Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Sengerema, naomba kuchangia katika Wizara ya Madini.
Mheshimiwa Spika, napenda kuzungumzia kuhusiana na suala la wawekezaji. Tunao wawekezaji wengi ambao wamefanya kazi ya utafiti wa madini katika nchi hii. Wawekezaji hawa mpaka sasa hivi wako ambao wametoa taarifa zao na wako ambao taarifa zao bado hazijaenda katika Wizara kuonyesha kwamba wametafiti kitu gani na wamepata madini ya aina gani. Pamoja na hali hiyo, wako watafiti ambao tayari wameshamaliza utafiti wao na wako katika ngazi ya kupata leseni.
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana mdogo wangu Mheshimiwa Doto Biteko, kafanya kazi kubwa sana. Kwa mfano, Sengerema tuna Mgodi mpya wa Nyazaga, ameshakuja Sengerema zaidi ya mara sita, tumefanya vikao pale. Vilevile tumeshakwenda na Waziri wa Uwekezaji wa wakati huo, Mheshimiwa Kitila Mkumbo tumepanda juu ya milima yote kule Nyazanga na wamemlalamikia kuhusiana na suala la kuchelewa kupata leseni. Wakati Waziri anakuja kufanya majumuisho ya bajeti yake, naomba anieleze lini leseni ya Mgodi wa Nyazaga itatoka? Kama hatatueleza leseni hiyo itatoka mwaka huu, leo ni mwaka wa nne, shilingi ya mshahara wake japo ni mdogo wangu nitaing’ang’ania kwa niaba ya wananchi wa Sengerema, haitawezekana, hatutakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo naishauri sana Wizara hii wajaribu kutengeneza sera maalum ya wachimbaji wadogo katika nchi hii. Leo hii sheria zilizopo haziendani na sera. Kwa hiyo, lazima tujue nchi hii imeandaa nini kuhusiana na hawa wachimbaji wadogo?
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, leo tunazungumzia wachimbaji wadogo, wanagundua wao, wanafanya uvumbuzi wao wenyewe, wanaangalia eneo hili lina dhahabu, kesho kutwa anakuja mtu anakwenda pale na GPS anawahi kwenda kusajili. Waliogundua ni watu wengine wamekaa kule porini miaka sita au miaka mitatu, anakwenda mtu anapata leseni, anaanza kuwahangaisha hawa wananchi. Naomba sera yetu ya madini kuhusiana na wachimbaji wadogo na uwezeshwaji wao iwe bayana katika nchi hii.
Mheshimiwa Spika, la tatu katika jambo hili la hawa wawekezaji, wakati wanakwenda kupewa leseni lazima wawekewe masharti maalum. Masharti haya ni kwamba watoe eneo la wachimbaji wadogo na lililopimwa. Siyo wanatoa eneo la wachimbaji wadogo hawaelezi kwamba mwamba uko wapi? Wanaendelea kuachwa pale, wanakaa wanahangaika kwa miaka mingi. Wale wanafanya roho mbaya, waeleze kwamba mwamba umeelekea Mashariki, watu wachimbe kuelekea eneo hilo na wapate dhahabu waendeshe maisha yao.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la vifaa vya uchimbaji, tunaiomba Wizara kupitia STAMICO; kama STAMICO wameanza kutoa mafunzo, hawa STAMICO pia wanunue vifaa ambavyo vitakuja kuwasaidia wachimbaji. Kwa mfano, pump za kutolea maji katika mashimo ya migodi, sasa hivi migodi mingi ina maji.
Mheshimiwa Spika, tunamwomba Waziri, yeye mwenyewe bahati nzuri anatoka katika lile eneo, anajua maji yanavyosumbua wachimbaji wetu. Umeme tunamshukuru Mwenyezi Mungu umeanza kupelekwa katika maeneo ya wachimbaji, lakini pump zilizopo ni za China ambazo zina muda mdogo sana wa kufanya kazi. Watafute pump kutoka Japan, kutoka Uingereza, zije zisaidie uchimbaji wa dhahabu mwone dhahabu itakayozalishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine la mwisho tunaomba vifaa vya wachimbaji wadogo na vyenyewe vipewe ushuru. Kama mchimbaji mkubwa anapewa nafuu ya kodi, halipi kodi kwa miaka kadhaa, anaingiza vifaa vyake bila kodi, hawa wachimbaji wadogo ambao ndio wenye nchi yao, hawapewi nafuu ya kodi katika vifaa vya kuchimbia. Jambo hili linahatarisha sana amani katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, tunamwomba Waziri, tunamwona anavyofanya kazi, anachakarika na maeneo mengi anakwenda, tafadhali sana wawahurumie wachimbaji wadogo katika nchi hii. Suala la vifaa vya uchimbaji kwa mfano gololi za kuchimba za kwenye makarasha, kuandaa makarasha, hayo ni mambo ambayo mngeyapeleka SIDO, wakatengeneza makarasha ya gharama nafuu mkawapelekea wachimbaji wakakopeshwa haya makarasha, tungekuwa tunazalisha dhahabu nyingi sana ya kutosha. Leo karasha mtu anakwenda kununua kwa shilingi milioni saba, shilingi milioni kumi, ataipata wapi mtu masikini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wasaidieni wananchi katika nchi yao. Naombeni sana katika jambo hili. Nakuomba sana katika jambo hili la hawa wachimbaji wadogo hata wewe Spika unaweza ukafanya ziara; ukipata nafuu ya pumziko, uje uwaangalie wachimbaji wadogo wanavyopata shida. Nawe utaomba kabisa kwamba sasa tutengeneze sera maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika nchi hii.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)