Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu. Na kwasababu, muda ni mfupi basi nitachangia katika jambo moja na kama itatosha basi, nitaenda kwenye jambo la pili. Ninapenda kuishauri Serikali katika suala zima la wafanyabiashara wetu hapa nchini. Tunatambua umuhimu wa wafanyabiashara na lazima Serikali ilione hilo kwasababu hawa wafanyabiashara wakifanya biashara katika mazingira rafiki, kwa maana ya mazingira ya amani yenye kutenda haki ndivyo ambavyo watalipa kodi na wakilipa kodi ndivyo ambavyo hii mipango yote tunayoiongea humu Bungeni inaweza kwenda kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia huko nyuma jinsi ambavyo wafanyabiashara wengi wamepitia kadhia mbalimbali. Na tunamshukuru Mheshimiwa Mama Samia angalao ameliona hilo na ameanza kulisemea kuhusiana na changamoto ambazo wafanyabiashara wanazipata. Sasa pamoja na Mheshimiwa Mama Samia kulisemea, tunaomba watendaji walioko chini wanaosimamiwa na Mheshimiwa Rais haya anayoyasema yaende kutekelezwa kwa vitendo kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanatendewa haki, wanafanyiwa makadirio ya kodi ambayo ni rafiki na yanalipika. Lakini kama haitoshi wanahakikisha kwamba, sheria, taratibu na kanuni zilizoko zinatekelezwa, ili mwisho wa siku huyu mfanyabiashara alipe ile kodi ambayo anastahili kulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho ni muhimu kitazamwe na Serikali ni lazima kuwepo na viwango vya kodi ambavyo ni reasonable, ili mfanyabiashara aweze kulipa, lakini pia tusifikirie kuweka wigo makadirio makubwa ya kodi, tukipunguza makadirio ya kodi tutawafanya wafanyabiashara wengi walipe kodi na kodi itaongezeka. Ukifanya kodi kuwa kubwa maana yake utawapunguza wafanyabiashara, lakini ukipunguza utaongeza na wengine wengi watalipa kodi bila kusumbuana, bila bughudha yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Awamu ya Tano kulikuwa kuna task force ziliundwa, na hizi task force zimewafuata baadhi ya wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi zikawafanyia uhakiki wa hesabu kwa miaka mitatu, mitano ya nyuma iliyopita. Tunatambua kuna tamko limeshatoka, lakini tunaomba hilo tamko liwe kwa vitendo, kuna wafanyabiashara bado leo wanaambiwa wana ma- document wanaambiwa walipe. Hawa wafanyabiashara walishalipa kodi kwa utaratibu unaotakiwa wakapelekewa task force wakaanza tena kukagua kwa upya wanaambiwa tena walipe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali ilifanye hili kwa vitendo kwasababu, nimeona Waziri wa fedha amelisema kupitia vyombo vya habari, lakini hawa watu watapataje comfort kama hawana hata document kutoka TRA kwamba, zile hesabu zako za nyuma sasa hatuzifanyii kazi tena tunatizama mbele. Kwa hiyo, niishauri Serikali wafanyabiashara wote ambao wamepitia adha hii tunaomba muwape comfort ama uhakika wa hayo kwa kuwaandikia barua ili wawe na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kati ya mwaka 2019 na mwaka 2020 wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha katika Mkoa wa Arusha na maeneo mengine nchini hao nao ni kati ya watu ambao wameumizwa kwa kiwango kikubwa na hawajui hatima yao. walipelekewa task force wakanyang’anywa fedha zao tena ni unyang’anyi, wakachukua fedha zote zikaenda Benki Kuu, wakiuliza sababu hakuna sababu. Na tukumbuke utaratibu unasemaje, mfanyabiashara yeyote anapotaka kuanzisha biashara yoyote lazima apate TIN Number, apate leseni ya biashara, kabla ya leseni ya biashara maana yake atapata tax clearance. Maana yeke huyu hana shida yoyote anapewa hiyo leseni ya kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hawa wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha katika Mkoa wa Arusha na maeneo mengine walikuwa wamefuata procedure zote za kuanzisha biashara, wakawa wana leseni zote tena leseni Hai, wanalipa kodi inavyotakiwa, lakini ikaja task force kwa bunduki, kwa magari mengine ambayo hayajulikani sijui namba zipi, wakakwapua fedha zao zikarudishwa BOT. Tunaomba kufahamu nini hatima ya wafanyabiashara hawa? Kwa sababu, walikuwa wanaendesha biashara kihalali kabisa, mmewachukulia fedha zao; Serikali inaema nini kuhusiana na hawa watu ambao mmewanyang’anya fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi hata wako wengine ambao wamepoteza maisha kwa matukio ya namna hii. Mtu unamnyang’anya karibia bilioni kumi, ishirini na anafanya biashara kihalali matokeo yake mtu anafariki kwa pressure, kwa mambo kama haya. Na hawa mnawafidia nini kwasababu wana familia wana watu waliowaacha kwa hiyo, ni vema mkalitizama hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi kuna wafanyabiashara wengine wapo magereza leo kwa kubambikiziwa kesi za uhujumu uchumi, kukwepa kulipa kodi wakati wanalipa kodi, hatujasikia nao hawa mnawafanyia nini? Tunatamani kuona yale ambayo Mheshimiwa Mama Samia ameyanena basi tuyaone kwa vitendo kwa watu kama hao ambao wameonewa kwa namna moja ama nyingine haki itendeke, watoke wawe huru, kama kuna sheria ambazo tunahitaji kuzifanyia marekebisho Serikali mzilete hapa Bungeni tufanye marekebisho Watanzania wafanyabiashara wafanye biashara kwa uhuru, haki na amani lakini wakijua wajibu wao ni kulipa kodi ambayo inaweza ikalipika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)