Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nishukuru kwa nafasi uliyonipatia niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nami niungane na wenzangu katika kuwahakikishia Watanzania kwamba nchi yetu ipo katika mikono salama ya mama yetu, Samia Suluhu Hassan. Matumaini makubwa Watanzania waliyonayo kwa mpendwa wetu, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, na kazi kubwa aliyokuwa ameifanya katika nchi hii, niwahakikishie kwamba Tanzania kamwe haitafutika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa lolote linapozungumzia maendeleo au vipaumbele vya nchi katika maendeleo ya wananchi wake pamoja na kiuchumi, kamwe huwezi kuacha kuzungumzia suala zima la elimu. Mabadiliko ya mtaala wa elimu 2005 yaliyofanyika yalisisitiza Masomo ya Stadi za Kazi na TEHAMA yafundishwe kikamilifu katika shule zetu za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, masomo haya yalikuwa na nia kubwa sana ya kuwandaa wanafunzi wetu kutoka shule za msingi kupata stadi mbalimbali ambayo ingewawezesha wenyewe waweze kuja kupata maarifa, ujuzi ili waweze kuutumia katika maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna masomo ya TEHAMA na Stadi za Kazi; haya masomo yanapofundishwa kikamilifu katika shule zetu wanafunzi hupata ujuzi mbalimbali. Mfano, Somo la Stadi za Kazi, kupitia somo hili leo hii somo hili lingekuwa limefundishwa kwa ukamilifu na watahiniwa wakafanyiwa mitihani ya kuwapima kama wamepata ujuzi na maarifa, tungekuwa na wasanii mbalimbali, wanamuziki, wachoraji, mafundi ujenzi na wapishi waliobobea. Kutokana na changamoto mbalimbali somo hili leo halifundishwi kikamilifu na limekuwa ni somo la option, kwamba kuna shule zinafundisha lakini kuna shule zingine pia hazifundishi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na somo la TEHAMA ambalo ni Teknolojia ya Habari na Mawasiliano basi niombe Serikali ione umuhimu sasa wa kuhakikisha kwamba haya masomo yanafundishwa kikamilifu katika shule zetu ili Watoto waanze kupata ujuzi katika umri ule wa shule za msingi na kuendelea. Hii itasaidia Watoto wetu wapate ujuzi na mwisho waweze kujitegemea katika maisha yao, ukilinganisha na kwamba sasa hivi tuna tatizo kubwa la ajira katika nchi yetu tukiwapatia taaluma hii Watoto wetu watapata maarifa na ujuzi wa kutosha ili waweze kusimama wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sera ya nchi yetu ni elimu bure kuanzia darasa la awali mpaka kidato cha nne na hii elimu ni haki sawa kwa watu wote. Naomba nijikite kwenye elimu maalum kwa watu wenye ulemavu, pamoja na kwamba Serikali ni yenye jukumu la kuhakikisha kwamba watu hawa wenye ulemavu wanapata elimu stahiki na watu ambao hawana ulemavu lakini bado kuna changamoto nyingi mno katika utekelezaji wake. Na hii imesababisha kwamba hata watu wale wenye ulemavu Watoto hawa hawapelekwi shule, imebidi wazazi sasa ukipata Watoto wenye ulemavu ni kuwaficha, hatimaye wale Watoto hawapati haki zao za kupata elimu hii inayotolewa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata maeneo yale ambayo elimu hii hutolewa bado kuna changamoto nyingi mazingira yao si rafiki kwa Watoto hao kupata elimu, ikiwepo madarasa wanayotumia, ukosefu wa meza za kusomea, hata wale ambao wenye uoni hafifu hawana lenzi za kusomea pamoja na vitabu vile ambavyo ni sahihi kwa ajili ya Watoto wale wenye ulemavu wa macho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe hawa Watoto ili waweze kupata elimu sawa kama Watoto wa kitanzania ni vema Serikali sasa ione ni namna gani kuweka karibu huduma hii ya elimu maalum katika maeneo yetu ikipendeza nishauri kwamba shule zetu za elimu maalum walau kila wilaya ipate shule maalum ili kila mtoto ambaye anapata ulemavu aweze kupata elimu hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii itaturahisishia kwamba hata walimu ambao wamesomea elimu maalum sasa hivi wanapelekwa kwenye shule zetu za mchanganyiko ambao hawana tatizo hilo la elimu ya watu wenye ulemavu. Walimu hawa watumike ipasavyo endapo tutakuwa na shule zenye elimu, watu wenye elimu maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, walimu hawa wakipelekwa kwenye shule hizo tunauhakika watafanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa mno badala ya kuwachanganya wale Watoto wenye uhitaji maalum na Watoto ambao hawana uhitaji huo inasababisha kwamba yule mwalimu anapewa masomo mengi kufundisha Watoto wenye elimu maalum na wakati huo huo afundishe na masomo mengine. Utendaji wa mwalimu unakuwa mgumu na hivyo kufanya yule mtoto hawezi kufanya vizuri darasani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie suala la Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule, huwezi kuongelea elimu bora kama huna udhibiti ubora wa shule. Idara zetu za Udhibiti Ubora wa Shule, niipongeze Serikali kwa kuwanunulia magari, kwa kuwajengea Ofisi, Ofisi zetu za Idara ya Udhibiti Ubora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo Ofisi hizi hufanya vizuri kwa upande wa shule za msingi tu. Ukiangalia shule zetu za msingi asilimia 90 wanakaguliwa. Lakini ukija kwenye shule zetu za Sekondari ni asilimia 30 tu ndo huwa hukaguliwa na hawa wakaguzi wa udhibiti ubora. Hivyo, huchangia kwamba shule zetu nyingi hazikaguliwi katika shule za sekondari hivyo basi, inasababisha kutogundua mapungufu yaliyopo kwenye elimu kule shule za Sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii inachangiwa kwamba hawa watu wa udhibiti ubora wako ngazi ya kanda sasa ngazi ya kanda kuna kanda zingine sina mikoa miwili kuna kanda zingine zina mikoa mitatu. Sasa mfano mkoa wetu wa Manyara ukiangalia kanda ya Kaskazini Mashariki tuna mikoa miwili, leo hii Mkaguzi wa Kanda akague mikoa miwili kwa maana Manyara na Arusha, Mkaguzi huyo atoke Arusha aende mpaka vijijini na hivi sasa hivi katika kila kata kuna shule ya sekondari, lakini mkaguzi huyo huyo alioko kanda akague shule za sekondari zilizopo kwenye kata zetu, kwanza anatembea umbali mrefu sana kwenda kukagua shule zetu lakini pia wanatumia gharama kubwa kwenda kufanya kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nishauri Serikali sasa ione umuhimu wa kuanzisha Ofisi zetu za Udhibiti Ubora kwa kila mkoa ili hawa watu huduma zao ziwe karibu na waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwa na elimu bora ni lazima pia uangalie maslahi ya walimu. Maslahi ya walimu…
NAIBU SPIKA: Ahsante sana kengele ya pili imeshagonga.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kuunga mkono hoja.