Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wewe utakuwa shahidi, duniani watumishi ambao wanatoa huduma kwa wananchi na hasa kazi zao ngumu wamekuwa wakilipwa vizuri sana. Ukienda Marekani, Uingereza, Afrika Kusini na maeneo mengine, Walimu, Madaktari, Manesi na Polisi na vyombo vingine vya usalama wamekuwa wakilipwa vizuri, mazingira yao ya kazi yakiwa mazuri, pamoja na makazi yao kutokana na kazi ngumu wanazozifanya lakini na risk wanazoweza kukutana nazo kwenye kazi wanazozifanya.

Mheshimiwa Spika, mbali na changamoto za kiutendaji, lakini Polisi wetu wamekuwa wakilipwa mishahara midogo, hasa Polisi wa chini. Lakini sio tu, nyumba zao, ofisi zao ni aibu kulingana na mzigo waliopewa wa ufanyaji kazi katika Taifa letu. Nikitolea mfano pale Buhigwe, najua sasa hivi watakwenda kufanya kwa sababu ndio anakotoka Makamu wa Rais. Kuna muda Polisi walikuwa anafanyakazi kwenye matenti, kuna muda walikuwa wanatumia Ofisi ya Mtendaji wa Kata, lakini kuna wakati mwingine walikuwa wanakwenda kuchapisha documents mtaani. Hivi kuna siri za nchi au za kiupelelezi zinazoweza kuwa salama! Lazima tuboresha mazingira ya Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumesema tunataka jeshi letu liwe la kidijitali lakini leo computer imekuwa anasa, sio hitaji la msingi. Unaweza ukakuta Makao Makuu ya Polisi, nenda Wilayani, nenda mkoani kwa Bunda pale jimboni kwetu, maana nikisema langu italeta mgogoro, Jimboni kwetu pale Bunda, utakuta ofisi ya OCD ndio kuna computer, kwa OC-CID na traffic ziko computer tatu. Leo sisi hapa tuna Ipad kwa sababu tunataka twende na teknolojia na wenzetu duniani wanavyokwenda. Tubadilike tufanye jeshi letu liwe la kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye Jimbo la Bunda Mjini. Pale Jimbo la Bunda Mjini ndio Makao Makuu ya Wilaya ya Bunda ambayo ina majimbo matatu, Bunda Mjini, Bunda Vijijini na Mwibara. Kituo cha Polisi cha Jimbo la Bunda Mjini ni aibu, hakuna nyumba, wanakaa mtaani, hata hizo nyumba chache tu zilizokuwepo ni aibu. Hivi leo Sajenti anapewa labda chumba kimoja kwa sababu cheo chake kidogo hatakiwi kuwa na familia! Akiwa na watoto walale wapi, sebuleni? Wanandugu wakija. Please, tuwatendee haki hawa askari wetu ambao wanalinda Taifa hili kwa jasho na damu.

Mheshimiwa Spika, nilipokuwa Mbunge wa Jimbo at least kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo niliwasaidia jengo la upelelezi; nilipokuwa Mbunge wa Vijana, niliwapa mabati katika kujenga bwalo lao, tangu nilipofanya mimi kimya! Please, naomba Wizara iboreshe kile kituo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halafu na mahabusu, uzuri nami nililala pale, kwa Mkoa wa Mara labda kama sijalala mahabusu ya Serengeti. Mahabusu ile ni ndogo na mbaya yaani haina hadhi, inawezekana mahabusu hiyo watu 10 ikawa ni shida, hewa hakuna. Please, tunaomba pia Wizara ikarabati mahabusu ya Bunda.

Mheshimiwa Spika, tunaomba kile Kituo kiendane na hadhi ya wilaya, Wizara ipeleke na magari. Hivi leo hii akitokea mwizi Nyamswa, kukitokea uhalifu Mwibara, mafuta yenyewe shida, katika Wilaya yetu ya Bunda ambayo inaunganisha majimbo hayo matatu kama nilivyosema.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nizungumzie gereza la Jimbo la Bunda Mjini. Nilipokuwa Mbunge niliwakarabatia mahabusu moja, ikawapelekea na tv pale, ile mahabusu inatia aibu, nyumba za magereza Bunda Mjini ni shida.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na mradi umeanza tangu nilipochangia kidogo leo nyumba zipo kwenye lenta. Mpaka sasa hivi bado kuna shida kubwa mahabusu ile ya gereza la Bunda pale ni shida, lakini hata dawa kwenye Gereza la Bunda hakuna. Mdogo wangu kwenye uchaguzi alikamatwa, ilikuwa anaandika dawa ndiyo nampelekea. Je, wafungwa wengine wanakuwaje wasiokuwa na ndugu na wanatoka kwenye maeneo mbalimbali? (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, jambo lingine mlipe madeni ya polisi ya kuhamisha na mnapowapeleka kozi muwalipe kama watu wengine sio mnawakata kwenye mishahara yao wakati mnaenda kuwaongezea ujuzi. Ni aibu. (Makofi)