Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, naomba kuchangia hotuba ya Bajeti ya Serikali za Mitaa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza kabisa, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Ummy Mwalimu kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa. Ni kwamba mashine iliyotoka ilikuwa ni ya kusaga na kukoboa na mashine iliyoingia sasa hii ni ya kusaga na kupepeta. Kwa hiyo, shukrani sana Mheshimiwa Samia kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najikita katika sehemu ya utawala bora katika Halmashauri zetu na Serikali za Mitaa katika nchi hii. Serikali imekuwa ikitafuta fedha hizi kwa shida; inakusanya kodi kwa wananchi kwa ajili ya kuhudumia miradi ya maendeleo iliyopo katika Halmashauri zetu. Hii miradi inayopewa fedha ni ya maendeleo kwa ajili ya kuwaondolea wananchi kero na adha walizonazo katika miradi ya elimu, afya, barabara, maji na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na utaratibu wa kufanya kazi zake za miradi ya maendeleo za ujenzi kwa kutumia force account. Utaratibu huu umekuwa na mafanikio kwa ajili ya kupunguza gharama za uendeshaji katika miradi hii katika nchi nzima. Kuna maeneo hatua hii imekuwa ni sehemu ya chaka la kuibia fedha za Serikali kwa kiwango cha kuchota kwa koleo; siyo kiwango cha kuchota kwa kunywa kwa mrija; zinachotwa kwa koleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika Jimbo la Sengerema, namshukuru sana aliyekuwa Waziri wa Fedha na sasa hivi ni Makamu wa Rais, kwani nilikwenda kwake katika kumlilia kuhusu fedha za miradi ya maendeleo ambazo zimekwama katika Halmashauri ya Sengerema na bahati nzuri nilipewa fedha karibu shilingi 2,212,000,000/=. Fedha hizi zilikuwa katika mgawanyo ufuatao:-

Mheshimiwa Spika, kuna fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya shilingi milioni 749 ambazo ni za kuanzia. Wakati huo huo nikapewa fedha nyingine kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kumi shilingi milioni 125. Bado nikapewa fedha tena shilingi milioni 188 kwa ajili ya kumalizia maabara zilizojengwa na wananchi kule kwa nguvu zao wenyewe kwa ajili ya kufanyia finishing; nikapewa fedha nyingine kwa ajili ya kumalizia zahanati shilingi milioni 150; na nimepewa fedha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kumalizia Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, kipi kilichotokea katika hali hii? Kule kuna kazi. Kwa mfano, kazi moja tu ya ujenzi wa Halmashauri ya jengo la Halmashauri kwa kutumia nafasi hii ya kuwaachia wazi hawa Wakurugenzi wetu, tayari hao ma-engineer na watu wa manunuzi wanatumia nafasi hii kuchimba msingi na kujenga msingi wa jengo la Halmashauri hiyo na structure za nguzo fundi analipwa shilingi milioni 160. Hii ni hatari kubwa sana. Jengo ni dogo, halina upana wowote. Sasa kama kwangu Tabasam kuna hali hii, je, katika Halmashauri nyingine karibu 200 kukoje?

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Ummy Mwalimu akija kumalizia hotuba yake, atoe na majibu kwa hili, kwa ajili ya ndugu yake mimi Tabasam, vinginevyo nitaing’ang’ania shilingi na kama hali hii kule Sengerema itaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, katika ujenzi huu kuna hii shilingi bilioni moja inajenga majengo matano. Wodi inajengwa kwa shilingi milioni 204; kuna ujenzi wa kujenga incinerator, hii tu ya kuchomea takataka shilingi milioni 30. Kajengo kadogo, yaani kakizimba, sijui tunaitaje kwa Kiswahili, maana yake ni kichomea taka, kwa shilingi milioni 30. Jengo kwa ajili ya kufulia nguo shilingi milioni 115; jengo kwa ajili ya mortuary ambayo haina cold room shilingi milioni 130. Hii ni hatari kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hili suala la Sengerema Mheshimiwa Ummy, unafahamu kuna Wakurugenzi wengine wanajua tayari wanatakiwa kuondoka, kwa hiyo, wanafanya haraka sasa kunyakua hizi hela. Nakuomba sana uzuie matumizi ya hizi fedha kule Sengerema haraka iwezekanavyo. Peleka timu ikaangalie ile hali iliyoko kule, kuna wizi wa kutisha! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri hizi tunashangaa zinapewa hati safi, lakini Sengerema imepewa hati yenye mashaka. Ni maajabu makubwa! Kuna fedha zinazokusanywa katika hili suala la utawala bora na makusanyo ya Halmashauri ya fedha za masoko na magulio katika own source. Fedha za kwenye kutumia POS hizi mashine za kukusanyia ushuru shilingi milioni 350 zimeibiwa, lakini watumishi bado wapo kazini.

Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo, alikuwepo pale DT Sengerema, ameondoka na shilingi milioni 250. Pamoja na Mheshimiwa Jafo kuja Sengerema na kuagiza kwamba wakamatwe mara moja, bado wapo kazini. Mheshimiwa Jafo aliagiza watu wa TAKUKURU Mkoa wafanye kazi hiyo, jamaa anaendelea kupeta na anaendelea kula ulanzi huko kijijini. Hii ni hatari kubwa sana katika nchi hii!

Mheshimiwa Spika, huko kwenye Wizara ya TAMISEMI ndipo ambako ni chaka la kupotezea pesa za Serikali. Ukisikia pesa za Serikali zinakusanywa; na tundu lipo wapi? Tundu lipo kwenye Halmashauri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ummy Mwalimu una kazi kubwa sana dada yangu. Una kazi kubwa sana kwenye kuzuia hilo tundu. Atakuwa anachota Mheshimiwa Mwigulu Nchemba halafu tundu kule linatoboka na wananchi wanaendelea kupata shida.

Mheshimiwa Spika, tunavyozungumza na wewe hapa ni kwamba majengo ambayo yanafanyiwa kazi kule hayalingani na thamani ya fedha. Wanaleta maelekezo kutoka TAMISEMI yanakwenda kule kwamba jengo moja la kumalizia kupiga ripu na kumalizia bati shilingi milioni 12, siyo kweli. Wananchi wanajenga jengo, wanamaliza boma kwa shilingi milioni sita, halafu kulimalizia jengo, kupaka rangi na kuweka madirisha na milango shilingi milioni 12; ni jambo ambalo halikubaliki.

Mheshimiwa Spika, kuna haya maboma ambayo anayataja Mheshimiwa Ummy Mwalimu katika hotuba yake; maboma yaliyopo kwetu kule ni mengi. Halmashauri moja kama Sengerema tu ina maboma karibu 200 na kitu. Sasa maboma haya hatujaambiwa yatatekelezwa namna gani. Haya maboma hayako kwangu tu, yapo karibu kwa Wabunge wote wanaotoka katika Halmashauri za Wilaya. Wanayo maboma ya kutosha; maboma ya zahanati hatujaelezwa kwamba kuna maboma labda 1,000 yatatekelezwa hivi; ya zahanati, kuna maboma ya madarasa, kuna maboma ya nyumba za walimu, kuna maboma ya vituo vya afya yatamalizwa namna gani? Hili hatujaelezwa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ummy katika hotuba yake amesema amekarabati shule, mimi nashukuru. Shule ya Sengerema Sekondari imekarabatiwa kwa shilingi bilioni 1.2 lakini shule hii…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. Ahsante Mheshimiwa.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Namwomba tu Mheshimiwa Ummy Mwalimu aangalie suala la Sengerema kwa upande wa watumishi wake kuanzia Mkurugenzi, Engineer na DT, ni kwamba tayari sasa hivi wanajua safari yao imeiva, wanataka wanyakue hizi fedha haraka. Nakuomba sana uzizuie hizi fedha kwa haraka sana. Hizi fedha zizuiwe leo dada yangu, la sivyo nitakunyang’anya shilingi.

Naunga mkono hoja. (Makofi)