Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa
Spika, ahsante sana nakushukuru sana nianze kwanza kwa kukushukuru wewe kwa kuliongoza Bunge letu vizuri tunakupongeza sana na hasa kwa kuchaguliwa tena kuwa Spika. Lakini tunampongeza pia Naibu Spika wako kwa kazi nzuri mnayoifanya tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nichukue nafasi ya pekee kabisa kumpongeza Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kupata kibali mbele ya Mwenyezi Mungu kuliongoza Taifa letu la Tanzania hatuna mashaka naye na sisi wengine ambao tumefanya naye kazi tunajua udhibiti na umahiri wa uongozi wa Mama Samia kwahiyo tunamtakia kila la kheri na tutamuunga mkono sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu niseme kitu kimoja kipekee kabisa sifa ya ziada aliyonayo Mama Samia toka tumepata uhuru katika Taifa letu hatujawahi kupata Rais mwanamke kwahiyo ana sifa ya ziada na sifa hiyo hata kama kuna mtu mwingine yoyote angetamani hawezi kupata sifa ya kuwa mwanamke na kuongoza sasa Taifa letu. Kwa hiyo sisi tunaamini kabisa atatuvusha vizuri lakini kwa kweli niungane na watanzania wote kupeana pole kwa msiba mzito wa Hayati Dkt John Pombe Magufuli Rais wetu Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi, nitaendelea kumkumbuka nina heshimu uteuzi wake alionipatia katika kipindi cha miaka mitano lakini kwa moyo wa shukrani sana ninamshukuru mama yetu Samia Rais wetu kwa kuendelea kuniamini na kuniacha nimsaidie Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye Wizara hii namuahidi utumishi uliotukuta na nitatekeleza majukumu yangu sawasawa. (Makofi)

Kwa kweli nitakuwa sijajitendea haki kama sitompongeza kwanza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuendelea kuaminiwa kuwa kwenye nafasi hiyo. Lakini vilevile ninamshukuru sana mimi najua ni kwa kiasi gani Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa ni mwalimu wangu kwenye kazi hii ambayo ninaifanya chini ya Ofisi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu nakushukuru sana na ninakuombea dua kwa Mwenyezi Mungu na ninaomba niwaambie watanzania na Waheshimiwa Wabunge hakika ndugu yetu Kassim Majaliwa Majaliwa ana kitu cha ziada katika moyo wake ana kitu cha ziada katika utumishi wake na ninaamini Mwenyezi Mungu alitupatia Waziri Mkuu huyu kwa makusudi maalum. Mheshimiwa Waziri Mkuu ninakushukuru sasa sana, nakushukuru na ninaomba nikuhakikishie nitaendelea kuwa msaidizi wako nikizingatia miongozo na taratibu zote ambazo umekuwa ukitupatia katika kukusaidia ili haya mambo yote unayoyasimamia yafanikiwe ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba nimpongeze Makamu wa Rais ana sifa na vigezo vyote tulivisema ndani ya Bunge sitaki kuvirudia. Lakini kwa namna ya pekee niwashukuru watendaji wote Ofisi ya Waziri Mkuu Makatibu Wakuu, Manaibu na Makatibu Wakuu ambao tulifanya nao kazi kwa bajeti hii tunayoimaliza kwa sasa ninawashukuru sana. Lakini kwa namna ya pekee nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kweli kwa kuamua kuniteua kugombea nafasi ya Ubunge kwenye Jimbo la Peramiho naishukuru Kamati Kuu, iliyoongozwa na Hayati Dkt John Pombe Magufuli lakini nashukuru Sekretarieti iliyoongozwa na Dkt Bashiru, lakini nashukuru pia Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ilinithibitisha lakini nawashukuru wapiga kura wa Jimbo la Peramiho kazi inaendelea ahsanteni sana kwa kunirudisha tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Kamati zote tatu ambazo Ofisi ya Waziri Mkuu tunafanya nao kazi kamati ya Katiba na Sheria chini ya uongozi wa ndugu yangu Omary Mchengerwa ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora walifanyakazi kubwa sana ya kutushauri katika kipindi hiki chote akisaidiwa na Makamu wake ndugu yangu Najma na Wajumbe wote wa kamati. Lakini kwa kweli Kamati ya Bajeti Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti tulipitisha fungu la Bunge kwa kweli tunawashukuru sana na Kamati ya masuala ya Ukimwi na Dawa za Kulevya ninawashukuru sana kwa miongozo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru Wabunge kazi ya kushughulikia masuala ya Bunge si ndogo unakutana na Wabunge wenzako kila siku lakini kwa kweli ninawashukuru sana ninawaahidi utumishi wa unyenyekevu ushirikiano katika kila siku ili kuweza kuyatekeleza majukumu haya sawasawa. Nawashukuru Manaibu Mawaziri ambao nafanya nao kazi.

Mheshimiwa Spika, mambo ni mengi ambayo tunatakiwa kuyajibu kwenye mkutano wako huu wa leo lakini naomba tu niseme kwamba tumepokea hoja za Wabunge zote na tutajitahidi kuzijibu kwa maandishi na kila hoja zote tutaziwasilisha kwenu Wabunge wote kwa maandishi ili angalau muweze kuona tumeweza kufanya nini katika kipindi hiki chote ambacho tumetekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa moja kabla sijaingia katika mambo mengine naungana mkono na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi lakini vilevile na Waziri mwenzangu wa masuala ya Uwekezaji na hasa kuitikia wito wa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha kwamba tunatengeneza mazingira bora ya uwekezaji nchini na kuondoa vikwazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikwazo kikubwa ambacho kiko katika Ofisi yetu ni mfumo huu wa kuratibu vibali vya ajira za wageni. Kwahiyo jambo hili sisi tumelichukulia kwa uzito mkubwa kwanza tunafikiri ni lazima tufanye mabadiliko ya sheria. Sheria ya uwekezaji na sheria ya vibali vya ajira za wageni ziweze kusomana vizuri, na Wabunge mmetushauri vizuri sana hapa tuone je sheria hizi mbili kwa mazingira tuliyonayo sasa kweli ni sheria Rafiki? Zinaweza kutusaidia kweli kuruhusu uwekezaji ninaomba nilihakikishie Bunge lako kwamba kazi hiyo tumeshaianza na tunataka tuwe na mfumo mzuri wa kuharakisha vibali vya ajira za wageni bila kuzuia ajira za watanzania wenyewe. Kwahiyo jambo hilo tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili tumefikiri tuwe na mfumo kwasababu utoaji wa vibali huu umeambatana na mazingira ya rushwa sana kwahiyo tumeshatengeneza mfumo shirikishi ambao utajumuisha watu wa Uhamiaji, wenzetu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye tunasimamia vibali hivyo vya ajira za wageni tutakuwa tunasoma vile vibali on line kila kibali kwahiyo hakuna tena temptation ya rushwa na tutauzindua mfumo huo haraka sana iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine tumesema kwamba tunazungumza tatizo la ajira katika Taifa letu lakini ni lazima tujue tunahitaji nini ili watanzania na hasa vijana waajiriwe. Tumeamua kufanya tafiti kubwa mbili ambazo tumeanza kuzifanya, utafiti wa kwanza tunataka kufanya utafiti wa hali ya nguvu kazi tuliyonayo nchini je inaendana na mahitaji tuliyonayo sasa? Na kazi hiyo tumeanza kuifanya.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi mmeona kama wenzetu TAMISEMI wanabadilisha tahsusi (combinations) ambazo zinatakiwa zianze kusomwa na vijana wetu. Lakini ni lazima tunapobadilisha hizo combination ama tahsusi ziendane na mahitaji ya ujuzi kwa sasa ndani ya Taifa letu kusudi watoto wa Kitanzania kama ana opt kusoma kitu fulani kiendane na mahitaji ambayo yanahitajika ya ujuzi kwenye Taifa letu. Kwahiyo tunafanya hizo tafiti ili tuende sambamba lakini tumekubaliana na Waziri wa Elimu pia na yeye tutafanya naye tafiti zetu tutakwenda kukaa nao kusudi tujue tuwafundishe nini vijana wa Tanzania elimu ambayo inatakiwa iweze kutumika ndani ya Taifa hili. Kwa hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu tumejipanga tunadhani ni wakati muafaka wa hayo kuyafanya kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Wabunge hapa wameomba sana ile fedha tunayopewa kwaajili ya skills development iongezeke wamegundua kwamba imepungua. Nakubaliana nao kwamba tunatakiwa kuiongeza ila sisi tumepata challenge katika utoaji wa mafunzo hayo ya ujuzi. Tumefanyakazi nzuri sana na wajumbe wamesema Wabunge wamesema na ripoti ya kamati imeeleza eneo hili limeweza kufanyiwaje kazi vizuri lakini tumeanza kujitafiti na sisi hivi ni kweli mafunzo ya ujuzi tunayoyatoa sasa kila siku tunasema watu wafundishe masonry sijui wafundishwe ushonaji, sijui wafundishwe mambo hayo ambayo ni skills ambazo zimezoeleka kila siku.

Mheshimiwa Spika, lakini tunajua sasa hivi mageuzi makubwa ya uchumi yanakwenda kwenye green economic, blue economic na TEHAMA. Kwa hiyo, kuna haja ya mafunzo haya tutakayoanza kuyatoa kwa bajeti ya kuanzia mwezi wa saba tunafikiri sasa yaende huko kwenye green economic, kwenye blue economic na kwenye TEHAMA. Tukifanya hivyo tunaweza tukasaidia sana Taifa letu na sisi likapiga hatua kwa haraka. Kwahiyo tunadhani ni wakati muafaka.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine ambalo tutaliwekea mkazo sana ni eneo la local content tuna mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania kama tukijipanga vizuri kwenye local content watanzania watafaidika sana kwenye mradi huu wa bomba la mafuta. Lakini vile vile lhata hii miradi mingine ya kimkakati tunadhani sasa ni kipindi ambacho ni lazima tusimame imara kwenye dhana ya local content watanzania wengi waweze kufaidika na miradi hii ya kimkakati. Kwahiyo nadhani haya yote yatatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo labda nikilisema kwa haraka ni hili la sekta ya hifadhi ya jamii, kwanza naomba tu nitoe taarifa kwenye Bunge lako Tukufu thamani ya mifuko yote ukijumuisha mifuko yote Worker’s Compensation, NHIF, NSSF na PSSSF mpaka sasa thamani ya mifuko hii imeishafika trilioni 11.510 kwa hiyo, thamani imeendelea kuongezeka. Lakini ninachotaka kusema hapa ni nini. Historia ya sekta ya Hifadhi ya Jamii toka tulipopata uhuru imekuwa ikibadilika kulingana na wakati na hali halisi ya mazingira. Hata tunachokifanya sasa ni muendelezo wa mabadiliko hayo hayo ya sekta ya Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetuagiza mambo ya kufanya lakini baada tu ya Uhuru unaona mwaka 1964 Serikali ilianzisha Mifumo ya Hifadhi ya Jamii kwa mfano NPF ilianzishwa mwaka huo, lakini mwaka 1999 ilianzishwa NSSF, mwaka 2006 -2012 tulibadilisha mfumo wa LAPF na mfumo wa GPF, kahiyo mwaka 2018 tumefanya mageuzi mengine makubwa.

Mheshimiwa Spika, Lengo la mageuzi haya ni kuifanya sekta iwe sustainable, kwa hiyo, hata sheria hizi tulivyobadilisha na ku-merge hii mifuko lengo letu ni kufanya mifuko hii iwe endelevu na iwe imara iweze kutusaidia. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge baada ya kumaliza actuarial tukishapata actuarial ripoti ya PSSSF, tukapata actuarial ripoti ya NSSF ninawahakikishia Serikali itakuwa imejipanga kumaliza matatizo ya mifuko hii na hasa mfuko wa PSSSF ambao sasa tunataka kuupa kikokotoo kitakachoweza kuwa sustainable kwa faida ya wanachama lakini na uhimilivu wa mfuko na uendelevu wa mfuko. Kwa hiyo, sisi tunapokea mawazo yenu yote lakini tukipata actuarial ripoti itatusaidia sana kufanya maamuzi endelevu.

Mheshimiwa Spika, kuna miradi kweli ambayo kidogo ilikuwa inasuasua, naomba niwahakikishie kwamba tumejipanga kuhakikisha miradi hiyo haiendelei kuleta hasara. Serikali ya Awamu ya Tano iliikuta miradi hiyo imeanza kutekelezwa, ilichokifanya ni kufanya maamuzi magumu ya kuifanya miradi hiyo isiwe ni hasara lakini iendelee na kujenga faida kwa wanachama na kwa mfuko kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, tunayo miradi mingi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba nimshukuru sana Waziri Mkuu yeye mwenyewe yuko mstari wa mbele kuratibu miradi yote ambayo iko ndani ya Ofisi yetu. Mmeona tumeratibu kuhamishia Serikali Dodoma, watumishi takribani elfu kumi na nane wameshahamia hapa. Pia mmeona ameratibu mazao ya kimkakati kahawa, chikichi, chai, vyote ameviratibu vizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie kuna miradi mingine mikubwa miwili sasa hivi tunaendelea kuiratibu. Mradi wa kutengeneza mnyororo wa thamani kutosheleza mahitaji ya mbegu nchini ambayo utatolewa taarifa na Wizara ya Kilimo unaratibiwa na Ofisi yetu na mradi wa uvuvi ambao unakwenda kununua meli nne za uvuvi Tanzania Bara na meli nne za uvuvi Tanzania Visiwani ambao nao utaratibiwa na Ofisi yetu. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri na tunakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaratibu suala la lishe kuhakikisha tunaondoa utapiamlo nchini. Hapa naomba nimpongeze sana Mbunge mwenzetu Neema Lugangila, kwa kweli huyu ni Balozi wa Lishe. Nampongeza sana kwa kazi nzuri anayoifanya. Vilevile, naomba nichukue nafasi hii kuipongeza ile Kamati ya Wabunge ya Masuala ya Lishe na yenyewe imetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakwenda vizuri kwenye suala zima la lishe bora Tanzania. Kama Ofisi ya Waziri Mkuu tunaliratibu hilo lakini bado kuna mikoa inafanya vizuri kwenye uzalishaji wa chakula lakini kiwango cha utapiamlo na udumavu kipo juu. Kwa mfano, Mkoa wa Iringa hali bado siyo nzuri, kiwango cha kitaifa ni asilimia 40 lakini Iringa wamefika asilimia 47.1 na Songwe pia wamefika asilimia 43.3. Kwa hiyo, ni lazima tuende na mikakati ya pamoja ili kuhakikisha kwamba tunasaidia mikoa hiyo waweze kufanya vizuri kwenye suala la lishe ili kuondoa udumavu. Tukijipanga vizuri kwenye elimu na kila kitu tusipoondoa udumavu tutakuwa na watoto ambao bado hawafanyi vizuri katika masomo yao darasani. Kwa hiyo, hilo nalo tunaliratibu na tunakwenda nalo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeratibu masuala ya uchaguzi na tutatoa maelezo vizuri kwenye taarifa yetu na majibu ya hoja tutakayoyatoa. Uratibu wa uchaguzi uliofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu umepelekea Serikali kuwa madarakani na sisi Wabunge kuwa humu ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya vizuri kuratibu tatizo la dawa za kulevya nchini. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu mpaka sasa asilimia 90 ya dawa za kulevya zilizokuwa zinaingia kutoka nje ya Tanzania sasa haziingii tena na tutaendelea kusimama vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tuna mambo mengi ya kujibu lakini basi itoshe kwa haya machache ambayo nimeyasema. Nichukue nafasi hii kuunga mkono hoja asilimia mia moja na tutaleta majibu kwa maandishi ili kuweza kutosheleza kiu ya Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)