Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Ummy na Manaibu wake, amepata watu wa kazi naye anafanya kazi nzuri. Nawapongeza Katibu Mkuu na timu yake, Bunge linawaamini watafanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna miradi ambayo imekuwa ikizungumzwa hapa na Waheshimiwa Wabunge juu ya miundombinu katika miji 45 na Makambako Mji umo. Wamekuwa wakijibu kwamba mikakati na michakato inaendelea. Tunaomba michakato inayoendelea waimalize haraka ili Makambako tuweze kupata soko kubwa na zuri; tupate barabara ambazo zitaletwa na huu mkopo ambapo fedha zitatolewa na Benki ya Dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wamezungumza hapa wenzangu juu ya afya. Mimi naunga mkono kwamba kwenye afya kuna changamoto, hasa upande wa bima. Watu wanashindwa kujiunga na bima za afya kwa sababu wakienda kwenye matibabu hawapati dawa. Kwa hiyo, tunaomba sana ili tupate watu wengi wa kujiunga na bima ya afya tupeleke dawa, hususan katika Jimbo langu la Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna zahanati tatu pale Makambako ambazo zilitengewa shilingi milioni 150, Mheshimiwa Ummy na wasaidizi wake wanajua. Tunaomba fedha hizi ziende ili wananchi wale kwa zahanati ambazo tumeshawaambia shughuli hizi ziweze kukamilika na kuwahudumia wananchi wa Makambako.
Mheshimiwa Spika, katika elimu bajeti hapa inaonesha mtaongeza sekondari za kata katika nchi hii. Niombe na mimi kwenye Jimbo la Makambako kata mbili hazina sekondari. Kata hizo ni Kitisii na Mwembetogwa, tunaomba tupate fedha ili tuweze kujenga sekondari katika kata hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzangu wamezungumzia sana suala la TARURA na mimi nawaunga mkono. Nina barabara pale ya kutoka Makambako – Mulowa – Kifumbe – Mutanga hadi Lupembe. Tunaona kwamba fedha ambazo TARURA wanatengewa ni kidogo sana.
Mheshimiwa Spika, amezungumza jana Mbunge mwenzangu mmoja hapa; ili kuongeza mfuko huu tufanye kama tulivyofanya kwenye Mfuko wa Maji na Mfuko wa TANROADS, tuongeze angalau shilingi 100 kwenye simu kama walivyochangia Waheshimiwa Wabunge jana. Pia tuongeze hata kwenye mafuta shilingi 50, itaongeza mfuko huu kuwa mkubwa ambapo barabara zetu zitatengenezwa vizuri. Mjini Makambako tuna barabara moja ya mjini pale inayopitia Golgota, ilitengenezwa lami kilometa moja, imebaki kilometa moja na kitu, niombe Mheshimiwa Ummy kupitia TARURA barabara hii iishe.
Mheshimiwa Spika, sasa nina suala maalum. Tangu kitokee kifo cha mpendwa wetu, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kweli mambo ambayo sasa yameanza kuwekwa kwenye mtandao yanahatarisha amani. Ni hatari kwa nchi yetu, ni hatari kwa Taifa letu na vyombo vya usalama vimebaki kimya.
Mheshimiwa Spika, mfano, ukifungua mule unakuta sasa wamemuweka Mheshimiwa Rais wetu Mstaafu Kikwete, Mheshimiwa Katibu Mkuu Mstaafu Kinana, Mheshimiwa Nape na wewe umo, sasa nani atafuata, hii ni hatari! Ni lazima tukemee jambo hili ambalo ni la kutugombanisha Watanzania kwamba watu hawa ni hatari ndiyo waliofanya vitu ambavyo wameandika mule. Hili ni hatari tukiliacha likaendelea, kesho hatujui atawekwa nani.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kikwete apumzike Msoga kule amefanya kazi yake vizuri na Mzee Kinana naye akapumzike. Huyu Mheshimiwa Nape wewe ni shahidi, 2013, 2014 mpaka 2015 wakati wa uchaguzi akiwa na Mzee Kinana walizunguka miaka mitatu kutafuta kura za CCM. Mheshimiwa Nape huyu alikatwa mpaka kiganja na Kinana alipata maumivu ya bega mpaka alikwenda kutibiwa, tuache! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wewe sasa wameanza kukuweka kwenye mtandao. Jamani Spika wetu anafanya kazi nzuri, tumuache Spika afanye kazi yake. Suala la Bagamoyo Spika alichosema kibaya ni nini? Amesema mikataba ile ijadiliwe, ninyi ndio mna uwezo wa kusema hiki hakifai, hiki kinafaa; Bunge hili. Tunaelewana ndugu zangu, Spika alichosema kibaya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo kwenye mitandao, aah Spika sijui nini…
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, ndugu zangu, niombe tumuache Spika na Naibu Spika waendeshe Bunge hili vizuri.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)