Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema ambapo nimeweza kusimama ndani ya Bunge hili na pia niwatakie Waislam wote Ramadhan Kareem. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha vizuri bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka wa 2021/2022. Nikimpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba ninukuu sehemu ya kipande cha Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan wakati wa shughuli ya kumuaga Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano kama ifuatavyo; “Tunapokwenda kumpumzisha Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tunaweza kusema bila kigugumizi kuwa tuko tayari kuiendeleza kazi yake nzuri kwa nguvu kasi na ari ile ile.”
Mheshimiwa Naibu Spika, nimenukuu maneno haya ya Mheshimiwa Rais Mama Samia na nampongeza sana, baada ya kuona ahadi aliyoiahidi na uwasilishaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaenda sambamba. Nasema hivyo kwa sababu nikiangalia majumuisho yake ya mambo ambayo Serikali itajielekeza nayo, akifanya summary ya bajeti yake nzima, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati iliyoanzishwa na Hayati Rais Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mradi huo ni ununuzi wa ndege na Serikali imesema hapa imeshalipia ndege tatu, majadilliano mbalimbali yamefanyika ndani ya Bunge, nayaunga mkono, lakini nataka kusema moja tu, wengi wamekuwa wakinukuu taarifa ya CAG, hata watumiaji wengine wa taarifa hii baada ya kuwasilishwa Bungeni, lakini nataka niseme, tusimuwekee maneno zaidi CAG, kwa sababu kwenye ukurasa wake wa 16 na 17 pamoja na hasara ya Shirika la Ndege hii, CAG hajasema kama uwekezaji huu ni hasara, badala yake ameshauri kudhibiti gharama za uendeshaji pamoja na za kibiashara ili kampuni hii isiendelee kupata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania tupate tafakuri mpya, kama TANROAD tunaiwekea zaidi ya trilioni tatu kwa ujenzi wa barabara na haiandai taarifa ya kuonyesha kwamba tunahitaji kuona faida na hasara, ni huduma tu kwa sababu barabara zinasaidia sekta nyingine, ufike wakati tuliamini shirika la ndege linatoa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mradi mwingine wa kimkakati ambapo Waziri Mkuu kupitia hotuba yake amesema atauendeleza ni ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na mradi huu CAG amekagua na nataka niseme ni mradi pekee ambao ameukagua wenye kurasa nyingi kama
32. Watumiaji wengi wa ripoti yake wamejielekeza kwenye kipengele kimoja cha kutokuwepo kwa upembuzi wa kina, ningeomba niwashauri waisome vizuri…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Subira Mgalu, subiri kidogo, Mheshimiwa Halima naona umesimama.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, yes. Mheshimiwa Subira ni Mjumbe mwenzangu wa Kamati ya Bajeti…
NAIBU SPIKA: Ngoja nijue ni kuhusu utaratibu, taarifa au kitu gani?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa.
NAIBU SPIKA: Sawa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa kutokana na alichokisema, nasema hivi Mheshimiwa Subira anafahamu chini ya taarifa ya Msajili wa Hazina ya Mashirika ya Umma ya Serikali, kuna mashirika ambayo yanatoa huduma na kuna mashirika ya kibiashara. ATCL ni shirika la kibiashara, kwa hiyo ni muhimu wakati tunachangia haya mambo, tujue linatoa huduma lakini ni la kibiashara, halijawekwa pale kutoa huduma per se, linafanya huduma then we expect to make profit. Kwa mazungumzo anayozungumza asi-mislead juu ya jukumu la shirika letu la ndege. Ni hayo tu. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Subira Mgalu, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokea hiyo taarifa kwa sababu hakunisikiliza vizuri. Ni kweli natambua na yeye ni mjumbe mwenzangu wa Kamati ya Bajeti, nimesema ni kweli shirika la ATCL ni miongoni mwa mashirika 28 ambayo taarifa ya CAG imesema imepata hasara, ni shirika pekee la kibiashara, lakini nimetoa maoni yangu kwamba kama TANROADS tunaiona inatoa huduma inatengeneza barabara ni kwa nini usifike wakati shirika hili ambalo nalo lina wajibu wa kuchochea sekta nyingine kupitia huduma ya usafiri wa anga, kwa nini nalo lisitoe huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee katika mradi huu wa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na ukaguzi mzuri uliofanywa na CAG, nimeainisha kwamba katika kuhuisha upembuzi yakinifu CAG amesema, tathmini ya athari za mazingira imefanyika, usanifu wa kiufundi na utafiti ya geology umefanyika, utafiti wa kitaaluma ufanisi wa miamba umefanyika. Naomba nimnukuu kwenye ukurasa wa 128, maelezo ya CAG namnukuu: “Kulingana na tathmini iliyofanywa hadi sasa, nilibaini kuwa hakuna udhaifu mkubwa wa kiufundi ambao unaweza kuzuia mradi kufikia malengo mahsusi yaliyokusudiwa.”
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi, wasimlishe maneno Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, hiyo ndio ripoti. Katika hili niiombe Serikali, katika moja ya hoja kwenye mradi huu ni makubaliano ya mkataba ya asilimia nne kwa ajili ya miradi ya kijamii ya maeneo yanayotekeleza mradi huu. Wananchi wa Rufiji, wananchi wa Morogoro vijijini wanasubiri kwa hamu mchango wa asilimia nne wa mkandarasi wa gharama ya mradi kwa ajili ya miradi ya elimu na kwa ajili ya miradi ya afya. Kwa hiyo niiombe Serikali hilo lishughulikie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo yalitolewa maoni hapa pamoja na wachangiaji, tuongeze bidhaa ili tuweze kukusanya mapato Zaidi. Mradi huu unaenda kuleta bidhaa ya umeme, umeme utakuwa mwingi ambao unatakiwa uuzwe nchi za jirani na Serikali imejipanga vizuri, inajenga sasa transmission line ya Singida – Namanga ambayo itawezesha kiwango cha umeme kingine kuuzwa nchi jirani tukapata mapato na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze pia katika moja ya kipaumbele cha Mheshimiwa Waziri Mkuu kusimamia makusanyo ya mapato. Katika hili nimwombe Mheshimwa Waziri Mkuu atakapokuwa anapitia, natambua tulipokuwa tunamwona kwenye ziara mbalimbali akija kwenye halmashauri zetu, anakuja na taarifa kabisa na wengi wale ambao waliokuwa wanajihusisha na ubadhirifu wanasimamishwa, wanapisha uchunguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe katika hili kwa kuwa tunatafuta mapato ya nchi yetu na kwa kuwa Serikali imepewa maelekezo na Mheshimiwa Rais Mama Samia ya kupanua wigo wa ukusanyaji mapato; na kwa kuwa katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameainisha namna gani Serikali ina mpango wa kupunguza mashauri katika Mahakama, katika hili naomba niseme, katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, naomba Serikali iimarishe mamlaka za rufaa za kodi. Fedha ya mapato inaweza ikapatikana pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza kwa mujibu wa taarifa ya CAG, kuna kesi zaidi ya 1,097 zenye thamani ya trilioni 360, utaona ni kiasi gani cha fedha zilizopo kwenye masuala ya kesi mbalimbali. Endapo Serikali itaingilia kati na hapa nakumbuka hata Hayati Dkt. John Pombe Magufuli Rais wetu alitoa maelekezo hayo kwamba mamlaka za kodi za rufaa zisikilize hizi kesi haraka ili kama kuna mapato yoyote Serikali iweze kuyapata.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naipongeza sana Serikali na nampongeza sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu. Ahsante sana. (Makofi)