Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia. Niungane na wasemaji waliopita, kuwapongeza viongozi wa Wizara hii, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa mabadiliko yaliyo bora kwenye sekta hii ya madini. Tunachoomba ni kuboresha zaidi ili tuweze kunufaika kwa upana zaidi.

Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya hawa mineral explorers wanachukua leseni, wanashikilia maeneo kwa muda mrefu sana wakionyesha kufanya utafiti, lakini wananchi hawa wachimbaji wadogo wadogo wanakuwa wanafahamu kwamba maeneo hayo kuna madini. Matokeo yake inaanza kuingia migogoro baina ya hao wenye leseni na wale wachimbaji wadogo wadogo. Ushauri wangu, haya nimeyaona kwenye Jimbo la Butiama yakijitokeza. Kwa mfano, ipo leseni ya muda mrefu eneo linaitwa Rwamkoma, wana zaidi ya miaka sita wana leseni ile ya utafutaji madini. Pia lipo eneo lingine Katario, huyu mwekezaji wa kati ana leseni zaidi ya miaka nane lakini hajafanya chochote.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba, Wizara ikubali wawekezaji wa namna hii, haya maeneo wayaache kwa ajili ya wachimbaji wadogo waanze kuchimba madini, wafanye shughuli zao za kiuchumi badala ya kuendelea kuyaweka na wakati mwingine kukimbizana wakionekana ni vibaka wanaingia kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hili litafanyika kwa mfano kwenye Wilaya ya Butiama, Vijiji vya Nyakiswa, Kiawazaru, Katario, Kiabakari, Nyamisisi, Singu, Nyakiswa, watanufaika sana na wataweza kutoa CSR kwenye halmashauri na hivyo kuboresha huduma za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna eneo lingine ambalo tunadhani Serikali itusaidie, nimewatembelea wananchi kabla ya kuja huku Bungeni, wanasema, wamejifunza Mererani na Wizara ikawa-encourage kujenga fence kuzunguka kwenye mgodi wao unaitwa Irasanilo Mine kule Buhemba. Wamejenga ukuta ule zaidi ya milioni 200 wameshawekeza pale wale wachimbaji wadogo. Ushauri wetu kwamba Wizara isaidie kukamilisha fence ile ili wao waendelee kuwekeza kwenye uchimbaji, badala ya kuwaachia wananchi peke yao wale wachimbaji wadogo wakijenga fence kuzunguka eneo lote la mgodi. Hilo likifanyika litakuwa kwa kweli limewatendea haki sana watu wa Buhemba na Irasanilo Gold Mine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, nafahamu kwamba, Wizara imeipa nafasi STAMICO kuanza kuchimba madini na eneo hili la Buhemba ni eneo lililochaguliwa na STAMICO. Sasa inavyoonekana kama Waziri ataiachia STAMICO ichimbe pale, wale wachimbaji wadogo wataathirika sana. Sasa, najua kuna maeneo mengi, lakini ikiwapendeza, Wizara ione uwezekano wa eneo la Kilamongo kuliacha kwa ajili ya wachimbaji wadogo badala ya eneo lote kuiachia STAMICO. Kwa sababu, STAMICO ni wachimbaji wa kiwango cha kati, itakuwa ngumu sana kwa wananchi hawa ambao walikuwa wanachimba pale itaonekana kama tumewatelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako malalamiko ya baadhi ya wawekezaji kwenye sekta hii hususan kwenye eneo la makinikia. Sasa, liko eneo ambalo lina dhahabu kule Butiama, eneo la Nyasirori, kuna wawekezaji wa Kichina pale, lakini tunamuuliza kwa nini hachangii maendeleo ya halmashauri, anasema zaidi ya miaka minne hajaweza kufanya chochote kwa sababu, so far nchini hapa hatuna teknolojia ya ku-process makinikia, bado yanatakiwa yasafirishwe nje, lakini anasema pana vibali ambavyo kwa muda wote huu havijaweza kutolewa na kwa hiyo, muwekezaji huyu yupo tu lakini hakuna chochote kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, ni ushauri wangu kama Serikali inatambua kwamba, hatujawa na technology ya ku-deal na haya makinikia, basi hizo taratibu za kuwezesha hawa wawekezaji kusafirisha makinikia huko nje ziendelee. Bahati nzuri katika ripoti ya Mheshimiwa Osoro ilionekana wazi kwamba, wanaweza kufanya tathmini ya kujua kwenye makinikia kuna dhahabu kiasi gani. Sasa kama uwezo huo wanao, wafanye assessment kwa yale makinikia, huyu mwekezaji aruhusiwe kuyasafirisha, kodi za Serikali zilipwe ili halmashauri na wananchi wanufaike.

Mheshimiwa Spika, najua kwamba iwapo mgodi ule utaruhusiwa kuendelea, zaidi ya ajira 500 zitapatikana. Kwa hiyo, Serikali pia itapata kupitia pay as you earn. Kwa hiyo, nashauri haya yakifanyika yatakuwa yametusaidia sana kule Nyasirori ili Butiama nayo ianze kuchangamka kwenye sekta ya madini kama maeneo mengine yalivyochangamka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)