Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi nikushukuru sana kwa hii nafasi. Vile vile nichukue nafasi hii kipekee kumshukuru sana Waziri wa TAMISEMI, dada yetu Mheshimiwa Ummy pamoja na timu yake kwa kazi nzuri ambayo anaifanya.

Mheshimwa Naibu Spika, tunamfahamu vizuri sana dada yetu Mheshimiwa Ummy, hatuna wasiwasi kabisa na utendaji wake. Pia tunawafahamu Manaibu wake vizuri sana, hatuna wasiwasi kabisa na utendaji wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nina mambo matatu ambayo nahitaji kuishauri Serikali. Jambo la kwanza nitashauri kwa upande wa afya ya msingi, jambo la pili nitashauri upande wa barabara na madaraja na jambo la tatu nitashauri kuhusu suala la ugatuzi wa madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Jimbo langu la Manyoni Mashariki lina zaidi ya vijiji 60. Katika vijiji vile 60 nina vijiji 29 ambavyo vina Zahanati. Vile vile nina Kata 19 na katika Kata hizo, nina Kata mbili ambazo zimejengewa Vituo vya Afya. Kwanza nachukua nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kutujengea Vituo vya Afya viwilli; Kituo cha Afya cha Kintinku ambacho tayari kimeanza kutumika na Kituo cha Afya cha Nkonko ambacho tayari kilishakamilika, lakini bado kuna changamoto za hapa na pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kumshukuru sana Waziri, lakini naomba nimkumbushe mambo mawili. Jambo la kwanza, kwenye Vituo vya Afya viwili ambavyo vimejengwa hususan Kituo cha Afya Nkonko tayari kimekamilika, lakini bado hatuna wataalam. Tulipeleka mtaalam mmoja ambaye ni Daktari (Medical Doctor), hakuweza kuripoti. Kile Kituo cha Afya ni kikubwa sana, kinahudumia zaidi ya Kata sita. Naishukuru tena Serikali kwa kutupa hiyo nafasi, lakini bado kile Kituo cha Afya hakitumiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba niishauri Serikali, kwa sababu tuna tatizo la hao wataalam kwenda kwenye Vituo vyetu vya Afya, nadhani tunahitaji kuja na mbinu mbadala. Naishauri Serikali husasan Wizara ya TAMISEMI tuangalie jinsi gani tunaweza tukafanya mapping ya wale vijana waliomaliza Shahada za Udaktari kwenye kanda husika, kwa mfano, Kanda ya Kati ili tunapowapangia vile vituo, tupange kulingana na kikanda. Hii itapunguza kasi ya vijana kutowasili au kutoripoti kwenye vituo vyao. Naomba nilishauri hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nawaza kuhusu balance kwamba, kati ya kujenga Kituo cha Afya na Zahanati kipi kianze? Natambua kwamba Sera yetu ya Afya inatambua kila Kata lazima iwe na Kituo cha Afya, kila Kijiji lazima kiwe na Zahanati, lakini katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi vile vile imebaini kwamba kila Kata inatakiwa iwe na Kituo cha Afya, lakini kila Kijiji kiwe na Zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu nini? Ni wakati gani sasa tunahitaji kuanza kujenga Kituo cha Afya na ni wakati ambapo tunahitaji kuanza kujenga Zahanati? Hoja yangu inajikita kwenye eneo langu la Jimbo la Manyoni Mashariki ambapo nina vijiji zaidi ya 60 lakini nina Zahanati 29 tu; nina Kata zaidi ya 19 na Vituo Afya viwili. Nadhani Mheshimiwa Waziri unahitaji kuangalia zaidi jinsi ya ku- balance unapofanya maamuzi aidha uanze ku-exhaust Zahanati kwenye Kata then twende kwenye kujenga Kituo cha Afya, badala ya kujenga Kituo cha Afya kwenye Kata ambayo haina Zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nalisema hili? Kuna vijijij vipo mbali sana na kupata huduma za afya. Ningetamani kuona kila Kijiji kinapata Zahanati, then ile Kata ambayo tayari ina Zahanati i-qualify kupata Kituo cha Afya. Lengo letu ni kupunguza umbali wa watu kupata huduma za afya, lakini vilevile ku-promote suala health seeking behavior ili watu wasikimbilie kwenye dawa za kienyeji.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala la barabara. Naishukuru Serikali kwanza kwa Kuanzisha TARURA, nilishasema huko nyuma; na kwa Jimbo la Manyoni Mashariki tuna mtandao wa barabara zaidi ya kilomita 1,000 na bajeti yetu kwa mwaka tunapata takribani milioni 600. Mwaka huu tumekumbwa na matatizo makubwa sana ya kuharibika kwa barabara, barabara ya Kintinku Makanda takribani kilomita 30 imejifunga kuanzia Januari mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Makanda kuna mnada mkubwa sana ambao unachangia pato la Wilaya yetu ya Manyoni, lakini tuna barabara ya kutoka Iseke - Mpapa - Simbanguru – Mangori, ilijifunga kwa muda mrefu sana. Vile vile tuna barabara ya kutoka Chikuyu - Chibumagwa - Mahaka kwenda Sanza, nayo ilijifunga kwa muda mrefu sana. Tunahitaji kufanya nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ni muda muafaka, watu wengi wamesema tunahitaji kuipa nguvu TARURA, naunga mkono hilo. Kwa upande wa Manyoni Mjini ningemshauri Mheshimiwa Waziri hasa kwa mijini, wilaya ambazo tunazo, Makao Makuu ya Wilaya, sidhani kama bado TARURA wanahitaji kuendelea kukarabati kwa kiwango cha vumbi.

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani kuona katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri wanatenga angalau kilomita moja kwa ajili ya kujenga barabara za mijini, Makao Makuu ya Wilaya kwa kiwango cha lami, kuliko kuja na barabara za vumbi kwenye Makao Makuu ya Wilaya. Hizi barabara za changarawe na vumbi tuzipeleke vijijini, Natamani kuona tunaboresha Makao Mkuu yetu ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sanjari na hilo, vile vile natamani kuona mnapokuja na mpango wa kujenga barabara za lami kwenye maeneo ya Makao Makuu ya Wilaya tuangalie jinsi gani tutaweka taa za barabarani kwa ajili ya kuboresha miji yetu na vilevile kuwafanya wafanyabishara weweze kufanya kazi kwa muda mrefu na pia itaboresha usalama wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni suala la ugatuzi wa madaraka. Mimi ni muumini wa ugatuzi wa madaraka, nimehusika sana katika mchakato wa kuandaa Sera ya Ugatuzi Madaraka. Wote mnatambua kwamba suala la ugatuzi wa madaraka lilianza miaka ya 1998 ambapo tulianza na D by D Policy Paper, ambayo imekaa kwa zaidi ya miaka 20, lakini hatujawahi kuwa na Sera ya Ugatuzi wa Madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, D by D Policy Paper ndio ilitumika kama sera ambayo tumeitumia sana kuja na program ya kwanza ya maboresho ya Serikali za Mitaa na program ya pili ya maboresho ya Serikali za Mitaa ambayo iliisha 2014. Kuanzia mwaka 2019, natambua TAMISEMI walianza mchakato wa kutengeneza Sera ya Taifa ya Ugatuzi wa Madaraka. Hoja yangu ni nini? Napenda kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, mchakato wa ile sera ya ugatuzi wa madaraka imefikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, namshukuru Mheshimiwa Waziri, katika bajeti yake ameweza kutenga fedha kwa ajili ya program ya kuimarisha Serikali za Mitaa na Mikoa, yaani Regional and Local Government Strengthening Program. Napenda kujua kwamba ni kwa jinsi gani sasa Wizara inakuja kuwahusisha wadau wa maendeleo?

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba katika kuandaa hii program na hata hii Sera ya Ugatuzi wa Madaraka, wadau mbalimbali walihusika sana wakiwepo USAID, UNICEF, EU, DFID, JICA na wengine: Je, Mheshimiwa Waziri amejipangaje kuhakikisha anawahusisha hao wadau ili kiasi cha one point five billion ambacho tumekipanga kwenye bajeti yetu tuweze kupata nguvu vilevile ya wadau ambao walihusika sana katika kuhakikisha kwamba suala la ugatuzi wa madaraka linaenda kupata kipaumbele?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake na ninaomba niseme kwamba naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)