Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwanza nianze kuwapongeza Wizara hii ya TAMISEMI, nimpongeze Mheshimiwa Ummy kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dkt. Festo hongereni sana. Najua nyinyi ni wachapakazi na kwasababu tumeshafanyakazi kwa awamu, yaani miaka mitano iliyopita najua uchapakazi wenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si vibaya nikushukuru sana Mheshimiwa Ummy ulipokuwa Waziri wa Afya kwa kweli ulifanya kazi vizuri na najua utendaji wako wa kazi. Niishukuru pia Serikali kwa kunijengea Hospitali ya Halmashauri ambayo kimsingi haikuanza kazi ila kwa kweli imemalizika lakini yapo mambo machache ambayo tungependa yakamilike. Ziko fedha ambazo kimsingi zilishafika kwenye account za halmashauri lakini bahati mbaya sana fedha zile zimeondoka kutokana na kwamba muda wa bajeti ulishafika kwa hiyo, wakati wa mwaka mwingine fedha zikachukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe zile fedha zikirudi basi hospitali hiyo itakamilika na hatimaye kuanza kazi kwasababu ni hospitali hiyo tunaitegemea tu ya Halmashauri ya Mbulu. Na kwa hiyo, nishukuru sana lakini kingine nikushukuru pia kwa kituo cha afya cha Dongobeshi ni hicho kituo kimoja tu. Lakini ombi langu unajua unaposhukuriwa Mheshimiwa Waziri tuna principal za kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wakristo kuna sala ya Baba Yetu tunasema Baba uliye Mbinguni unamshukuru Mungu, unasema jina lako litukuzwe unamshukuru Mungu, unasema mapenzi yako yatimizwe unamshukuru Mungu lakini baadaye huyu Mungu unamuwekea ombi unasema utupe riziki za kila siku sasa Mungu anapenda sifa na anamjalia mja wake anapomuomba. Sasa nimekusifia na nyinyi mawaziri ili haya maombi yapitie hii sala na mtume basi huko vijijini ili mambo yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu ni kujengewa vituo vya afya, Mbulu vijijini kama Jimbo tuna kituo kimoja tu acha afya kama Mke wa Mkristo kwa hiyo maana yake ni huyo tu, Wadongobesh ndiyo kituo kimoja. Na sisi kama Halmashauri ya Jimbo la Mbulu Vijijini wananchi wamejenga Vituo vya Afya vipo hatua mbalimbali; kuna Kituo cha Afya cha Getere ambao wameshazeeka kwa hiyo, tukipata fedha kidogo tunamalizia. Kuna kituo cha afya cha Maretadu na tuna zahanati nyingi tumeshajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ujue kwamba tukishajenga vituo hivi mkishatupatia zile fedha na sisi watumiaji wazuri wa fedha mkishatupa katika halmashauri yetu. Kuna Zahanati ya Galabadi, Zahanati ya Halsha, kuna Zahanati ya Hanaj na maboma mengine ambayo yapo kimsingi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri pia nishukuru umetupa fedha katika zahanati tatu nimeziona juzi. Lakini mkituongezea basi ni wazi kwamba kwa jimbo la Mbulu vijijini tunaweza kuihudumia wananchi wetu kwa afya zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Wizara hii ya TAMISEMI saa hizi majimbo yetu ya vijijini yameanza kuwa na kata zake ni kubwa, kwa miaka zaidi mitano tunaenda mwaka wa sita hapajatokea kabisa ugawaji wa Vijiji na Vitongoji na Tarafa. Sasa niombe muangalie kwenye bajeti yenu ijayo muweze kutenga fedha za kugawa Vijiji na Vitongoji na Kata kwasababu zimekuwa kubwa sana hazitawaliki. Na sisi tuna Tarafa ambayo tunaiomba sana mara nyingi tunaleta maombi kwenye tuna Tarafa tunaiita ya Hedayachini kule kuna Wahadzabe eneo lao ni kubwa sana ina kilometa 245. Kwa hiyo, ni Tarafa ambayo kwa kweli ukiangalia tunahitaji jambo dogo tu kuwapatia ule uwezo wa kugawanya Tarafa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na TARURA, umezungumza katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri umeonyesha kwamba kuna jambo la ugatuaji wa madaraja D by D nitaizingatia sana. Lakini ni ngumu kwasababu moja kwenye Jimbo la Mbulu vijijini kwa sababu tu ya miundombinu ya barabara ambayo kimsingi haiwezi kwasababu kwanza TARURA pesa zake zinazopatikana ni kidogo sana, sisi kwa mara ya mwisho tumepewa milioni 671 na tuna barabara zetu zenye urefu wa kilometa 1,093.7. Kwa fedha hizi kwa kweli hatuwezi kujenga hizi barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna maeneo korofi ambayo kimsingi imekuwa na shida tunatakiwa tujenge madaraja kumi yenye jumla ya shilingi bilioni 11 hasa umepewa Milioni 66. Nimpongeze sana Meneja wangu wa TARURA wa Wilaya anajitahidi sana kufanya kazi na nishukuru umempa gari lakini shida iliyopo pale ni kwamba hakuna namna yoyote ya kujenga hizo barabara. Lakini nishukuru sasa pamoja na hayo yote nimeona kuna kama kamilioni kadhaa kameongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hasa niombe tumeweka madaraja yetu mfikirie namna ya kuyajenga kwasababu kuna shule kama saba sasa haziendeki kutokana na miundombinu. Kuna daraja la Masyeda, kuna daraja la Getere na Miodad hayawezi kabisa kupitisha wanafunzi na kwasababu mvua ikinyesha tu hizo shule tena hazifikiki kwasababu umbali ule na makorongo yamejaa. Kwa hiyo, naomba TAMISEMI wafikirie na hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi tumeleta maombi ya kupandisha mji wetu wa Haydom kuita Manispaa aah na ni hii mji wa Haydom. Tumeleta maombi yetu na Mji wa Dongobesh tumeleta maombi tufikirie na hilo lakini mwisho kabisa najua dakika zimekwisha tuna ahadi za kilometa 5 ya mji wa Haydom, tuliahidiwa na viongozi wetu naomba tumejenga kilometa 1.8 naomba sasa tuweke fedha ili walau zile kilometa za ahadi za Mheshimiwa Rais ziweze kutimilizika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa nishukuru pia kwa utendaji wenu wa kazi lakini niwakumbushe pia pamoja na wewe Mheshimiwa Ummy unakumbuka umefika Haydom na umefika Dongobesh zile ahadi zetu tulizoziweka pale ukanisaidie sana kuzitimiza na kwasababu umeingia TAMISEMI Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)