Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Solwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii. Kwanza naiunga mkono hoja.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri makini sana katika Wizara nyingi na ninaamini kabisa katika Wizara hii ya TAMISEMI, pamoja na wasaidizi wake tunakwenda kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nianze na TARURA moja kwa moja. TARURA ni mamlaka iliyotengenezwa kwa ajili ya kutengeza barabara vijijini. Inafanya vizuri. Katika Jimbo la Solwa kule kwangu wanafanya vizuri sana, lakini shida kubwa kabisa katika TARURA ni upungufu wa fedha watu wanazoziomba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nina kilometa 743, lakini fedha ambazo tunahitaji ni shilingi bilioni saba na fedha ambazo tumepata mwaka huu ni shilingi bilioni 1,100 na something. Utaona kwamba tatizo kubwa kwenye TARURA ni upatikanaji wa fedha tu. Sasa Wabunge wengi katika Bunge hili wamechangia sana na ukienda katika michango mikubwa, hasa katika Wizara hii ya TAMISEMI ni suala zima la TARURA.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai, tumekuwa na Mfuko wa Maji, tumekuwa na Mfuko wa REA wa usambazaji wa umeme vijijini, tumekuwa na Mfuko wa Road Fund; sasa mifuko hii inaonekana kama kwa namna fulani wanafanya vizuri. Kwa hiyo, tuendelee na mifuko hiyo hiyo. Sasa tuwe na Mfuko wa TARURA, tuwe na Mfuko wa Ukamilishaji Maboma ya Halmashauri zetu. Tufanye hivyo tu, na fedha zipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama alivyongea Mheshimiwa Zungu jana, nimemsikia hapa na Waheshimiwa Wabunge, fedha zipo kwenye mitandao, kwenye simu na kwenye mafuta na wananchi hawashindwi kulipa. Kwa maana ukichaji shilingi kumi kwa kila dakika, kwa kila mtu anayepiga simu au kwa kila lita shilingi 50, tutakuwa na mfuko wenye fedha wa kutosha kabisa kwenda kukamilisha miradi yetu katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye Hospitali ya Wilaya, nashukuru sana, nimepata shilingi milioni 800 kwenda kukamilisha majengo yaliyobaki. Naomba tu Wizara hii ifanye kila itakavyofanya; na kipaumbele cha Wizara hii kwa mwaka huu, nilifurahi sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu alivyosema wanakwenda kwenye tiba; vifaa tiba na afya yenyewe. Sasa kwenye hospitali yangu ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Jimbo la Solwa, tunahitaji vifaa tiba ili tuendelee na kazi kwenye Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukija kwenye maboma, nataka sasa niongee juu ya maboma haya. Katika Jimbo la Solwa tuna zahanati 42. Naishukuru sana Serikali imetupa shilingi milioni 150 kwa zahanati tatu ambapo sasa hivi tunakwenda kukamilisha zahanati hizo; Zahanati ya Kilimawe, Zahanati ya Mwamedilana, tunakwenda kukamilisha zahanati tatu. Vile vile katika ceiling tuliyoipata mwaka huu ni kwa ajili ya zahanati tisa tu. Maana yake katika 42 ukitoa tisa unabaki na 33. Tukienda kwa bajeti tatu bado tutakuwa na upungufu wa ukamilishaji wa zahanati kwa miaka mitatu mpaka 2024.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa Wizara ione namna ya ukamilishaji wa maboma haya, siyo tu Jimbo la Solwa, hata nchi nzima tuwe na mipango mikakati. Wizara ikinipa shilingi milioni 500 ya ukamilishaji wa majengo ya zahanati, ikanipa shilingi milioni 500 ya ukamilishaji wa majengo ya sekondari, wakanipa shilingi milioni 500 ya ukamilishaji wa majengo ya shule ya msingi, kila mwaka tutakuwa tumekamilisha kweli.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano elimu ya sekondari, nina majengo 63. Nikija kwenye shule za msingi majengo 80, kwenye zahanati majengo 42 yanataka ukamilishaji wa katika Jimbo la Solwa, ambapo tunakwenda kuwa na zahanati zaidi ya 80 out of vijiji 126. Naomba sana, sana tu, Wizara kama Wizara, tunapokuwa na miradi mikubwa, well and good, mradi wa reli safi kabisa; mradi wa umeme kule, safi kabisa; sasa twende kwenye huduma za jamii moja kwa moja. Hizo huduma za jamii ndiyo zinakwenda kusaidia wananchi wenye hali ya chini kule (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitengeneza maboma haya ya zahanati, shule za msingi na nyumba za walimu tukaenda kwenye sekondari, kama ulivyosema wewe wiki iliyopita, unapowapelekea madawati, mtoto wa masikini anapokaa, ni fadhila kubwa mno kwa Mungu. Sasa ndiyo twende huko. Tujikite sana kwenye maboma na ukamilishaji wa maboma katika Jimbo la Solwa pamoja na nchi nzima kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni upungufu wa watumishi kwenye zahanati zetu. Nina upungufu mkubwa mno katika zahanati mno. Serikali izingatie hili kupitia TAMISEMI,
Mheshimiwa Ummy namwaminia sana, upungufu wa watumishi ni mkubwa sana… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ahmed Salum.
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Spika, dakika ni chache, unaweza kuniongeza mbili!
SPIKA: Dakika tano ni chache sana. (Kicheko)
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, Mungu akubariki sana. Ahsante sana.