Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Wete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu- Wataala aliyetupa uhai wa kuimiliki siku ya leo tukawepo katika Bunge hili. Pia niwatakie mfungo mwema kwa wale Waislamu na wenzetu ambao sio Waislamu kwa kutuunga mkono kwa njia moja au nyingine katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa kutoa kauli ya Mheshimiwa Marehemu Shaaban Robert; alizungumza katika kitabu chake cha Adili na Nduguze, akasema kwamba haja ikishughulikiwa kwa matendo humalizika upesi na ikishughulikiwa kwa maneno, huchelewa kama sadaka. Kwani tendo hukidhi haja maridhawa kulikoni maneno na mwenye matendo hula uhondo na asiye matendo hula uvundo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa ruhusa yako naomba nitoe kauli moja tu ya mshairi mmoja wa Kiarabu aliyesema kwamba Inna Safina Tajir illa ljabas. Hakika ya Safina haitembei katika nchi kavu. Nina maana ya kwamba nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, asiogope, asonge mbele na nina Imani kwamba Tanzania hii itapata maendeleo makubwa chini ya uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naomba sasa nijikite kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niende moja kwa moja katika ukurasa wa 71 ambao ulikuwa unazungumzia kuhusu cross cutting issues au masuala mtambuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Visiwa vya Zanzibar; Kisiwa cha Pemba ni kisiwa ambacho kina ukubwa wa square kilometer 198 na Zanzibar 1,666. Visiwa hivi vimebarikiwa na neema kubwa; vimebarikiwa na neema ya visiwa vidogo vidogo vilivyozunguka visiwa vikubwa hivi. Ila visiwa hivi vinapotea siku hadi siku. Suala la mazingira katika Visiwa vya Zanzibar ni tete. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mnamo mwaka wa 1970 huko, kule Tanga Kisiwa cha Maziwe kilipotea na sasa hivi tunajivunia visiwa vyetu vya Zanzibar; na kauli njema kabisa inayozungumzwa hata na wahiribu wakubwa pale Zanzibar wanasema, “Zanzibar ni njema, atakaye aje.” Hata hivyo ukiangalia visiwa hivi ambavyo tunavinadi kwamba Zanzibar ni njema, atakaye aje, kila siku vinapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka maji ya bahari yanakula 5% ya visiwa vile. Kuna maeneo mengine ambayo, bahati nzuri mwaka wa 2019 Mheshimiwa Zungu alifika sehemu moja inaitwa Sipwese Kengeja. Akatembelea katika lile eneo na akaitaka idara inayohusika kufanya upembuzi yakinifu ili kuona athari kubwa ya kimazingira iliyopo katika eneo lile. Kisiwa kimoja tu, ni eneo moja tu hilo ambapo athari yake mpaka sasa hivi tunavyoongea ni kwamba maji ya bahari yanaingia kuzuia kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wanaosoma katika shule, wanaotoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ambao ni vijana wanaotoka Sipwese kwenda eneo lingine la kisiwa wanafunzi wanashindwa kwenda kusoma. Hata Magereza wameyahama maeneo yao, haiwezekani kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa heshima kubwa na taadhima, basi tufanye upembuzi yakinifu katika visiwa hivi vya Unguja na Pemba kuona je, athari ya mazingira iko kwa kiwango gani ili tuvihame visiwa hivi tuweze kuringia Muungano huu wa Zanzibar na Tanganyika? Kwani vikipotea visiwa vya Zanzibar, tayari tutakuwa hatuna tena nchi ya kusema kwamba tuna Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)