Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Kwanza nami naomba nimshukuru sana na nimpongeze sana Mheshimiwa Biteko pamoja na Naibu Waziri wake kwa namna ambavyo wamekuwa wakisimamia vizuri sana sekta hii ya madini na Watanzania wote wanaona mafanikio na sote kwa ujumla tunanufaika kwa kuongeza pato la Taifa kwa asilimia zaidi ya tano kutokana na sekta hii ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kwanza nataka nizungumzie kuhusiana na suala la Mgodi wa Mwadui. Mgodi wetu wa Mwadui sote tunafahamu kwamba, Serikali ina asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75, lakini Mgodi huu tangu tarehe 8/4/2020 umesimamisha uzalishaji, lakini suala hili limetokana na kwanza kulikuwepo na kuporomoka sana kwa bei ya Soko la Dunia la Almasi na sote tunafahamu soko lile la almasi liko Ubelgiji peke yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya tatizo hilo, muda ule ule palitokea tatizo la Covid 19 na tangu kipindi kile mgodi wa Mwadui hadi sasa tunavyozungumza; tangu tarehe 8 ya mwezi wa Nne, mpaka sasa mgodi huu haufanyi kazi.

Mheshimiwa Spika, tunaweza tukajua pale katika eneo lile kuna watumishi zaidi ya 1,200, sasa Serikali inaweza ikaona tu kwamba kuna watumishi wengi sasa ambao wanapata shida na mahangaiko makubwa. Tatizo kubwa hili la kuteremka kwa bei ya almasi, bado ni changamoto hadi sasa, lakini angalau kuna improvement; na juzi waliamua kuanzisha uzalishaji, tatizo linalosumbua pale ni mtaji kwa ajili ya kuhakikisha mgodi ule sasa unaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ziko taratibu ambazo wameanzanazo ili mradi waanze ku-run huo mgodi na waanze kuzalisha, lakini tatizo kubwa ni mtaji wa kuanzia kwa sababu, zinatakiwa dola milioni 25 ambazo unaweza ukaona ni karibu shilingi trilioni tatu. Fedha hizi ni fedha nyingi. Kuna wakati wamezungumza na CRDB na NMB. CRDB walionesha mwelekeo wa kutaka kusaidia Mgodi wa Mwadui ili mradi uanze kuzalisha, lakini baadaye walirudi nyuma. Wameanza mazungumzo na NMB, lakini NMB mpaka sasa hivi hawaja-respond sawa sawa.

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni Serikali kuweka mkono wake ili mradi waone kwamba mgodi huu unaanza kuzalisha. Faida kubwa ya mgodi huu iko kote kote; kwenye Halmashauri kuna Service Levy ambayo Halmashauri Halmashauri ya Kishapu itaweza kupata, lakini kuna CSR ambayo inaweza ikasaidia mambo mengi sana kusukuma mbele shughuli za maendeleo, lakini na Serikali inapata mapato makubwa kutokana na mgodi huu. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweke jitihada za karibu sana, pengine wazungumze na waweke mkono wao ili CRDB ama NMB waweze kutoa fedha na mgodi huu uanze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna tatizo lingine katika mgodi huo. Kulikuwepo na suala zima la almasi ambazo ziliweza kukamatwa zilizokuwa na matatizo, Serikali imeshughulika na baadhi ya watumishi wetu walihusika katika kuhujumu. Tatizo hilo nadhani lilienda Mahakamani likazungumzwa likafikia hatua za mwisho.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naiomba Serikali iweze kutoa maamuzi, ikiwezekana kama sehemu hiyo ingefaa kurudishiwa sehemu ya zile mali Mgodi wa Mwadui waweze kurejeshewa, lakini hatua zile za kisheria kwa watumishi wetu ambao walikiuka ziweze kuchukuliwa, lakini mgodi uweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kuna masuala yale ya VAT kabla ya sheria haijaweza kubadilishwa, Serikali iweze kuangalia. Kwa sababu, kuna VAT ambazo zilipaswa kurejeshwa katika mgodi huo, hizi nazo pamoja na mali zitakazorejeshwa zinaweza zikasaidia mgodi ukaweza kufanya kazi yake…. (Sauti ilikatika)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka kuzungumzia suala la migogoro ya mipaka kati ya Nyenze na Ng’wang’holo. Kuna mwekezaji aitwae El-hilal ambaye eneo lile la Mwan’gholo na Nyenze kabla ya miaka miwili huko nyuma wananchi walikuwa wanalitumia kwa kilimo, kuchunga na mambo mengine, lakini juzi wachimbaji wadogo wakaja kuibua madini ya almasi, lakini huyu mwekezaji aliibuka na kusema eneo lile ana hati.

Mheshimiwa Spika, kipindi cha uchaguzi, aliyekuwa Rais wetu mpendwa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alielekeza jambo hili kwamba anakwenda kulishughulikia kwa sababu alitambua kwamba wananchi ndio waliogundua kule, lakini akaona ukubwa wa eneo hilo na akasema kwamba ipo haja ya wachimbaji wadogo kukatiwa sehemu ya eneo hilo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Boniphace!

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Serikali iweze kuchukua uamuzi na kuweza kufidia ili mradi…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: …wachimbaji wadogo waweze kupewa eneo hilo, lakini pia Wizara ya Ardhi waweze…

SPIKA: Mheshimiwa Butondo.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: … katika eneo hilo… (Sauti ilikatika) (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Wachimbaji wadogo leo wana watetezi kweli kweli.