika ukurasa wa 22 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameongelea suala la uendeshaji mashtaka na utoaji wa haki. Nipende kusema kwamba huu ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhani; tarehe 03 Novemba, 2014, nilisimama hapa kuongelea ucheleweshwaji wa kesi na niligusia sana kuhusu kesi ya Mashekhe wa Uamsho kutoka Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema – wakati huo kesi ile nadhani ikiwa kama na miaka minne – leo tena ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, nasimama hapa kusema, tayari umefika mwaka wa nane, tunakwenda mwaka wa tisa. Kesi ile imechelewa sana na wanasiasa wanapenda kusema justice delayed, justice denied, lakini wanazungumza mdomoni, hawaitafsiri kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mshtakiwa anapokwenda mahakamani anachokisubiri ni hukumu ya makosa yake. Haki ya mtuhumiwa ni kuhukumiwa, siyo kukaa gerezani katika kipindi kirefu. Kunyongwa ni hukumu, kufungwa maisha ni hukumu, kufungwa miaka kadhaa ni hukumu; ni haki ya mshtakiwa kulingana na makosa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapomnyima hizo hukumu wakati ilikuwa ni haki yake tayari unamyima haki yake ya msingi. Matokeo yake ni nini; kwa mujibu wa sheria zetu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri anayo mamlaka ya kumsamehe mfungwa yeyote aliyeko gerezani. Lakini Mheshimiwa Rais hana mamlaka ya kumsamehe mtuhumiwa aliye na makosa. Kuchelewesha kumpa hukumu mtuhumiwa aliyeko gerezani ni kumnyima Rais wa Jamhuri haki yake ya kuwahurumia baadhi ya wafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano tulionao leo, akina Babu Seya leo wasingekuwa huru kama wasingekuwa wamehukumiwa. Kama wangekuwa wanaendelea kushutumiwa na kukaa pale mahabusu, bado wangekuwa wako mahabusu. Lakini kwasababu walihukumiwa, Mheshimiwa Rais alitumia nafasi yake ya kikatiba kuwasamehe watuhumiwa wale, na leo wako huru na familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda mwaka wa tisa, sheria zetu Waheshimiwa Wabunge, tuna dhima kwa Mwenyezi Mungu tunapopitisha sheria ya kwamba anayehukumiwa kwa kosa la ugaidi, utakatishaji fedha, uhujumu uchumi, akishtakiwa kwa makosa hayo hapewi dhamana. Tuangalie upya namna gani ambavyo tunakiuka haki za msingi za binadamu. Kwasababu laiti ingekuwa anayeshtakiwa kwa makosa haya ana hukumu ya kukaa katika hali ya kuwa mahabusu, ingekuwa bado tumetenda haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwendesha mashataka anapoamua tu kwamba shtaka hili linaangukia katika maeneo haya matatu basi huyo haki yake ni kukaa rumande katika muda usiojulikana. Waheshimiwa Wabunge, kama tunalamikia kupanda kwa bei za bundles na tukapiga makelele ikasimama, kikokotoo kikasimama; kwa nini tusilalamikie haki za wananchi wetu ambao wakishtakiwa kwa makosa hayo wanasota magerezani kwa muda wa miaka kadhaa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Walahi juzi kuna mama mmoja alikwenda kumuangalia mtoto wake katika washtakiwa wale wa uamsho, alipotoka mahakamani tu umauti ukamchukua. Alipotoka Segerea hajarudi kwao Zanzibar, umauti ukamchukua kwa uchungu aliopata kwa watoto wake kukaa gerezani muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaapa kwa Mungu kila siku atuongoze kufanya mema na tumshauri Rais katika mambo ili nchi hii ipate tija kwa Mwenyezi Mungu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)