Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya TAMISEMI. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kunijalia afya na kuniwezesha kusimama hapa na kuchangia hotuba katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy kwa uteuzi. Sina mashaka na utendaji wake, ninaamini kabisa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu atasimamia Wizara hii sawa sawa ili mambo yaweze kwenda sawa sawa huko chini. (Makofi)

Mheshimwa Naibu Spika, siku zote mazingira bora ya kufundishia na kujifundishia yanategemeana sana na uwepo wa miundombinu rafiki na wezeshi. Hali hii huko chini haipo. Ninaposema hali hii huko chini haipo, ni ukweli usiopingika, miundombinu ya kufundishia siyo rafiki kabisa. Mimi natokea Mkoa wa Tabora ambao ni moja kati ya mikoa iliyoko pembezoni na ni moja kati ya mikoa ambayo ina changamoto kubwa sana za miundombinu ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mkoa wa Tabora ni moja kati ya mikoa mitatu ya juu ambayo inaongoza kwa watoto kupata ujauzito. Hii inatokana na watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule zilipo. Vile vile Jimbo la Tabora Mjini ni moja kati ya majimbo ambayo yana changamoto kubwa sana ya Shule za Sekondari. Mtoto anatoka umbali mrefu mno kufuata shule ilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano wa Kata chache za Tabora Mjini. Kuna Kata ya Kakola ambayo haina kabisa Shule ya Sekondari, haina! Watoto wa Kakola, anatoka Kata ya Kakola umbali wa zaidi ya kimometa 30 kufuata shule kwenye Kata ya Uyui. Anapotembea kutoka Kakola kuja Uyui, siyo kwamba anatembea kwenye barabara, ni pori kwa pori mpaka afike kwenye Kata nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yanayomsibu mtoto wa kike kwenye maeneo hayo ni mengi sana. Tutalaumu wazazi, lakini mwisho wa siku wazazi pia wanajitahidi kwa kadri inavyowezakana. Naiomba sana Serikali, iangalie uwezekano wa kupeleka Shule za Kata kwenye maeneo ambayo hayana Shule za Kata hasa kweye kata za pembezoni katika Jimbo la Tabora Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Shule nyingine za Kata ziko katika Kata nyingine. Kwa mfano, Kata ya Gongoni ambayo mimi ndio natokea, Kata ile tunaambiwa kuna shule pale, lakini shule hii iko kule Lwanzari ambako ni Kata ya Ng’ambo. Kwa hiyo, mtoto anapofaulu katika Shule za Kata ya Gongoni anatakiwa moja kwa moja aende Lwanzari, atembee zaidi ya kilomita 20 kufuata Shule ya Sekondari ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii taarifa kwamba kila Kata ina Shule za Sekondari, kwa kweli siyo sahihi. Tatizo hili lipo kwenye kata nyingi. Kata ya Kanyenye; Shule ya Sekondari ya Kata ya Kanyenye inapatikana katika Kata nyingine kabisa ya tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, Wizara iangalie…

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami Mbunge ninayetoka Mkoa wa Tabora. Anasema kutoka Gongoni kwenda Lwanzari ni kilometa 20, hapana, ni kilometa nne. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Mwaifunga unaipokea taarifa hiyo?

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, inategemea na Gongoni sehemu gani? Kwa hiyo, asichukulie Gongoni ya hapa mpaka pale kwamba ni kilomita nne. Kwa hiyo, naomba atulie kwanza, naye ataweza kuchangia kwa nafasi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto iliyopo kwa shule ni kubwa sana. Kata ya Itonjanda katika Jimbo la Tabora Mjini ni kata ambayo ina changamoto kubwa sana ya Shule ya Sekondari. Kuna Shule ya Sekondari moja pale Itonjanda Centre, lakini wazazi wa Kata ile katika Kitongoji cha Kilino waliamua kwa nguvu zao kujenga Shule ya Msingi. Walipata msaada wakajengewa madarasa mawili na ofisi ya mwalimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kujengewa madarasa yale, watoto wa Kitongoji cha Kilino wanasoma darasa la kwanza na la pili peke yake, basi. Ukitaka kumuendeleza mtoto wako madarasa yanayofatia ni lazima uende centre. Kutoka Kilino kwenda pale centre ni umbali mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazazi wale waliamua kujichangisha wenyewe, wakaweka mawe, wakanunua na cement. Kwa masikitiko makubwa cement ile imekuwa jiwe, kwa sababu Serikali imeshindwa kuwasaidia kuendelea kujenga madarasa yanayofuata ili watoto wao waweze kupata elimu, ukizingatia kitongoji kile watu wanaoishi kule ni wafugaji wa jamiii ya Kisukuma, walioamua kwa dhati ya moyo wao kwamba watoto wao waende shule, lakini wakisoma darasa la kwanza na pili, biashara imekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie aje aone hilo eneo, aone ni namna gani Wizara inaweza kusaidia watoto wale ili waweze kuendelea na masomo badala ya kuendelea kuwa wafugaji maisha yao yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Shule za Tabora Mjini zina zaidi ya watoto 2,000 katika shule moja. Tunaposema elimu bora ndugu zangu, ni pamoja na kuangalia idadi ya watoto katika shule husika. Wakati sisi tukiwa tunasoma; mimi nimesoma Shule ya Msingi Isike, darasa langu lilikuwa na wanafunzi 48 peke yake mpaka namaliza darasa la saba, lakini leo darasa moja lina watoto zaidi ya 100 na kitu. Hii idadi ya watoto 2,000 kwenye hizi Shule za Msingi, ni kipindi ambacho tuko kwenye kampeni, ndiyo idadi hiyo ilikuwepo. Sijui sasa hivi watoto waliosajiliwa kuingia Darasa la Kwanza hali iko namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, miundombinu ya madarasa haipo, siyo rafiki kabisa, watoto wanabanana, watoto wanasoma asubuhi na jioni na elimu ya mchana siyo elimu nzuri hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya kwenye suala la elimu, namwomba sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu atusaidie katika Mkoa wetu wa Tabora katika zile shule 300, naomba sana, chonde chonde, Mheshimwa Waziri atuangalie kwa jicho la tatu Mkoa wa Tabora hasa Halmashauri ya Tabora Mjini ili tuweze na sisi kupata hizo shule ziweze kusaidia wananchi wetu kupata elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Sekta ya Afya.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)