Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia jioni hii.
Mheshimiwa Spika, nimeomba maalum kwa ajili ya wananchi wa Kata ya Mayanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na ni kuhusu malalamiko makubwa ambayo yanatokana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na Kiwanda cha Simenti cha Dangote. Nitakwenda moja kwa moja, labda kama muda utaruhusu basi naweza nikaongea jambo lingine.
Mheshimiwa Spika, haya ni malalamiko ya muda mrefu na kwa taarifa ambazo nimezipata ni kwamba hata NEMC walishawahi kufika Dangote pale na waliwaandikia barua ili waweze kurekebisha hiyo hali. Kiwanda hiki cha Dangote ni kiwanda ambacho kipo katika Kata ya Mayanga, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Mheshimiwa Spika, mwanzoni wakati hiki kiwanda kinajengwa, tuliambiwa kwamba kutakuwepo na mechanism ambayo itakuwa inazuia zile pollutants kufika kwenye mazingira ya wananchi. Kwa bahati mbaya sasa, mwanzoni kilipoanza tukawa tunapata taarifa kwamba, nyakati za usiku unatoka moshi na vumbi lingi sana, tena wanasubiri nyakati za usiku ndipo hali hii inatokea, lakini imeendelea hivyo na baadaye sasa tunaona hata mchana hali hii inajitokeza.
Mheshimiwa Spika, sasa NEMC kwa taarifa hizo ni kwamba wameshapeleka barua Dangote, lakini mpaka sasa bado hali ni ileile. Kwa bahati mbaya ni kwamba wananchi wanapoona hali inazidi kuendelea wanaamua kwenda pale Dangote ili waonane na uongozi, lakini bahati mbaya tena zaidi ni kwamba wanazuiliwa getini, hawawezi kuonana na uongozi.
Mheshimiwa Spika, ni ombi langu kwamba Waziri, Mheshimiwa Jafo pengine na Naibu wake, walifanyie kazi hili. Wafike pale waonane na wananchi ili waweze kuwaeleza hali halisi. Hata hivyo, naomba zaidi sana hatua za haraka zichukuliwe ili kuweza kunusuru mazingira haya ambayo yanachafuliwa. Kwa kweli hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda unaruhusu, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan, kwa kupata nafasi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba. Nimpongeze sana kwamba jana tumesikia ametoa msamaha kwa wafungwa 5,000 na hii ina implication kwenye mazingira ya Magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumpongeze sana kwa sababu wafungwa wanaposongamana magerezani inaharibu pia mazingira ya magerezani na kuharibu pia afya zao. Kwa hiyo tunamshukuru sana na tunampongeza kwa kufanya jambo hili.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia…
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Wambura anasema Mheshimiwa Rais amesamehe wafungwa, siyo wale waliofungwa juzi pale Uwanja wa Benjamin Mkapa, hapana; wafungwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Wambura, endelea, nilikuwa nasisitiza unachokisema.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kutoa ufafanuzi; ni kweli wengine wasingeweza kunielewa.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Dkt. Philip Mpango kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Makamu wa Rais na kwa kupitishwa kwa kura nyingi sana na Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Jafo na Naibu wake; tumewaona wakipita katika maeneo ya machimbo na kusisitiza hali ya kuzuia uchafuzi wa mazingira. Kwa hiyo naomba waendelee na kasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kama muda upo, nizungumzie kidogo kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi ambapo tunaona sasa hivi mafuriko yanatokea mara kwa mara, wakati mwingine pia madaraja, barabara zinakatika. Nitoe mapendekezo kwa Serikali, mipango miji; tumezoea kuona wenzetu wa mipango miji wanatandika jamvi la viwanja. Inaweza ikatoka wilaya moja hadi nyingine, hakuna nafasi hapo katikati ya kuruhusu water sinks.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nipendekeze kwamba, wanapopanga mipango miji na kukata viwanja basi wawe na tabia sasa ya kuona kwamba mafuriko yanaweza yakatokea, kwa hiyo waache sehemu ambazo mvua zikinyesha zitapokea maji kwa sababu sehemu kubwa itakuwa imefunikwa na mapaa ya nyumba.
Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa miundombinu tubadilishe sasa standards tuongeze viwango vya barabara zetu, viwango vya madaraja, ili yaweze kuwa imara kuhimili mafuriko.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)