Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie Wizara hii. Mimi nitajielekeza kwenye eneo la tafiti tu, limesemwa na wajumbe wengi lakini na mimi niseme hapa kidogo.

Mheshimiwa Spika, kwanza muhimu ni vizuri tujue hata nini maana ya tafiti katika elimu ya juu. Mwananzuoni mmoja anaitwa Godwin Kalibao anasema, utafiti unahusisha kukusanya data, habari na ukweli kwa ajili ya kuendeleza ujuzi. Yupo mwingine anaitwa John W. Gasswell anasema, utafiti ni mchakato wa hatua za kukusanya na kuchambua habari ili kuongeza uelewa wetu wa mada na masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kwa kina sana na nilimsikiliza vizuri wakati anaendelea kuzungumzia baadhi ya vyuo vyetu kuanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Mzumbe, DUSE na vyuo vingine vya ufundi na zaidi katika eneo la tafiti. Nampongeza kwa sababu kama Serikali pia bado inaendelea kutoa fedha kidogo kwa ajili ya machapisho na tafiti mbalimbali lakini hazitoshelezi. Ukiangalia uhitaji wenyewe kwa takwimu mbalimbali ambazo unaweza ukazipata, mimi nimejaribu sana kwenda kwenye taasisi zetu za tafiti mbalimbali kuanzia NBS na nyingine nyingi, inaonyesha tunahitaji tafiti na machapisho mbalimbali kwa kiasi kikubwa kuliko ambavyo vimewasilishwa katika bajeti ya 2021 hata matarijio ya bajeti yetu tunayokwenda nayo sasa au tunayoianza hii ya 2021/ 2022.

Mheshimiwa Spika, pamoja na faida nyingi za tafiti, kwa muda siwezi kusema yote, zipo faida mbalimbali; moja, ikiwa ni kupata taarifa muhimu kuhusu suala linalotafitiwa; kuongeza hazina za maarifa katika eneo hilo lakini kupima joto la hali, fikra na mitazamo mbalimbali. Pamoja na faida hizi zote katika maeneo ya tafiti hatujafanikiwa kama taifa kwa sababu ya changamoto zilizopo. Changamoto kubwa kama Taifa ni mbili; ya kwanza ni gharama na ya pili ni wataalam wabobezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la gharama nimefurahi sana, Mwenyekiti wa Kamati alivyokuja mbele hapo amesema kwenye eneo hili hatujafanikiwa sana na akatolewa mfano COSTECH wameweka shilingi bilioni 3.8 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na anasema hazitoshi kabisa, sasa hili ni eneo moja tu. Pia Mwenyekiti amesema katika nchi za Ulaya wameweka makadirio ya mchango wa Pato la Taifa liwe ni asilimia tatu ambayo inaenda kwenye utafiti lakini kwenye nchi za Afrika ni asilimia moja. Unaweza ukaona bado kama Afrika tunahitaji kujivuta sana in particular ni Tanzania sisi tupo wapi. Hali yetu bado si nzuri sana katika eneo la gharama.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine nijaribu kusema, hili la gharama mara nyingi tumeendelea kutegemea wafadhali ndiyo maana katika bajeti yetu hatuwezi kuiona imeweka kiasi kikubwa kwa ajili ya tafiti. Tunakubali, tunahitaji wafadhali watusaidie tufanye tafiti lakini ukweli hawa wafadhali ili watupe fedha zao tufanye tafiti ni lazima tafiti zitaenda kwa ajili ya majibu yao na hiyo ndiyo changamoto. Hizi tafiti sisi tunazotaka kuzifanya ni za aina mbili tu, tafiti za msingi ambazo wanaziita basic research lakini na tafiti tumizi applied au pure research. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Taifa lazima tujue hizi tafiti za msingi ambazo ndiyo zinatumika kwa muda mrefu, je, tunazo kwa kiasi gani? Hitaji letu ni lipi? Zimepungua kwa kiasi gani? Zinahitaji gharama gani? Tunashindwa kufika hapo. Hizi za muda mfupi ambazo ni tafiti tumizi, tunazo kwa kiasi gani? Mpaka sasa zimetafitiwa kwa kiasi gani katika hitaji lipi la jamii katika maeneo mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa, tunapokosekana kwenye eneo hili la tafiti, tunashindwa kujielekeza katika mipango yetu mbalimbali. Mheshimiwa Mpina asubuhi amezungumza juu ya kushindwa kujielekeza kujua kwa sasa tunahitaji elimu ipi? Elimu yenye ujuzi kwa kiasi gani? Watu wafundishwe nini ili wakaombe, wakapate soko la ajira ambalo linafanana na elimu wanayoihitaji? Yote ni kwa sababu ya kukosa tafiti.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo ya kilimo, Mheshimiwa Naibu Waziri mara nyingi anasimama hapa, anatueleza juu ya uhitaji wa mbegu za kisasa na kadhalika. Huwezi kujua hitaji la mbegu kwenye nchi kama hatuna tafiti za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika maeneo mengine ya afya na usalama wa wananchi wetu, ili tuweze kujua yote ni lazima tafiti mbalimbali za muda mfupi na mrefu ziweze kufanyika. Nilisema maeneo mawili ni changamoto. Eneo la pili, ni la wataalam wabobezi. Hao wanaweza kuwa ni wale wenye shahada za uzamivu na umahiri, Ph.D na Masters, lakini zaidi ni hawa za uzamivu Ph.D.

Mheshimiwa Spika, wewe utakuwa ni shahidi, Mwenyekiti pia kasema, changamoto ya kwanza katika elimu ni upungufu wa wataalam katika vyuo vyetu. Hili wote tunakubaliana kwamba ni kweli, tuna changamoto ya wahadhiri. Hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ameendelea kueleza udahili wa wanafunzi katika eneo hili la umahiri na uzamivu, kote amesema katika vyuo vyote; nami nimeendelea kuweka pale 28, 34, 18, 64 wanaingia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukimtafuta Mheshimiwa Profesa Ndalichako ambaye ni mbobezi wa zaidi ya miaka 18 mpaka 20 ni sawa na wale wanaoenda kufundishwa leo! Nataka kusema nini? Nataka kusema, leo tuna changamoto ya ubora wa elimu katika nchi yetu (quality). Katika hili hatupingani. Tunakubali watoto wetu wanakwenda, enrollment ni kubwa katika kipindi cha miaka mitano mfululizo, lakini katika wataalam hakuna ongezeko. Yaani ukitafuta hizi mbili, line moja inaenda katika kuongeza watoto wengi mashuleni kwa kipindi cha miaka mitano… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Issa Mtemvu. Muda hauko upande wako. (Makofi/Kicheko)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)