Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ili kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Madini. Pia nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, yeye pamoja na Naibu Waziri, lakini pia na timu yote nzima ya Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwa kweli tuwapongeze Wizara hii kwa kuweza kuchangia pato la Taifa na mpaka kufikia mwezi Septemba, 2020 iliweza kukua kwa asilimia sita. Kwa hiyo, tunaipongeza kwa kazi kubwa sana ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niipongeze pia Wizara kwa namna ambavyo iliweza kusimamia uanzishwaji wa masoko. Masoko haya makubwa takribani masoko 39 yalianzishwa, masoko madogo zaidi ya 41 na mengine yanaendelea kuzalishwa, yanaendelea kujengwa. Pia vituo vya ununuzi vidogo vidogo vile katika vijiji, vinaendelea kujengwa katika vijiji vyetu na hili linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa sana namna nzuri ambavyo tunaweza tukazuia utoroshaji wa dhahabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hivi vituo kuna changamoto kidogo ambayo wananchi wetu wanaweza kuipata kule. Moja ya changamoto ambayo wanaipata ni masoko haya kutofanya kazi siku za Jumamosi na Jumapili, lakini pia siku za Sikukuu. Kwa sababu, wachimbaji wetu wadogo wengi uchimbaji wao na kipato chao kinategemea kwa siku, aende asubuhi achimbe na jioni aweze kuuza. Sasa mchimbaji huyo anachimba vizuri, lakini akienda muda wa kwenda kuuza anaambiwa kwamba, sasa leo weekend soko limefungwa. Kwa hiyo tuone njia nzuri aidha haya masoko madogo kwa maana ya brokers na hizi buying station hizi ziweze kufunguliwa siku saba za wiki na hata siku ambazo ni za sikukuu pia, ziweze kuweza kufanya kazi ili wachimbaji wetu hawa wawe na uhakika wa kuuza dhahabu zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine, tumeona hapa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna vipaumbele ambavyo ameviweka, kipaumbele kimojawapo ni kuweza kuwaendeleza wachimbaji wadogo. Kweli juhudi kubwa zinafanywa, Wizara inafanya jambo kubwa kuwaendeleza wachimbaji wadogo na sisi sote tumekuwa mashahidi tunaona namna iliyokuwa bora ambavyo wachimbaji hao wanaweza kuendelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikumbuke hapo nyuma kidogo wakati Wizara imetengeneza utaratibu wa kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo iliweza kutengeneza mfumo wa kuwapa ruzuku. Wachimbaji wadogo walikuwa wanapewa ruzuku. Nakumbuka miaka kadhaa walikuwa wanapenda ruzuku na mara ya mwisho nadhani kama 2017 au 2018 ndiyo ruzuku hii ilikoma. Sasa hivi tukitaka kuweza kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo, tuweke mazingira mazuri ya kuweza kurudisha tena ile ruzuku. Ile ruzuku inawasaidia sana wachimbaji hawa, inawasaidia kimitaji na wao wanaweza kukua. Waliokuwepo Wizarani watakumbuka, wachimbaji wengi waliopata ruzuku ile miaka ya nyuma, leo hii wamekuwa wachimbaji wa kati, wameweza kukua na wao wameweza kuajiri wachimbaji wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Wizara iweze tena kuweza kutoa ruzuku kwa wachimbaji hawa wadogo, ili na wao waweze kukua na wao wataweza kutoa ajira, lakini pia pato kwa Serikali kwa sababu wataweza kulipa kodi vizuri zaidi. Nizungumzie suala la GST, GST hii Taasisi inategemewa sana sana na wachimbaji kwa sababu inafanya kazi kubwa na sisi wachimbaji tunaiona kazi ambayo wanaifanya. Nikiangalia kwenye taarifa hapa aliyokuwa anasoma Mheshimiwa Waziri, fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza utafiti kwenye hii taasisi ni takribani bilioni 3.4 tu. Kwa kweli fedha hizi ni kidogo mno, ukiangalia kazi kubwa ambayo taasisi hii inafanya na sisi wachimbaji tunategemea iendelee kufanya. Nashauri tuone namna iliyokuwa bora zaidi kuweza kuongeza fedha kwenye Taasisi ya GST, ili na wao sasa waweze kuwa na nguvu kubwa Zaidi, waweze kufanya kazi vizuri, waweze kuwafikia wachimbaji wetu huko na zile tafiti zao ziweze kuwasaidia wachimbaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii GST tunafahamu kwamba wako hapa Dodoma, tunashauri waweze kupewa fedha ili washuke chini huku mikoani maeneo ambako uchimbaji huu unafanyika. Wakiweza kushuka huku itatupunguzia gharama kwa wachimbaji wetu, mchimbaji anatoka Chunya, anatoka Itumbi aweze kuja mpaka Dodoma kuja kuleta mawe yake ili yafanyiwe utafiti, gharama inakuwa kubwa lakini pia inachukua muda, angalau ikisogezwa kwenye maeneo yetu ya mikoani kule itaweza kutusaidia sana sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye GST hii vile vile, ikumbukwe kwenye mabadiliko ya sheria ya mwaka 2017, iliyataka makampuni yote yanayofanya utafiti yakimaliza tafiti zao, copy ya tafiti zile ziweze kupelekwa GST. Sasa nishauri pia GST, zile tafiti wanazozipata waweze kuzinyambua katika lugha ambayo ni rafiki kwa sisi wachimbaji wadogo, ili baadaye wachimbaji hawa wadogo wakihitaji zile tafiti waweze kupewa, ziweze kuwasaidia katika uchimbaji ambao wanafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji ambao wapo hapa wanafahamu namna ambavyo wachimbaji wadogo wanachimba kwa kubahatisha, ni kama vile wanapiga ramli tu. Sasa tuondoke kwenye uchimbaji wa kupiga ramli, sasa twende kwenye uchimbaji ambao umefanyiwa utafiti mzuri ili wachimbaji wetu wanapochimba wawe na uhakika na kitu kile ambacho wanakifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la kodi, kuna wachimbaji wetu wa ndani lakini pia tuna wachimbaji wetu wa nje. Wachimbaji wetu wa ndani ambao wanachimba nje wakitoka na mali kule kuingia nazo ndani, bado TRA wanawakata kodi wanavyoingia na ule mzigo hapa ndani. Hata carbon wakitoka nazo nje, wakiingia nazo ndani bado TRA wanawakata kodi na bado wakija kuchenjua, baadaye wakipeleka mzigo sokoni bado wanaendelea kukatwa kodi kwa maana ya kwamba zile tozo ya mrabaha asilimia sita na inspection fee asilimia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri sasa tuone namna iliyokuwa nzuri zaidi ya kwamba, kama mtu anatoa mzigo nje anatuletea ndani, tusiwe tena tunamkata hiyo kodi kule. Ibakie kodi ya ndani, hii itawasaidia wachimbaji wa kwetu ambao wako nje, waweze kutoa mali kule kuleta ndani na sisi tutapata kodi kubwa zaidi hapa ndani. Kwa hiyo, upande wa kodi niishauri pia namna iliyokuwa bora zaidi ya mchimbaji huyu wakati anauza dhahabu zake tumkate kodi kwa asilimia, pale anapouza tumkate kodi kwa asilimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii itaweza kuwasaidia sana kwanza itasaidia Serikali kuweza kupata mapato ya uhakika, maana yake kila anayeuza dhahabu yake au madini yake atakatwa kodi pale pale. Pia itaweza kuwasaidia wachimbaji wetu, mchimbaji leo anachimba, anapata leo, lakini mwisho wa mwaka anakuja kulipa kodi. Kipindi ambacho anaambiwa alipe kodi fedha nayo hana, matokeo yake anakuwa na malimbikizo ya kodi na anashindwa kulipa hii kodi. Tukiweka utaratibu huo kwa asilimia utaweza kusaidia zaidi kwa wachimbaji hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna wale wachimbaji ambao huwa wanachimba lakini hawana eneo, hawana claim, hawana PML, sasa huyu mchimbaji huyu kila anachokipata, maana yake kama amekipata shambani kwake, huyo hawezi kulipa kodi kabisa. Sasa tukiweka utaratibu huu, maana yake hata huyu ambaye amepata dhahabu yake kwenye shamba lake, ataweza kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa TASAC. TASAC...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)