Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na shule za ufundi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Shule ya Ufundi Moshi (Moshi Technical School), shule hii ya ufundi ilikuwa ikitoa elimu ya ufundi kwa wanafunzi kutoka mikoa mingi Tanzania na baada ya masomo ya elimu ya sekondari wanafunzi hawa walijiunga na Vyuo vya Arusha Technical na Dar Technical pamoja na Ifunda Tech. Kwa sasa shule hizi za ufundi zina hali mbaya sana hasa Shule ya Ufundi Moshi; majengo yamechakaa sana vifaa vya ufundi vingi vimekufa na hivyo umuhimu wa shule hii kama ya ufundi, inaendelea kushusha taaluma za ufundi katika nchi yetu na hasa kipindi hiki ambacho tunakwenda kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda ambao unategemea nguvukazi kubwa ya vijana waliopitia taaluma ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri anapohitimisha aniambie ametenga bajeti kiasi gani kwa ajili ya kuimarisha shule za ufundi Tanzania. Hii itasaidia sana vijana wetu ambao wamekuwa wakikosa ajira baada ya kumaliza shule na kujiunga kwenye vitendo visivyo na tija kwa Taifa ambapo wangekuwa na utaalam wa ufundi mbalimbali wangeweza kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakaguzi wa shule. Kumekuwa na changamoto kubwa kwa wakaguzi wa shule ambao wengine wamepewa magari ya kuzungukia na kukagua shule, lakini tatizo la magari hayo wakati mwingine yanakosa bajeti za mafuta ya kuwawezesha wakaguzi kufanya kazi zao kwa ufanisi. Naomba kujua kuwa Waziri amejipanga vipi kuhusiana na changamoto hii na atalitatuaje kupitia bajeti yake ya 2016/2017 ili kuhakikisha wakaguzi wanapata fursa ya kufikia kwenye shule zote nchini na kufanya ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa shule. Uboreshaji wa shule za msingi na sekondari uangaliwe kwa karibu ili kuongeza tija, shule zetu ni chakavu sana, huduma za madarasa, vyoo havifai kwenye shule zetu, hakuna viwanja vya michezo, madawati, nyumba za Walimu. Pamoja na changamoto zote hizo, tatizo la vitabu ni kubwa sana, naomba Waziri anapohitimisha atuambie amejipangaje kwa bajeti yake ili kuweka sera za kusaidia huduma shuleni kupunguza gharama kubwa kwa wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mishahara ya Walimu. Mishahara ya Walimu ni midogo sana ukilinganisha na kazi kubwa anayoifanya Mwalimu. Naomba Waziri aangalie ni namna gani anaweza kuangalia upya suala la mishahara ili kuwapa motisha Walimu wetu. Hali ya maisha imepanda sana, hivyo kupelekea Walimu kushindwa kujikita katika ufundishaji na kujiingiza katika biashara ndogondogo baada ya vipindi vya darasani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia suala la elimu kwa watumishi waliopo kazini. Kumekuwa na wafanyakazi ambao wamekuwa wakifanyia kazi idara mbalimbali kwa muda mrefu na baadaye kutaka kujiendeleza kutokana na uzoefu wao wa kazi wanazozifanya. Wanapotaka kujiendeleza wanaambiwa cheti cha form four, ambacho pengine wakati huo hakikuwa kizuri ila amekuwa mzoefu wa kazi hata kwa miaka zaidi ya 10. Naomba Waziri anapohitimisha atuambie ni namna gani anaweza kutengeneza mfumo wa elimu ya juu kwa watumishi wa umma wanaohitaji kujiendeleza.