Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii, nikiwa naenda kufunga dimba kabisa kwa siku ya leo, nikushukuru sana. Nami niungane na wenzangu wote kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri na timu yake nzima ya TAMISEMI, Katibu Mkuu na wasaidizi wake kwa kuendelea kuaminiwa na Serikali ili waweze kuitumikia na kututendea kazi ambayo Serikali inakusudia kuifanya kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapindunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianzie pale ambapo Mheshimiwa Mavunde ameishia. Ukweli ni kwamba majiji yetu na Manispaa, Miji pamoja na Halmashauri ambazo zinakua, zimenufaika sana na mradi wa TSCP na sina shaka, kwa rekodi peke yake kutoka mwaka 2010 mpaka mwaka 2020 kwa hii miaka 10 peke yake majiji yapatayo sita, Manispaa karibia nane pamoja na miji zaidi ya 16 imefaidika sana kwa miradi ya TSCP.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda hata Babati, Manispaa ya Ilemela, Mwanza, Tanga, Mbeya kule kwako zaidi ya kilometa 438 zimejengwa. Sasa naiomba sana Serikali, Mheshimiwa Waziri atakapokuja, kama Mheshimiwa Anthony Mavunde alivyosema, tuone namna gani mradi wa TACTIC ambao tayari wataalam kutoka World Bank na wataalam wa ndani, wameshatembelea Halmashauri zetu na kujiridhisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasemekana yapo mambo machache tu yamekwama huko kwenye Wizara, hebu tuyatazame tuone namna ya kuruhusu mradi huu uanze mara moja tuweze kuona tija ambayo tumeipata kutoka miradi ya TSCP na hatimaye tuone mafanikio na turahisishe, tupunguze mzigo kwa TARURA ambapo wote humu ndani tunalalamika kwamba fedha hazitoshi. Mradi huu tuna uhakika utahudumia zaidi ya Halmashauri 45 ukilinganisha na Halmashauri 18 na 9, jumla 27 peke yake kwa kipindi kilichokwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema nianze na hilo kwa sababu ni jambo muhimu. Naamini ukienda kule Mbeya, Tanga, Mwanza na hapa Dodoma na maeneo mengine ya Arusha, bado zipo barabara ambazo zinaunganisha miji hii na zitaleta tija sana katika mchango wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jiji la Mwanza peke yake tunategemea kuwa na barabara zisizopungua Kilometa 27 hadi 33. Barabara ya kutoka Buhongwa kwenda Igoma, barabara ya kutoka Sauti kwenda Luchelele, barabara ya kutoka Buhongwa kwenda Bulale inayokwenda kuungana na daraja la Masongwe kwenye Halmashauri nyingine ya Misungwi. Haya yote ni mafanikio ambayo yanaweza kuchagizwa sana na barabara hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni juu ya masuala mazima ya ardhi na upimaji. Utakubaliana nami kwamba jukumu la upimaji na Sheria ya Ardhi Na. 8 imezipa mamlaka zetu haki ya kupima, kumilikisha pamoja na kupanga. Sasa nimejaribu kuangalia kwenye kitabu, sioni maeneo ambayo Wizara imekumbuka kupeleka fedha kwenye Halmashauri zetu ili jukumu la kupima, kupanga na kumilikisha liweze kufanyika huko kwenye Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miji yetu bado ina changamoto kubwa. Kama Wizara inafanya jukumu lake la kupeleka watumishi na kuwalipa mishahara kupitia Wizara ya Ardhi, lakini jukumu la kwetu kama Wizara ya TAMISEMI ni kuhakikisha Halmashauri inaendelea kupima, kupanga na kumilikishwa ili tutoke hapa kwenye maeneo ambapo tupo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la muhimu kwenye Sekta ya Afya, upo mpango ambao ulipokelewa hapa na Wakurugenzi pamoja na watendaji kwenye Halmashauri. Maelekezo ya namna gani kila Halmashauri kulingana na mapato yake, kwa mfano, Jiji la Mwanza peke yake tumepangiwa kujenga vituo vya Afya vitatu, tujenge madarasa 100. Sasa nadhani hapa bado kuna changamoto tuiangalie vizuri. Mipango iliyopangwa kwenye Halmashauri na kuletwa bajeti kwetu, maana yake ni kwamba haitatekelezeka kama Halmashauri zitapokea maelekezo haya ambayo zinayo leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi leo hatuhitaji madarasa, maana yake tukisema madarasa, tunataka tukaongeze darasa kwenye kila shule. Sisi tunataka shule mpya. Tunazo shule 28; kila shule moja kati ya shule hizi, shule 27 kila shule ina watoto wasiopungua 2,400 sawa na shule nne. Kwa hiyo, tunadhani sisi leo tukiamua tunataka tujenge shule mpya zitakazowasaidia watoto hawa kukaa kwenye mazingira bora, salama na rafiki na yanayoweza kufundishika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naona umewasha kengele hapa, muda wenyewe umebana, lakini nakushukuru sana. Niseme tu kwamba tunahitaji mipango iliyopangwa na Halmashauri iweze kupokelewa na kuruhusiwa kufanya kazi ili iweze kuleta matunda na faida kwa wananchi kuliko maelekezo haya.
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, Mungu akubariki. Ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia. (Makofi)