Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ameendelea kutujalia afya. Pia naomba niendelee kukushukuru wewe sana kwa sababu nimepata nafasi ya kuchangia jioni hii katika bajeti hii muhimu ya Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu hasa nitajielekeza katika eneo la TARURA pamoja na elimu na kidogo nitagusia upande wa afya. Kwanza, naungana mkono kabisa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba ipo haja ya kuitizama TARURA kwa macho mawili na hasa katika eneo zima hili la kuongeza hii percentage ya kiasi ambacho TARURA wamekuwa wakipewa fedha kwa ajili ya kushughulikia barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo kubwa lenye mtandao mkubwa unaohitaji kutengenezwa ama kulipa kipaumbele ni eneo la barabara zilizopo vijijini. Eneo la Kishapu tuna jumla ya kilometa 1,030 ambazo zinahitaji kutengenezwa lakini zikiwa katika mazingira magumu kweli kweli. Yapo maeneo mengine yapo katika mbuga hasa lakini vile ni vijiji na kuna maeneo ya kiutawala ya kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa vyovyote vile huduma ya barabara ni ya msingi sana kwa sababu bila huduma ya barabara huduma hizi zingine; kwa mfano huduma ya afya wananchi hawawezi wakayafikia maeneo kwa ajili ya kwenda kupata huduma iwe katika health centre au dispensaries lakini hata katika sekta ya elimu kuna wakati watoto wanashindwa kufika maeneo ya shule kutokana na matatizo ya maji na hasa panapokuwepo na matatizo ya vivuko kadhaa kuharibika Zaidi, kwa hiyo, lipo tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia usafirishaji wa mazao kila mmoja hapa anafahamu Mkoa wa Shinyanga ni Mkoa ambao unalima sana pamba. Tunapozungumza zao la pamba ni Wilaya ya Kishapu ndiyo inayoongoza kwa kulima pamba. Tafsiri yake Wilaya ya Kishapu ni moja kati ya wilaya na inawezekana ikawa ya kwanza ama ya pili nchini kwa uzalishaji wa pamba. Sifa ya zao la pamba katika kuchangia uchumi wa nchi hii unaweza ukawaona hawa wana Kishapu ndiyo wanaongoza kwa adha ya barabara, hapa hakuna haki kabisa. Nataka niishauri sana Serikali na hasa Wizara yetu ione umuhimu wa Wilaya ya Kishapu kuhakikisha kwamba barababara zinatengenezwa na inaongezewa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niyataje baadhi ya maeneo ambayo yana hali mbaya kabisa, zikianza tu kunyesha mvua safari za kuelekea Kata za Itilima, Kiloleli, Mwaweja na Mwamalasa inakuwa ni shida, hizi ni kata ambazo hazipitiki kabisa. Hili ni tatizo ambalo kwa kweli tusipoliangalia tunaweza tukawakatisha tamaa sana wananchi. Zipo Kata za Uchunga, Mwataga na Somagegi, hizi ni kata ambazo na zenyewe zinakuwa kisiwani pale mvua zinapoanza kunyesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja ya Serikali kulitazama eneo hili na kuona haja ya kupeleka fedha za kutosha. Wenzangu wameshauri sana katika masuala ya simu, hili jambo tunaweza tukaliangalia na Serikali ifike mahala iwe serious, tuwahurumie wananchi. Bunge limekuwa likitoa mawazo hata katika eneo la mafuta, kwa nini tusifike mahali tukajifunga mkanda lakini lengo tuwafungulie njia wananchi? Nasema hivi kwa sababu Watanzania kwa ujumla wanahangaika na masuala ya barabara. Kwa hiyo, mimi naamini kwa sababu Serikali ya CCM ni sikivu kupitia mMwaziri wetu na hususani Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na wasaidizi wake ndugu yangu Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dkt. Dugange mfanye hili jambo ili mradi tuwapunguzie adha wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata habari kwamba kuna kama shilingi bilioni 100 zimeongezeka kidogo na wengine wameshaanza kupata taarifa, zimeshaanza kutumwatumwa kule, mimi naomba Kishapu tuikumbuke. Tuikumbuke Kishapu kwa jicho la huruma kwa sababu wananchi hawa wanateseka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka nizungumzie ahadi za viongozi wetu wakuu. Kipindi cha Uchaguzi aliyekuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alifika Kishapu na bahati nzuri aliweza kuahidi kilometa nne. Ahadi hii alikuja kusisitiza kwa sababu alishaiahidi awamu ile ya kwanza, maana yake miaka mitano barabara hiyo ilikuwa haijatekelezwa lakini imeanza kutekelezwa kwa mwaka fedha uliopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi kilometa nne tumepata jumla ya shilingi milioni kama 114, shilingi milioni karibu 380 zilikuwa hazijafika. Naomba sana fedha hizi ziweze kufika na kusaidia wananchi hawa ili mradi Mji wa Kishapu na wenyewe uweze kufanana. Kwa sasa hivi kazi iliyopo kwenye ile kilometa moja kuna asilimia kama 94, lakini nachoomba Wizara iweke msukumo na kuhakikisha fedha zile zinafika Kishapu na kuhakikisha kwamba mradi huo tunaukamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu wa walimu 1,611 katika shule za msingi, hapa kuna tatizo kubwa sana. Kwenye nyumba za walimu na penyewe pana shida kubwa. Kuna tatizo kubwa sana upande wa madarasa, wananchi wamejitahidi sana kutoa nguvu zao kuhakikisha kwamba wanasukuma mbele na kutoa mchango upande wa madarasa. Hata hivyo, kuna haja Serikali kuweka mpango maalum kuhakikisha kwamba ina-support nguvu za wananchi, yako magofu mengi ambayo yanahitaji support na hii ni katika shule za msingi na sekondari. Naomba sana Wizara hii iweze kutazama maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna Kata mpya za Shagihilu, Mwaweja, Bupigi, Mwasubi, Mwadui, Luhumbo na Mwamala tumeshaanzisha sekondari mpya na bahati nzuri Serikali imekuja na mpango wa kuhakikisha inapeleka fedha kwa ajili ya sekondari hizi. Naomba sana Wilaya ya Kishapu ipewe kipaumbele na wananchi hawa tusiwakatishe tamaa tuhakikishe tunawapelekea fedha kwa ajili ya kuhakikisha maeneo haya yanafanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni upande wa Waheshimiwa Madiwani na nataka nizungumzie maslahi yao. Nimekuwa Diwani kwa zaidi ya miaka 20 na nimekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa zaidi miaka 10. Nataka nizungumze Madiwani wana shida kubwa sana na kusema ukweli hawa Madiwani ndiyo wanaosimamia shughuli za maendeleo, ndiyo wanahamasisha shughuli za maendeleo. Hawa Madiwani ndiyo wanaotoka jasho kwa ajili yetu sisi Wabunge ili mradi tupate ushindi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna kila sababu Mheshimiwa Ummy, Mheshimiwa Silinde, Mheshimiwa Dkt. Dugange oneni huruma kwa hawa viongozi wenzetu waongezeeni posho, laki tatu na siyo hela. Jamani tuangalieni majukumu waliyonayo na wananchi wanaowahudumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine hawa watu posho zao za vikao ni matatizo makubwa sana, ipo shida kubwa. Pengine na mimi nilikuwa naungana mkono tuhamishe posho hizi za madaraka ziwe zinalipwa na Serikali Kuu tubaki na hizi posho za vikao kwa sababu mzigo kwa baadhi ya Halmashauri unakuwa ni mkubwa na Halmashauri zinashindwa kulipa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)