Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipatia hii nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu. Jambo la kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo ameitoa. Hotuba ambayo imekuwa ni pana, imekwenda kwa mapana na uwanda mpana sana. Karibu kila kitu amekizungumza vizuri sana. Kwa kweli tunampa hongera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nchi yoyote, kiongozi yoyote anayekuwepo katika taasisi au kwenye nchi lazima awe na maono. Kuwa na maono maana yake ni kuwa na dira na dira hiyo ukiwa nayo lazima uwe na uwezo wa ku- share na wengine wote na wenzako waweze kuiimba hiyo dira na hao waliofanya hivyo ndiyo walioweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baba yetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wetu alikuwa na maono makubwa, alikuwa na mtazamo na dira kubwa. Ile dira aliweza ku-share na wenzake na ndiyo maana nataka niseme Magufuli alikuwa akisema, wa pili mama yetu Samia Suluhu Hassan, yeye alikuwa anaenda kutekeleza na kufuatilia utekelezaji. Msimamizi wa Serikali, Kassim Majaliwa Majaliwa yeye ana wahi site, ikishasemwa tu anawahi kwenye utekelezaji na ninayo mifano michache ninayoweza kusema. Nakumbuka wakati ule hayati Dkt. Magufuli aliposema atahakikisha Serikali yake inahamia Dodoma, alipotamka tu lile neno niliona wale viongozi walivyotekeleza yale maono. Wa kwanza alikuwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu, akasema ndani ya miezi mitatu nahamia Dodoma na kweli akafanya hivyo. Makamu wa Rais kahamia Dodoma maana yake ile dira ilikuwa shared. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alipotamka kwamba tunatakiwa tujenge bwawa kubwa la kuzalisha umeme, walichokifanya nilimwona Waziri Mkuu ameenda site kwenda kuangalia mahali ambapo daraja litajengwa. Ukiangalia Makamu wa Rais ameenda huko, kwa hiyo mambo yote walikuwa wana-share na ndiyo maana hatuna wasiwasi na miradi yote ambayo imeanzishwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano kwamba yote itatekelezwa vizuri kwa sababu viongozi waliokuwa wanayaimba hayo ndiyo hao ambao bado wako madarakani. Kwa hiyo hatuna wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza. Kuna watu wana wasiwasi kwamba mradi wa SGR, eti hautakamilika, nani anasema? Ule mradi ni wa muhimu, reli ya Standard Gauge aliianzisha Dkt. Magufuli, viongozi wetu wakatufundisha, Bunge likapitisha fedha, leo hii usikamilike, tutakuwa kwa kweli hatujaitendea haki nchi hii. Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere, walipolisema tulipitisha hapa Bungeni, lile bwawa lazima likamilike na litaleta maendeleo makubwa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hiyo tu, barabara nyingi zimejengwa za juu, za chini; madaraja tumeona, viwanja vya ndege vimejengwa, ndege zimenunuliwa, nani leo hii anaweza akaiambia hii nchi kama wewe hujaweza kupanda hata hiyo ndege una tatizo lako binafsi, lakini ndege zipo. Hizi zote ndiyo zimebeba uchumi wa nchi yetu. Hawakuishia hapo, wameenda kwenye afya, elimu, maji na kadhalika. Tumeenda mpaka kwenye kujitosheleza kwa chakula. Nchi hii tulikuwa hatujitoshelezi kwa chakula, alipoingia Hayati Dkt. Magufuli akasema kokote kutakakokuwa na njaa, huyo Mkuu wa Mkoa na Wilaya watanikoma na kweli hatujawahi kupata njaa mpaka sasa hivi na ndiyo maana uzalishaji uko wa kutosha. Wananchi sasa hivi wanacholalamikia ni soko, wapi wauze mazao yao. Hilo ndiyo limekuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachotaka kusema walifanya kazi kubwa, alifanya kazi nzuri na mimi nasema tutaendelea. Miradi ya maji pale Vwawa alitoa fedha mradi wa maji, maji pale bado pana tatizo. Fedha zimekwenda, mradi umetekelezwa lakini maji bado hayatoki. Tuliahidi kwamba hospitali ya rufaa itajengwa pale Vwawa, Ilembo, imeletwa fedha imejengwa ilitakiwa ianze mwezi Novemba mpaka sasa hivi haijaanza. Naomba watendaji waende wakashughulikie hayo kwa sababu ni ahadi zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Sasanda kulikuwa na kambi ya kuendeleza vijana. Kambi ile ni muhimu ikaendelezwa ili vijana wa nchi hii waende sasa wakajifunze maarifa, uzalendo na miradi mbalimbali ili waweze kuchangia katika maendeleo ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo soko la mazao. Mheshimiwa Rais aliyeondoka alituahidi, yote hayo lazima tuyakamilishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nilichangie ni upande wa watumishi. Mahali popote ili uweze kukamilisha kitu cha kwanza ni watumishi na zamani tulikuwa tunasema mteja ni mfalme, siku hizi mteja ni namna mbili, wa kwanza ni mtumishi. Mtumishi yule ukim-treat vizuri ndiyo atakayefanya hata wateja waongezeke na wapatikane na waende vizuri. Kwa hiyo basi, kwa kuwa tumetekeleza miradi mikubwa na tunaendelea kuitekeleza na ahadi na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ilikuwa ni kwamba sasa tunaingia kwenda kuhakikisha watumishi wetu wanapata maslahi mazuri ili wale ambao madaraja yalikuwa hayajapandishwa, zile promotion ambazo zilikuwa hazijafanyika, mishahara ambayo ilikuwa haijaongezeka, basi sasa ni kipindi naiomba Serikali yetu sasa iwatazame hawa watumishi wa Serikali waweze kuongezewa ili waishi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hao tu, watumishi wa Sekta Binafsi. Serikali ilipanga vima vya chini vya mishahara ya Sekta Binafsi zote, vima vya chini vile waajiri wengi hawajavizingatia. Ningeomba ili Watanzania wawe na maisha mazuri ili wananchi wawe na maisha mazuri waweze kuchangia basi naomba Serikali ikaangalie maeneo hayo. Ninachotaka kusema, miradi mikubwa hii ya vielelezo, ndiyo imebeba uchumi. Uchumi wa nchi yetu umefika kuwa ya kipato cha kati kwa sababu ya hii miradi ya vielelezo na miradi hii tusimame pamoja isitokee hata mmoja wetu mara anaanza kubeza, mara mwingine anaanza kusema huu mradi tuuache tutakuwa kwa kweli hatujaitendea haki nchi hii. Miradi ya umeme, umeme kule wanahitaji, una shida sana kwenye Mkoa wa Songwe. Kule vijiji vyote ambavyo havijapata vinahitaji umeme, lakini hata mahali ambapo uko bado kuna changamoto unakatikakatika. Tunaiomba Serikali ikasimamie, ikatekeleze ahadi zake ili umeme ule upatikane. Zile barabara ambazo ziliahidiwa tulifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ninalotaka kusema ni kuhusu Mradi wa Chuma wa Liganga, huu lazima tuutekeleze. Ni mradi mpya lazima tuutekeleze, tutenge fedha, tukautekeleze huo, tukipata chuma chetu tutaweza kujenga viwanda imara, tutaweza kupata malighafi hapa hapa nchini na tukiwa na umeme wetu ndiyo maendeleo makubwa yataweza kuwepo. Bila kufanya hivyo, tutashindwa kwa kweli kuweza kufanikiwa kama nchi na kufikia yale malengo tuliyojipangia kwamba ifikapo mwaka 2020 tutafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naamini kwa jinsi tulivyojipanga na kwa jinsi Bunge hili linavyofanya kazi nzuri na kwa Watanzania ambavyo sasa tunataka kuona nchi yetu inaendelea, naamini tutaweza kufika kuwa nchi ya kipato cha kati cha uwanda wa juu na hayo yanawezekana kwa kufanya kazi kama timu, kwa kushirikiana, tuondoe ubaguzi, tuondoe utengano, tuwe kitu kimoja. Mungu awabariki. Ahsante sana. (Makofi)