Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mungu ambaye ametupa afya na uzima. Pia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Hai, naomba niishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo wanatujali, sasa hivi tunaona raha ya kuchagua Chama cha Mapinduzi. Raha hiyo tunaiona kwa sababu tayari tumekwisha kutengewa fedha kwa ajili ya mradi wa maji pale Kikafu, naishukuru sana Serikali.

Pia tumefanyiwa ukarabati wa shule zetu mbili; Lyamungo na Machame Girls. Vilevile tumeonja angalau lami japo kwa mita chache lakini ndiyo zimeingia kwa sababu tulichagua Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa sana hili ambalo tumelipata tumetengewa shilingi bilioni 1.6 kwa sababu ya kufufua Kiwanda cha Machine Tools. Hii ndiyo raha ya kuchagua Chama cha Mapinduzi, nawashukuru sana. Si hivyo tu, kwenye Wizara hii ambayo naenda kuchangia muda si mrefu tumepelekewa shilingi milioni 280 kwa ajili ya ukarabati wa Shule za Narumu, mabaara lakini na ujenzi wa nyumba za walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye kuchangia hoja iliyopo mezani. Nianze kwa kuunga mkono hoja kwa sababu nina imani kabisa na Mheshimiwa Waziri dada yangu Ummy pamoja na wasaidizi wake wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi si mahiri sana wa kusifia lakini ninazo sababu za kumsifia Mheshimiwa Waziri huyu kwa kazi nzuri anayoifanya. Majuzi wakati wa Pasaka nilitembelea Kituo cha Afya pale Kisiki, aliona kwenye taarifa ya habari yeye mwenyewe akanitafuta na akaniambia kituo hiki tunaenda kukitengeneza kiwe cha kisasa ndiyo maana namsifia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa Naibu Waziri Silinde majuzi tukiwa humu Bungeni alitoka akaenda kufanya ziara kule Hai. Ndiyo maana nasema hakika tuna timu nzuri ambayo inatusaidia hapo TAMISEMI. Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Festo naye leo asubuhi ameniambia tukimaliza Bunge hili tunaenda naye Hai. Kwa hiyo, ninayo sababu ya kupongeza timu hii nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu, pamoja na mazuri hayo machache ambayo tumefanyiwa kwa kipindi cha miaka 15 tuliyakosa sasa tumeyaanza kuyapata, naomba niseme kwenye elimu bado tunashida. Shule zetu za msingi pale Jimbo la Hai zimejengwa kuanzia mwaka 1950 na kurudi nyuma na sasa hivi zimechakaa sana, tuna shule 106 ni chakavu mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pasaka nilitembelea Shule ya Mafeto ukienda pale Mheshimiwa Waziri ni aibu na wewe nilikutumia clip ile uone shule ile imechakaa kabisa si rafiki. Shule zote hizi 106 zimechakaa kweli kweli. Niombe Serikali ielekeze nguvu hapo ili pamoja na nguvu za wananchi na mimi mwenyewe tunazozitumia kwa ajili ya kuboresha miundombinu hii lakini Serikali itusaidie kupeleka fedha pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni pamoja na shule za sekondari. Tunayo Shule yetu ya Lemila pale na yenyewe imechakaa. Shule hii kimkakati kwa sababu inazungukwa na Kata nne tunaomba sana Serikali itutazame tuwe na shule ya kidato cha tano na kidato cha sita kwa sababu shule ile mazingira ni rafiki lakini tunalo eneo la kutosha; tuna hekta ishirini kwa ajili ya ujenzi wa kidato cha sita pale. Naomba pia nikumbushe pamoja na shule hizo nilizozitaja tuna Shule ya Uduru imechakaa san ana Shule ya Mkwasangile imechakaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna eneo lingine ambalo niombe Serikali ilitazame sana. Pale Jimbo la Hai tulikuwa na shule tano, hizi shule tano zinaitwa shule za msingi za ufundi. Shule hizi zilikuwa zimejengwa mahsusi kwa ajili ya kuandaa vijana wetu kupata ufundi wa aina mbalimbali. Shule ya pale Mshara inaitwa Shule ya Msingi ya Ufundi Mshara, mle ndani kuna vifaa kwa ajili ya kufundisha watoto wetu kushona cherehani, kufuma lakini pia mafundi seremala. Ile shule imesimama, vifaa vipo mle ndani, watoto walianza kusoma lakini tangu mwaka 2019 walisitishiwa kufanya mitihani, hili linahusisha Wizara ya Elimu lakini pia TAMISEMI. Shule ya Mshara, Mkwasangira, Sare, Mroma lakini pia tuna shule moja ilijengwa kwa kusudio hilo na mradi wa TASAF na yenyewe imelala naomba ziangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule hizi zitatusaidia kuwaibua vijana wetu kwenye eneo la ufundi lakini wakati huo huo Wizara ya Elimu ijiandae kufungua shule hizo ili watoto hawa waweze kufanya mitihani ya ufundi lakini pia waweze kupewa vyeti. Hii itaendana sambamba na fedha nyingi ambazo Serikali imepeleka kufufua Kiwanda cha Machine Tools, tutapata watoto wa kwenda kufanya kazi kwenye kiwanda hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nililotaka kuchangia, nafahamu tumetengewa fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya pale Lundugai. Niombe sana Wilaya ya Hai tunayo changamoto kubwa, tuna mahitaji ya vituo vya afya 12. Bahati nzuri tumeshatenga maeneo, haya maeneo naihakikishia Serikali yapo, hayana mgogoro na sisi tupo tayari kuchangia pale ambapo itakuwa tayari na wao kutuletea fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa niombe sana pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri ameshanikubalia hiki Kituo cha Kisiki hatuna gari la wagonjwa, watumishi hawatoshi lakini pia hatuna jengo la mama na mtoto. Hii ni sambamba na Hospitali yetu ya Wilaya na yenyewe gari la wagonjwa hakuna, hakuna Jengo la Maabara wala Jengo la Mama na Mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kidogo kuhusu TARURA, wenzangu wamesema sana lakini kwa Jimbo la Hai kwa kweli mtutazame kwa jicho la huruma. Pale tuna mtandao wa kilometa 600 na mita 200 lakini bajeti ambayo tumewekewa makadirio ni shilingi bilioni 1.7 haiwezi kutusaidia. Wenzangu wameshashauri namna ya kufanya, niombe kwa mahsusi wake mtusaidie. Tuna barabara inayotesa wananchi kutoka pale Kwa Sadala - Uswaa, Kivuko cha Mkalama – Kikavu Chini lakini Boma Ng’ombe - TPC na barabara zingine ambazo nimekwisha kuzisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kwa haraka haraka, niombe sana Serikali tuna soko la kimkakati pale Kwa Sadala. Soko hili sipumui, simu yangu inajaa picha kwa sababu ya soko hili. Kila siku wananchi wanapiga picha wananiambia limechakaa halifai lakini tunalo eneo ambalo tumeshatenga kwa ajili ya soko hili. Ikumbukwe Wilaya hii kwa asilimia 78 tunategemea kilimo, wananchi wako tayari kulima soko lile liwe la kimataifa ili tuweze kukaribisha wawekezaji waje wanunue lakini pamoja na kuwa na viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejenga Kituo cha Afya Longoi na Naibu Waziri amekitembelea. Sasa tunaomba vifaa tiba na watumishi ili tuweze kufungua kituo kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumze jambo ambalo wenzangu wamesema pia. Haya yote tunayoyapanga na hizi bajeti tunazozipitisha wanaoenda kusimamia ni watumishi wa umma. Naomba sana Serikali ione haja ya kuongeza mishahara ya watumishi. Pia watumishi wale ambao wamepandishwa vyeo na wana barua zao mishahara yao irekebishwe. Changamoto kubwa tunayoiona hapa wakati mwingine tunalaumu sana Maafisa Utumishi lakini tujue sisi Wabunge hapa ndiyo tunaopitisha bajeti. Pale Wizarani naomba TAMISEMI mtashirikiana na Utumishi kuona namna ya kuongeza ma-approver wengi ili kazi inapofanyika huku kwenye level ya Halmashauri watumishi hawa mishahara yao iweze kuruhusiwa mapema na kuondoa kuwa na malimbikizo mengi ya mishahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisisitize barabara moja muhimu sana. Tuna barabara ya kutoka pale Mferejini – Narumu - Makoa ni kilometa 13 tu. Hii barabara inatupasua kichwa. Barabara hii iliitwa ya ng’ombe nimekuwa nikiisema sana na ni ahadi ya Rais, niombe sana mnifungue kwa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine kwa kuhitimisha, nimeona kwenye hotuba imeleeza kuwa na maeneo ya uwekezaji. Jimbo la Hai tunayo maeneo ya uwekezaji lakini changamoto yapo kwenye Vyama vya Ushirika 17. Jambo hili nimekuwa nikisema sana na hapa nasema mapema kabisa kwa Wizara ya Kilimo tutakapofika kwenye Wizara ya Kilimo ile shilingi nitaitazama mno namna ya kuifanya. Juzi hapa tumekuwa na Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, Waziri wa Utalii na Maliasili tumetembelea kule amejionea mwenyewe namna ambavyo kuna mikataba ya hovyo kwenye ushirika.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kuunga mkono hoja. (Makofi)