Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kukushukuru kwanza wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii adhimu, hasa tunavyotazamia kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika nchi yetu.
Lakini vilevile nitumie fursa hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri, Waziri Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa; pamoja na Naibu wake Deogratius Ndejembi kwa kazi nzuri ambayo wameanza kuifanya hususani nikiakisi hotuba nzuri ambayo imewasilishwa jana hapa Bungeni. Kimsingi mambo mengi ambayo nilitamani kuyazungumza Mheshimiwa Rais ameyatolea maelekezo jana na nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana japo bado hatujaingia katika mjadala wa kuijadili hiyo hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze mambo machache kwa ajili kuendelea kujenga na kuimarisha utumishi wa umma katika nchi yetu. Jambo la kwanza, tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi katika sekta zote. Nitakupa mfano, katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto hatuna kabisa Engineer wa Ujenzi. Hakuna Engineer wa Ujenzi kabisa, lakini tunapeleka fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, tunapeleka fedha nyingi kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati. Sasa unaweza kufikiria ni namna gani au ni miujiza gani inatumika kwenda kusimamia ujenzi wa fedha zote hizo za Serikali ambazo zinapelekwa kwenye Halmashauri zetu ikiwa hatuna wataalam kabisa katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sio huyo tu, Halmashauri hiyo hiyo haina Mwanasheria wa Halmashauri, haina mkusanyaji mapato kwa maana DT, hatuna treasurer kabisa kwenye Halmshauri ile. Sasa unaweza kudhani namna gani tuna upungufu mkubwa wa watumishi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoka kwenye uhaba huo wa watumishi ambao kimsingi inabidi kutumia nguvu ya ziada kama Taifa, pamoja na vipaumbele ambavyo vimepangwa katika miaka hii mitano, lakini tuwe na namna nzuri kubwa ya kuweza kuongeza na kujaza nafasi hizo za watumishi ili kusudi nguvu kubwa ambayo inawekwa hasa ya uwekezaji wa miradi na fedha nyingi iweze kuwa na tija kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maslahi ya watumishi bado ni changamoto, lakini nashukuru limeshatolewa maelekezo, lakini nisisitize tu kwamba hakuna wajibu bila haki kama ambavyo mama jana amesema. Ili tuweze kupata watumishi waweze kuwajibika vizuri ni vyema tukatoa haki kwa watumishi hawa, kwa maana ya malimbikizo ya madeni, wanadai fedha nyingi za likizo, wanadai fedha nyingi za overtime, wanadai fedha watumishi wa umma kwa miaka mingi, sasa pawe na kusudio maalum la kulipa haya madeni ili tuweze kwenda nao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitamani kulizungumza ni ushiriki wa watumishi kwenye uchaguzi, kwa maana ya ushiriki kwenye siasa. Ndugu zangu mtakumbuka mwaka jana wakati tunakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, ndipo ulipoanza kutumika rasmi Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa mwaka 2015. Waraka ambao ulitoa maelekezo ni namna gani mtumishi wa umma anakwenda kugombea nafasi za kisiasa hasa ya Ubunge na Udiwani. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Watanzania wote wanahaki ya kuchagua na kuchaguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, mtumishi wa umma anayo haki ya kuwa na chama cha siasa, lakini anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa umma kwa mujibu sheria hiyohiyo, wamewekewa utaratibu wa namna gani wanaweza kwenda kuchagua na namna gani wanakwenda kuchaguliwa. Namna nzuri ambayo imewekwa kwa mujibu wa sheria ni kwamba, mtumishi ataomba likizo bila malipo kwa miezi miwili na baada ya miezi miwili kwa maana ya ndani ya mchakato huo wa uchaguzi, kama atakuwa ameteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwenda kugombea kwenye jimbo au nafasi ambayo anakwenda kugombea maana nafasi yake pale itakuwa imekoma ile nafasi ya utumishi. Lakini wapo watumishi wa umma ambao mpaka sasa huu ni mwezi wa kumi wapo likizo ambayo hawajaiomba tena likizo ambayo haina mshahara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunatengeneza threat, tunatengeneza uoga kwa watumishi wa umma kwamba wasishiriki kwenye hizi nafasi za kisiasa. Mwisho wa siku, leo tunajisifu ndani ya Bunge letu Tukufu tuna watu wa mchanganyiko tofauti tofauti, tuna wataalam aina tofauti tofauti, hata Mheshimiwa Rais anavyoamua kufanya uteuzi hapati shida, watu wapo wenye taaluma tofauti tofauti. Lakini kama tunatengeneza huu uoga kwa watumishi wa umma kwenda kushiriki uchaguzi, maana yake ni kwamba miaka ijayo, tusishangae tukawa na hao darasa la saba walio wengi zaidi kwenye Bunge hili au kwa sababu ya kukosa ile motisha na namna ambavyo wanaweza wakalindwa wakiwa kwenye utumishi wa umma watakavyokuwa na nia ya kwenda kugombea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa mwaka 2015 mtumishi wa umma ikitokea hajachaguliwa kwa maana hajabahatika kupata nafasi yake anapaswa kurejea kwa kuomba kurejeshwa kwenye nafasi yake kwa mujibu wa waraka huo. Lakini kama hajapata nafasi ya kurejeshwa, anapaswa kulipwa mafao yake. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Husna Sekiboko kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kumpa taarifa mchangiaji. Anachangia vizuri anasema kwamba na….
MBUNGE FULANI: Declare interest.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu spika, na-declare interest kuwa mimi ni darasa la saba. Anasema kwamba humu ndani kuna watu wenye taaluma tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nafasi ya Ubunge ilitajwa kwamba mgombea Ubunge awe anajua kusoma na kuandika na sisi darasa la saba tunajua kusoma na kuandika, kwa hiyo asitutishe kwamba ikitokea tumekuwa yaani wataalam wamepungua wamebaki darasa la saba, hata sisi tunao uwezo wa kuiongoza Serikali. Nakushuruku sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, huo huwa ni mjadala mrefu, lakini kimsingi hili jumba hili ni la wa wawakilishi.
Kwa hiyo, wananchi yule wanayemleta ndio wanayeona ndio anaweza kuwakilisha hoja zao, yaani hoja ni uwakilishi, ndio maana Rais anakuwa na nafasi zake akiona humu kwenye uwakilishi hakutoshi analeta wa kwake anawapa hizo nafasi.
Kwa hiyo, kila kundi lina umuhimu wake humu ndani na wale wanao wachagua wanajua wanampeleka nani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Sekiboko malizia mchango wako.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu zimepungua naomba unilinde.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimalizie hii hoja kwa kuiomba Serikali sasa, Wakurugenzi hao ni watumishi wa umma na hata kabla ya kuteuliwa kuwa wakurugenzi walitokea kwenye Kanuni za Utumishi wa Umma, na namna ya wao kuingia na kutoka wanasimamiwa na Kanuni za Kudumu za Umma na Standing Order.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Makatibu Tawala wa Wilaya ambao nao ni watumishi wa umma per se, kuna Katibu Tawala wa Mkoa na wa Wilaya, kwa maana ya Makatibu Tawala. Sasa hao wote ningeiomba Serikali kutizama namna nzuri ya ku-handle hili suala lao. Ni kweli waliomba ruhusa wakaenda kugombea, lakini waraka umesema ni miezi miwili huu ni mwezi wa kumi. Ni vyema sasa Serikali itakoa hatma ya hawa watu kwasababu pamoja na kwamba baadhi yao wanatafsirika kama wateule wa Mheshimiwa Rais, lakini wanashughulikiwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)