Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Moja kwa moja niende kwa upande wa TAMISEMI katika kipengele hiki hiki cha TARURA. TARURA imekuwa kama kibogoyo asiyekuwa na meno, lakini analazimishwa kula mifupa. Nasema maneno haya kwa sababu TARURA hawana shida. TARURA siyo tatizo, tatizo ni bajeti wanayopewa. TARURA wapo tayari kabisa kufanya kazi, lakini fikiria bajeti nzima ya barabara, TARURA wanapewa asilimia 30 badala ya kupewa asilimia 40 mpaka 50. Mimi napendekeza TARURA waongezewe fedha kwa sababu wanachezea nafasi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilimsikia Mheshimiwa Waziri akisoma hapa, anasema TARURA kwenye kilometa za mraba, wako 144,000. Sijui kama ni kweli, lakini pia ina wingi sana wa barabara. Kwa hiyo, TARURA watengewe fedha za kutosha ili kilio hiki cha Watanzania basi waweze kufutwa machozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakwenda Dar es Salaam katika jiji ambalo ni kubwa, ambalo ni kitovu cha biashara na ni muunganiko wa Mikoa yote ya Tanzania. Dar es Salaam kumekuwa na msiba na kilio katika majimbo yote ya huko kuhusiana na barabara hasa zile za mitaa na barabara kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara za Dar es Salaam nyingi ambazo hazipitiki ni suluhisho la foleni za Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa mfano, Barabara inayotokea Kairuki kupitia Mikocheni, barabara ile inayopitia shoppers ilikuwa suluhisho kabisa la foleni za Dar es Salaam. Mtu anayesafiri Dar es Salaam kutoka Bunju kuelekea Posta ambapo ndipo kwenye Ofisi za Serikali, anachukua masaa matatu kama anatoka hapa kwenda Morogoro.
Mheshimiwa Spika, mtu huyu anafika ofisini anasinzia, akili imechoka, uwezo wake wa kufikiri umeshapotea. Tunaanza kusema watu wetu hawa-perform vizuri, hawa- perform kwa sababu hawapo active, wakifika pale kama mtu ametoka kulala kwenye msiba. Barabara nyingi ni kilio. Kuna barabara moja ipo Ununio; mwaka 2020, baada ya mvua hizi kunyesha nyumba 10, yaani familia 10 zilihama kabisa zikaondoka wakaenda TARURA wakaambiwa chimbeni mfereji. Hakuna miundombinu pale ya mfereji kuelekeza maji baharini. Wale watu wanapeleka wapi haya maji? Familia 10 zipo juu ya nyumba. Sasa hivi wanapiga simu wanasema Mheshimiwa Njau, tunaondoka sasa, wananiaga niwapeleke wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kitu kimoja. Barabara ni kwikwi Tanzania nzima. Nikisema za vijijini, Mikoa inayohusiana na Kilimo, inayohusiana na biashara na mazao, hakika tunadumaza pato la Taifa. Kwa sababu kama vijijini barabara ni mbovu, hawawezi kwenda kwenye Wilaya, hawawezi kwenda kwenye Mikoa kupeleka mazao yao, tunasema hatupati mapato. Barabara ni suluhisho la biashara na barabara ni suluhisho la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wengi wanaosimama hapa wanalia juu ya bajeti sehemu fulani. Twende tukatoe mzizi wa fitina kwenye miundombinu. Tukitoa hapa kwenye barabara, tunaweza kwenda vizuri. Pia niseme, hata wakijenga barabara hizi, kama Serikali hatujaweka nguvu kubwa katika kujenga mifereji, ni kazi bure. Barabara zinachongwa leo, baada ya siku tatu maji yanajaa na barabara zinakuwa vile vile. Kwa hiyo, lazima tuweke miundombinu ya mifereji. Kwa mfano, pale Mikocheni Shoppers, kuna adha ya mafuriko; pale ni mifereji tu ndiyo mchawi.
Mheshimiwa Spika, ikipatikana mifereji thabiti, barabara zikajengwa vizuri, barabara hizi zitakuwa imara. Barabara zinaharibika kwa sababu hakuna mifereji. Tuna wataalam wetu, wakandarasi; kuna msiba na kilio cha Makandarasi. Kwenye ripoti ya CAG ameainisha zaidi ya shilingi bilioni 81.52 hazijalipwa kwa Makandarasi, tunategemea kupata matokeo chanya kwa mtu ambaye anakudai na unampa kazi mpya! Hatuwezi kupata matokeo chanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukalipe madeni haya ya Makandarasi ili tuweze kuanza nao vizuri na kumaliza vizuri. TARURA hawa hawa ambao wanatengewa asilimia 30, wanaidai Serikali shilingi 125,854,000/=. Hivi kweli hawa ambao fedha zao hazitoshi, bado wanadai; tukawalipe TARURA Ninaongea haya kwa sababu tuna barabara za kimkakati; wakati tunatenga bajeti, hebu tuweke kipaumbele kwenye barabara za kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kawe tuna barabara inatoka Mabwepande kuelekea Kibamba - Mbezi, ile barabara ni ya kimkakati kabisa kwenda kupunguza foleni, lakini barabara ile imekaa kama haina mwenyewe. Kuna barabara zimejengwa nusu; barabara ya Shoppers imejengwa kwa lami nusu, mwaka wa nne leo watu wanachungulia na kurudi, iko nusu. Twendeni tukamalize miradi baada ya kuianza, ndipo tuweke miradi mipya.
Mheshimiwa Spika, nashauri wakati tunaanza kupanga bajeti, tuangalie miaka ya nyuma: Je, tulikuwa tuna kiporo? Siyo kila siku tunaibua miradi mipya wakati ya zamani imesimama. Tutakuwa kila siku tunaelemewa na tunaonekana hatufanyi kazi, lakini watu wanachapa kazi.
Mheshimiwa Spika, ninakwenda kwenye ulipwaji wa motisha na madeni. Viongozi kama alivyosema msemaji aliyepita, Madiwani hawana thamani. Kwa sababu hawa ndio wanaosimamia mapato yetu, twendeni tukawape motisha, tusimame nao, tuwasemee. Madiwani ukikaa nao anakwambia posho yangu; ananung’unik! Tunakutana na Madiwani, anasubiri apate huruma ya Mkurugenzi wakati yeye ndiye anatakiwa kumwajibisha Mkurugenzi. Hatuwezi kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, twende tukapange upya. Nina imani na Serikali hii, sasa nina imani Mheshimiwa Mama Samia amesimama na viongozi wake, siwezi kuwakosoa kwa sababu ndiyo wameanza, nawaona wanaweza kufanya mabadiliko makubwa na nchi hii ikaenda kuona maisha mengine tofauti.
Mheshimiwa Spika, nasemea Jiji la Dar es Salaam kwa sababu mwisho wa siku Jiji la Dar es Salaam ndiyo jiji ambalo limekusanya mapato ya ndani makubwa kwa asilimia 104, limevuka asilimia 100. Kama Jiji hili ndivyo lilivyo, basi turudishe mapato kule chini, kwa maana ya miundimbinu. Miundombinu ikipatikana, wafanyabiashara watafanya biashara zao na wafanyakazi watafanya kazi vizuri wala hutasikia minong’ono.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninakushukuru sana. (Makofi)