Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza, naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu lakini niseme Ramadhan Kareem kwa Waislam wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Waziri Mkuu na Mawaziri wote walioko katika Wizara yake bila kumsahau Mheshimiwa Jenista Mhagama. Kwa kweli wananchi wa Iringa wanasema kwamba mambo makubwa yaliyofanyika katika Mkoa wetu wa Iringa hatuwezi kumsahau Dkt. John Pombe Magufuli. Amefanya mambo makubwa ambayo hata kuyasimulia tunashindwa. Wameniambia niseme tu neno moja, gendelage ludodi baba, gendelage ludodi, Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na wote waliochangia kuhusu TARURA kupatiwa fedha za kutosha. TARURA ndiyo ambayo inahudumia barabara nyingi sana za vijijini ambazo ndizo zina matatizo mengi. Kwa mfano, Mkoa wetu wa Iringa mtandao wa barabara za TARURA ni karibu kilometa 4,597.9 na una mvua nyingi sana, milima, maporomoko, hivyo, TARURA inatakiwa iwe na pesa nyingi kwa ajili ya kujenga madaraja, makalvati kwa sababu barabara nyingi zimeharibika. Hizi barabara ni za kiuchumi zinapitisha mazao ya misitu ambapo magari ni mazito yanafanya barabara hizi zinakuwa hazipitiki wakati wa mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitende haki, nitaje baadhi ya barabara ambazo sasa hivi hazipitiki. Katika Wilaya ya Mfindi kuna hii barabara Mtiri – Ifwagi - Mdabulo - Kilosa haipitiki kabisa. Kuna barabara ya Ibwanzi – Lulanda; Nyololo – Mtwango; Mafinga - Mgololo, hizi barabara Mufindi wanapata mateso makubwa mno. Ukienda kwenye Wilaya ya Kilolo kuna barabara ya Boma la Ng’ombe – Jingula. Kata ya Masisiwe, kuna Kata ya Nyanzwa, Kijiji cha Mahenge na Magana kuna madaraja mawili yamekatika kiasi mtandao wa barabara hakuna kabisa. Ukienda katika Jimbo la Kalenga kuna barabara ya Lumuli – Magungu – Magulilwa - Nyenza, hizi barabara ni mateso makubwa sana kwa wananchi wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipokwenda kuwatembelea wakwe zangu kule Mwanza nilikuta kuna barabara pale Ilemela za VETA – Igombe TX; Airport - Nyagugi kama kilometa 18, toka nimeolewa bado hazijafanyiwa kazi yoyote. Naomba Waziri atusaidie kuziangalia barabara hizi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu walimu wanaohitimu katika vyuo vyetu vya elimu. Tunao walimu ambao kwa kweli wamekuwa wakijitolea mara nyingi hasa katika Mkoa wa Iringa hata katika maeneo mengine lakini zinapokuja ajira hawaajiriwi. Pamoja na kuwa Mkoa wetu wa Iringa umefanya vizuri sana katika elimu, tumekuwa tatu bora na hawa walimu wanachangia kwa sababu wamekuwa wanajitolea kwenye masomo ya sayansi na hisabati. Niombe Serikali iwape kipaumbele, hii itasaidia hata wengine kuwa na moyo wa kujitolea hata kama wamemaliza masomo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze pia kuhusu watu wenye ulemavu. Nishukuru Serikali kwamba imetoa ile sheria kwamba watu wenye ulemavu angalau kila mtu aweze kupata ile asilimia mbili. Hata hivyo, kuna wamama wengi ambao wamezaa watoto wenye ulemavu ambao kwa kweli wanapata matatizo makubwa sana kuwalea wale watoto kwa sababu wengi wamekimbiwa na waume zao unakuta wao ndiyo wanahudumia wale watoto kuanzia masomo na malezi. Niombe labda ile asilimia mbili na wenyewe wangepatiwa ili hawa watoto waweze kusomeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni uhaba wa watumishi katika sekta ya afya. Vimejengwa vituo vya afya na hospitali nzuri sana ila kuna uhaba mkubwa sana wa watumishi katika sekta ya afya. Nikichukulia tu mfano Kilolo tuna hospitali ya mfano, ni nzuri sana na imeshakamilika lakini kuna upungufu wa watumishi 93. Wilaya hii kwa ujumla ina upungufu wa watumishi katika sekta ya afya kwa asilimia 40. Niombe kwamba tunapokamilisha hivi vituo vya afya basi iendane na kukamilisha kabisa watumishi kwa sababu bado unaona wananchi wanapata shida sana kwenda kutafuta huduma wakati tayari tumeshajengewa vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu wazee. Wazee ni dawa na baraka lakini wamekuwa na changamoto nyingi sana. Niombe Serikali iangalie changamoto za wazee. Hata leo imezungumziwa kuhusu matibabu ya wazee na nishukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja kwenye kongamano la afya za wazee katika Mkoa wetu wa Iringa na wanakushukuru sana. Lile kongamano lilifanya tukajua changamoto nyingi za wazee, wazee hawahitaji dawa wakati mwingine wanahitaji kuangaliwa wajijue kwamba wanahitaji kula lishe, kufanya mazoezi au faraja. Wazee wengi sasa hivi wameondolewa kulipia kwenye nyumba zao lakini bado wanalipa kodi ya ardhi. Naomba pia ile kodi ya ardhi itolewe kwa sababu tumeshawaondolea kulipia kodi ya nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Bima ya Afya labda sasa izingatie ili wazee wetu waweze kutibiwa, kuchekiwa afya ya macho na vipimo vyote. Pia wanahitaji kupewa dawa lakini hazitoshi na leo lile swali limeeleza mambo makubwa sana kuhusu wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nizungumzie kuhusu matatizo ya maji kwenye Mkoa wa Iringa. Nishukuru sana kwamba Wizara ya Maji inafanya vizuri sana mijini lakini bado vijijini wamama wengi wanapata shida. Mkoa wetu wa Iringa una mito mingi; Mto Lukosi, Mto Ruaha ila kule vijijini maji hakuna. Ni kwa nini wasivute maji ili wananchi wa Iringa wapate maji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda umekwisha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mama Samia, kwa kweli akina mama tunaweza na tunashukuru baba yetu alimteuwa akawa Makamu wake.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ritta Kabati muda wako umeisha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nakupa big up, naunga mkono hoja. (Makofi)