Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kuwapongeza sana Waziri, Naibu Waziri wa Wizara hii ya Utumishi, lakini kwanza niendelee pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu shupavu, Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jana ametufundisha hapa, ametuelekeza masuala ya nidhamu na uwajibikaji katika kazi. Kwa hiyo, mengi yamezungumzwa kuhusiana na upungufu wa watumishi katika Halmashauri, Wizara naongeza na katika Balozi zetu. Kwa kweli eneo hili tuangalie, wakati mwingine, wakati tuna-solve suala upungufu tuangalie pia namna ya kutumia wanao-volunteer. Zipo idara zinaruhusu volunteers ambazo haziratibu nyaraka ambazo ni confidential, kule wanakoruhusu tuanze hata kutumia volunteers. Kuna wakati wananchi wetu wanakwenda katika ofisi unakuta ni muda wa kazi wakati mwingine maafisa hawapo ofisini. jukumu la utumishi wa umma ni kuhudumia wananchi. Wananchi wanafika katika ofisi zetu, unakuta watu hawapo na wakati mwingine mwananchi anaulizwa, una appointment? Sasa hii appointment niiombee wapi? Sijapewa email, sijapewa form ya kujaza appointment.
Tunaomba watumishi wa umma sekta zote na taasisi tunapoimarisha utumishi wa umma maana yake utawezesha hata uwekezaji. Anapokuja mwekezaji anahitaji ardhi, maji, masuala ya umeme, vibali mbalimbali, tunaposema tunakwenda kwenye uchumi wa kati basi kitu ambacho kinaimarisha ni pamoja na public service. Huduma hizi za Serikali tunaomba sana tubadilike, change of attitude, tunavyofika katika ofisi zetu wananchi wakija wale ndiyo mabosi wetu na sio sisi ambao tuko utumishi ndiyo mabosi. Tuwapokee wananchi vizuri. Ni mbaya sana mwananchi ana shida katika ofisi fulani anauliza, je, kuna mtu unamfahamu? Niepeleke ofisi fulani, no! wananchi wanapoenda katika ofisi za Serikali, wasikilizwe, waelekezwe na waoneshwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa lazima tubadilike unaenda kwenye ofisi unaambiwa mhusika huyo hayupo. Sasa lazima tujue kama mhusika umetoka kwa ruhusa umemuachia nani maana hizi ofisi tumetoa dhamana na tumeahidi wananchi tutawahudumia, leteni kero, msiwe na wasiwasi, sasa tunapokwenda katika hizi ofisi iwe ni halmashauri, iwe ni mikoa, iwe ni wizara, taasisi yaani hapa lazima tubadilike, tuwahudumie wananchi kiasi ambacho kinastahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naomba pia nilizungumzie, nipongeze sana PCCB., PCCB ina-fall chini ya Wizara hii wamefanya kazi kubwa sana. Wameokoa mabilioni katika uchunguzi, takriban bilioni 96 katika mifumo wameokoa takriban bilioni 11. Bado PCCB tunaomba mtusaidie katika miundo. Ni namna gani miundo hii kwanza tunaweza tukaokoa hizi fedha, lakini pia miundo mingi PCCB washauri iwe transparent. Upande wa TASAF, PCCB wamefuatilia masuala ya kaya na kuhakikisha maeneo yote kwamba hakuna kaya hewa, maana ziko kaya zingine zinaingia katika mfumo wa TASAF yamkini ni hewa.
Kwa hiyo, PCCB wafuatilie, kuhakikisha kwamba fedha tunazopeleka TASAF zinafika kwa walengwa kwa wakati unaostahili. Kwa hiyo, napongeza sana kazi nzuri, lakini bado kibarua cha kuboresha ili maendeleo yaweze kufika kwa wananchi yafanyike kwa ufasaha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni Serikali Mtandao. Serikali Mtandao ni eneo muhimu sana, niombe Serikali Mtandao tuweke taarifa muhimu. Sasa hivi watu wengi kutokana na hii changamoto ya Covid–19 mara nyingi sana wanatafuta taarifa katika mtandao. Kuna taarifa mbalimbali za Wizara mbalimbali; taarifa za masoko, bidhaa ambazo Tanzania tunauza katika Wizara zetu, kwa hiyo, wanapoingia wawekezaji na sisi wenyewe kupata taarifa fulani katika Wizara fulani tunaomba taarifa hizi ziwepo maana ni ngumu sana mwananchi kusafiri kutoka sehemu moja kwenda Makao Makuu ya Wizara wakati taarifa zingine unaweza ukapata katika mitandao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa kupitia e- government tuzidi kuweka ushirikiano na mahusiano ya Wizara mbalimbali na balozi zetu. Wakati mwingine kunakuwa kuna maswali mbalimbali katika Balozi zetu wanahitaji taarifa. Kwa hiyo, e–government tuone ni namna gani tutaweza kujitahidi kuweka taarifa stahiki zinazopaswa katika mtandao. Isiwe kwamba ah website haijawa updated tangu kipindi fulani. Katika eneo hili tuzidi sana kuboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine kama tulivyoambiwa nidhamu na uwajibikaji katika kazi ni suala zima la kupata mafunzo. Wakati umefika sasa watu wanaoajiriwa katika nafasi mbalimbali wapate mafunzo, the do’s and the don’ts, maana sasa hivi wakati mwingine katika ajira zetu unakuta bado taratibu zingine za kuhudumia wananchi watu hawajapata kuzielewa ipasavyo.
Kwa hiyo, Chuo cha Utumishi wa Umma nakipongeza sana na Kamati tulifanya ziara pale ya masuala ya Serikali za Mitaa, imefanya kazi kubwa, nzuri lakini tuendelee kuomba watoe mafunzo kwa taasisi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nalo ningependa kulizungumzia ni kuendelea kupongeza ujenzi wa Ikulu ya Dodoma. Ujenzi huu wa Ikulu ya Dodoma ni muhimu sana. Kwa hiyo, ujenzi huu utakapokamilika tuombe sana ujenzi wa Ikulu ya Dodoma uende sambamba na huduma. Maana tunaweza tukajenga vizuri sana, lakini ziwe ni zile huduma zinazopaswa kuwemo mle. Tunaita huduma za first class, hata Mheshimiwa wetu anavyofanya kazi Ikulu afanye kazi akipatiwa huduma za kutosha, stahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)