Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi kwanza nitoe pole kwa Mheshimiwa Rais mama Samia, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika na wewe Naibu Spika kwa kuondokewa na kipenzi chetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Watanzania kwa ujumla tunajipa pole sana kwa msiba huu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana, kuna baadhi ya watu muda si mrefu, hayati Dkt. Magufuli tangu tumemzika wameanza kuzungumza mambo ya ajabu, nashangaa! Msiba huu uliotukuta mama Samia, Waziri Mkuu wamezunguka nchi hii kututafutia kura sisi, kila mahali Waziri Mkuu amekwenda huku, Makamu wa Rais na ndio ambaye ni Rais amekwenda huko na ndiyo tumerudi hapa Waheshimiwa Wabunge. Leo mtu anasimama na watu wengine kwenye mitandao ya kijamii kumtukana na wengine ni kwa sababu wamekosa vyeo na kadhalika na ndiyo wanaosema maneno ambayo hayaeleweki, vyeo atatoa kwa watu wangapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wamelia, Naibu Spika umelia machozi, Spika wetu amelia machozi, mama Samia mliona analia machozi, Marais wastaafu amelia machozi, Mwinyi amelia machozi, walikuwa wanalilia nini? Wanalia kwa huzuni kwa sababu tumeondokewa na kipenzi cha Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo mtu mwingine anasema nilipougua nimepigwa risasi kule Nairobi hakuja kunitazama, alikuja mama Samia. jamani Wabunge tuwe wakweli, hivi ndani ya familia ukimtuma ndugu yako baba au mama si ndio wewe umekwenda kumtazama, sasa alitaka afanyiwe nini, amekwenda Makamu wa Rais ambaye sasa ni Rais kwa kutumwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa hiyo, lazima tushukuru kwa kila jambo ndugu zangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Wanamakambako au wananchi wa Jimbo la Makambako wamenituma, wanahuzunika sana na wanamtakia kila la kheri mama Samia, pamoja na Waziri Mkuu watekeleze wajibu wa Watanzania.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Deo Sanga kuna taarifa Mheshimiwa Msukuma.
T A A R I F A
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji kuhusiana na machungu yaliyopo kwa Watanzania kwamba, ndiyo maana kuna mzungumzaji amezungumza mchana humu anasema kwamba, baadhi ya Wabunge wakikosoa isionekane nongwa. Sisi tunaona nongwa kwa sababu wakosoaji wote waliokosoa ni watu waliokula viapo, sasa viapo huwa vinaendelea hata kama umetolewa kwenye madaraka. Tutaendelea kuwapiga mpaka watambue umuhimu wa kiapo walichokiapa. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Deo Sanga, malizia mchango wako.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika bajeti hii ndio Mtendaji Mkuu wa Serikali, sasa naomba nizungumzie changamoto, kazi kubwa zimefanyika katika Jimbo la Makambako na Tanzania kwa ujumla, lakini kwa leo naomba nichangie changamoto. Changamoto ya kwanza, tuna tatizo la fidia katika Mji wa Makambako, kuna wananchi wanaokaa katika eneo lile la Polisi, wananchi hawa wameanza kuishi pale kabla ya Polisi kupewa eneo lile mpaka sasa wanaishi maisha magumu, hawawezi kuendeleza kufanya kitu chochote.
Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake, Mheshimiwa Jenista dada yangu wahakikishe tunalipa fidia kwa wananchi hawa na IGP Sirro namwamini sana, anafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili, katika fidia pale Idofi, Idofi inajengwa one stop center, Serikali imepeleka fedha zaidi ya milioni 800 na kitu, zilizobaki tunaomba zimaliziwe ili wananchi wale waishi kwa amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya tatu katika fidia, kuna soko la kimataifa, walilipwa watu zaidi ya bilioni tatu, milioni mia moja na kitu, wamebaki watu kumi na nane, wanapata tabu, tunaomba Serikali imalizie katika kulipa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya nne katika fidia, kuna umeme wa upepo Mheshimiwa Dkt. Kalemani nimekwenda kwake zaidi ya mara mbili. Naomba wakae walitatue tatizo hili la kuwalipa wale wananchi fidia kwa ajili ya umeme wa upepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa afya, tumepewa zahanati nyingi, tumejenga katika Mji wa Makambako, wananchi wamefanya kazi hiyo pamoja na Madiwani, pamoja na mimi Mbunge. Tuna hospitali, tuna kituo cha afya, tunaomba vifaa tiba ili zahanati hizi pamoja na kituo cha afya kipo Lyamkena pale, kiweze kuanza. Tuna hospitali ya Halmashauri na kadhalika, tuna kituo cha afya ambacho kimeanza kujengwa kule Kitandililo ambacho Mheshimiwa Diwani na wananchi wake na mimi Mbunge wao tumeanza kukijenga, tunaiomba Serikali iunge mkono jitihada za wananchi ambazo zimeanzwa kule Kitandililo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho si kwa umuhimu, kwenye Halmashauri yangu ya Makambako, Madiwani posho wanayoipata kwenye kikao ni tofauti na halmashauri nyingine. Naomba Waziri Mheshimiwa Ummy yuko hapa, tafadhali niombe sana kupitia Waziri Mkuu, Madiwani hawa wapewe posho sawa na halmashauri zingine, kwa sababu nikiwatajia hapa wanapata kiduchu na ninajua tatizo lililopo Makambako lipo katika halmashauri nyingi. Niwaombe sana safari hii Madiwani hawa wapewe posho kama wanavyopewa wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)