Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia hii nafasi ili niweze kuchangia katika wizara hii. Jambo la kwanza, kwanza nawapongeza sana, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Manaibu Mawaziri lakini pia Katibu Mkuu na Manaibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi wote kwa namna ambavyo wamekuwa wanaisimamia hii wizara na wanatekeleza majukumu yao. Hii ni moja ya wizara kubwa ambayo inagusa Maisha ya watanzania kila mahali. Kwa hiyo ni wizara ngumu lakini naamini mungu atakuwa pamoja na nyinyi ili muweze kufanikiwa na kufikia matarajio ya watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naomba nishauri kwasababu ya ukubwa wa hii wizara na kwa umuhimu wa Wizara ya TAMISEMI ni muhimu tufike mahali tuingie kwenye mikataba ya utendaji. Mikataba ya utendaji itatusaidia kwamba kila halmashauri sasa, halmashauri iangalie mapato ndani, iweke kipaumbele angalau kimoja au viwili kama ni kujenga kituo cha afya mwaka huu wanajenga kituo cha afya, kama ni kujenga ni shule wanajenga shule. Katika halmashauri zote hizo baada ya miaka mitano tutakuwa tumefika mbali sana. Kwa hiyo, nafikiri hili ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, TARURA, TARURA ni muhimu sana, TARURA ndiyo imebeba barabara mbalimbali zilizopo mijini na vijijini. Kwenye Jimbo langu la Vwawa wananchi wa Jimbo la Vwawa ni wakulima, wakulima wa kahawa, wakulima wa mahindi wa mazao ya chakula na biashara na wanazalisha kweli kweli na ndio maana Mkoa wa Songwe Kitaifa unashika nafasi ya tatu kwenye uzalishaji wa chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili waweze kuendelea kuzalisha na huduma mbalimbali ziweze kuwafikia wakulima tunahitaji barabara zao ziimarishwe, zifike mpaka vijijini kule ili wale wananchi sasa waweze kupata pembejeo kwa wakati waweze kusafirisha mazao yao kwa muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika kufanya hilo barabara kama ile barabara ya kutoka Iyula kwenda Idunda kwa muda mrefu imekuwa haipitiki. Wananchi wale wa Idunda kwasababu ya mvua nyingi daraja lilikatika barabara haipitiki wanakosa huduma mbalimbali naomba barabara hii iyangaliwe. Kuna barabara ya kutoka Ichenjezya kwenda Mbozi Mission. Kuna barabara ya kutoka Ichenjezya kwenda Msia hizi barabara ni muhimu sana kwasababu zinaenda katika maeneo ya uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna barabara ya kutoka Chimbuya, Ukwile kwenda Chizumbi pale kuna daraja kubwa lilikatika wananchi wale wanakuwa hawana mawasiliano kipindi cha mvua ni muhimu TARURA wakaongezewa fedha ili waweze kujenga haya madaraja, wajenge barabara hizi zipitike kwa wakati wote na tunaamini uzalishaji utakwenda vizuri sana katika hali kama hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara nyingine ambayo inatoka njiapanda ya Iyula inaenda mpaka Iyula, ile barabara ni muhimu sana, sasa hivi imeharibika kabisa, utakuta kwamba wanashindwa kupeleka mbolea, wanashindwa kusafirisha kahawa, wanashindwa kupata huduma mbalimbali naomba hili nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara nyingine ya kutoka Ihanda inaenda mpaka Ipunga pamoja na kwamba imekarabatiwa bado kuna mambo hayajakaa vizuri katika eneo hilo. Kwa hiyo, ushauri wangu ni vizuri TARURA ikaongezewa mgao wa fedha, sasa hivi wanapata asilimia sijui 30, sijui 32 tukifika asilimia 40, TANROADS wakachukua asilimia 60 wale wakachukua 40 basi itasaidia sana katika kuweza kusimamia barabara mbalimbali zinazoenda katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu afya, nashukuru sana, naishukuru sana Serikali ilitupatia Mkoa wa Songwe kujenga Hospitali kubwa ya Rufaa ambayo inajengwa pale mpaka sasa hivi bado haijaanza. Naamini Serikali itachukua hatua kuhakikisha ile hospitali kubwa inaanza kufanya kazi. Lakini ile hospitali ni ya rufaa, tunahitaji tuwe na vituo vya afya, vituo vya afya katika Jimbo la Vwawa ambalo lina kata 18 tunavituo vya afya viwili tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba Mheshimiwa Waziri ikikupendeza basi Kata kama ya Ihanda ambayo inawakazi wengi sana tupatiwe kituo cha afya. Katika lile eneo ili kiweze kuhudumia wananchi wa Ihanda lakini pia na wasafiri wengi ambao wanaenda mpaka Tunduma wanapovuka mipaka kukiwa na ajali watakuwa na uwezo wa kupata huduma katika lile eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Msia tunahitaji kituo cha afya lakini pale Hezya tunahitaji Kituo cha Afya, na Luanda tunahitaji Kituo cha Afya. Katika kipindi hiki tukiweza kupata Vituo vya Afya kama vinne au vitano vitatusaidia sana katika kuimarisha huduma za afya katika maeneo yale na mkipeleka na watumishi na madawa nina imani wananchi wa Jimbo la Vwawa wataendelea na uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichangie kwenye upande wa elimu. Jimbo la Vwawa linashule za Sekondari zaidi ya 35. Tuna shule za msingi zaidi ya 90 katika Jimbo la Vwawa. Lakini shule za kidato cha tano ni chache, tuliomba katika kipindi kilichopita tukataka baadhi ya shule zipandishwe hadhi ili ziwe za kidato cha tano na ziweze kuchukua wanafunzi. Na katika hilo Serikali ilitoa fedha kidogo za kusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukapata Shule ya Msia, Shule ya Msia Sekondari ikapatiwa fedha kidogo kujenga madarasa. Shule ya Simbega Sekondari ikapatiwa fedha, lakini Mlangali ikapatiwa fedha yale majengo wananchi nao wakachangia matofali, wakachangia ujenzi wamejenga madarasa yamekamilika mpaka leo bado, bado zile shule hazijaanza kupokea wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Watoto wetu wanahitaji kwenda kidato cha tano sasa ni vizuri basi hizi shule zikasajiriwa na zikapokea wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu watakaotoka maeneo mbalimbali tutakuwa tumechangia sana katika kuendeleza elimu ya Watoto wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia kuna watumishi wengi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ambao hawako katika mfumo wa malipo ya Serikali, wapo kwenye mikataba inakuwa ni mzigo mkubwa sana kwenye halmashauri na hii inatokana kwamba tulipoondoa wale madereva ambao hawana vyeti na watu wengine Halmashauri imebaki haina baadhi ya watumishi ikalazimika kwenye ajira za ndani. Hebu Mheshimiwa Waziri lifanyieni hili kazi ili nalo liweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambao ningependa nichangie ni kuhusu Mkoa wa Songwe, Mkoa wa Songwe ni Mkoa wa mwisho kuanzishwa hapa Tanzania ni mkoa mchanga pamoja na uwezo mkubwa sana wa kiuchumi. Lakini mkoa huu bado unahudumiwa na Mamlaka ya Mji Mdogo hatuna Halmashauri ya Mji, hatuna Manispaa limekuwa ni ombi la muda mrefu, tumeomba angalau tupate Manispaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Manispaa vigezo vitakuwa havijafikia basi tuangalieni kwenye Halmashauri ya Mji ili Mkoa kama Mkoa uwe na halmashauri ya kuweza kuwahudumia lakini kwa hali ilivyo sasa hivi hali si nzuri.
Mheshimiwa Waziri naomba hili mlipe uzito ili angalau Mkoa wa Songwe tupate Halmashauri ya Mji ama Manispaa ya Mkoa wa Songwe itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tumeomba, tulimuomba Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alipokuja tulimuomba eneo la kujenga soko, soko la mkakati, soko litakaoongeza mapato kwenye halmashauri. Akatukubalia lile eneo la kujenga soko likaanzishwa pale, ikatengwa eka hamsini pamoja na kujenga stendi ya Mkoa wa Songwe. Tunaomba haya yote yakapewe uzito unaostahili, mkayaweke katika mtazamo ili kusudi wananchi wale wa Jimbo la Vwawa wakaweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jambo la mwisho ambalo ningependa kuchangia katika siku ya leo ni kuhusu Wenyeviti wa Vitongoji na Mitaa. Hawa watu wanafanya kazi kubwa wanakutana na wananchi wanatatua kero nyingi wanashiriki kwenye maendeleo lakini hawana posho. Hebu wafikirieni hawa watendaji hawa itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tuangalie Madiwani umefika wakati sasa Madiwani wawe na mshahara wa kudumu kuliko kutegemea kaposho. Wawe na wenyewe na mshahara hiyo itatusaidia sana kwasababu sisi Wabunge ili tuweze kufanya kazi tunawategemea sana Waheshimiwa Madiwani ili tuweze kushirikiana na kuchochea maendeleo kila mahali. Kwa hiyo nakuomba Mheshimiwa Waziri liangalieni hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine mengi naamini Wizara ya TAMISEMI mtatekeleza majukumu yenu vizuri mtashirikiana, Wakurugenzi watatekekeleza majukumu yao nchi hii itaweza kusogea mbele na tutaweza kufikia maendeleo yale ambayo tunayatarajia.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kusema kwamba, naomba kuunga mkono hoja. Nawashukuru sana kwa nafasi, ahsante sana. (Makofi)