Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hii hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyoonyesha na kwa muonekano wake, anaonekana amejiandaa na yuko tayari kulitumikia Taifa hili katika kuhakikisha kwamba katika kipindi chake cha miaka mitano basi suala la viwanda linakuwepo katika nchi yetu, nampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi yake nzuri ambayo anaifanya. Mahali popote unapopita, kwa kweli kila mmoja anaona kwamba sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeanza kwenda mchakamchaka. Sisi kazi yetu ni kuendelea tu kumwombea kwa Mwenyezi Mungu, aendelee kuwa na maisha marefu, lakini na kazi yake iweze kuendelea vizuri kwa kadri inavyoonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kumwomba Mheshimiwa Waziri, pale kwangu kwa maana ya Jimbo la Musoma Mjini, kwa bahati mbaya sana tuko pembezoni. Huwezi kupita Musoma kwenda mji wowote ule, ili uje Musoma lazima ufunge safari ya kuja Musoma na hatuna economic activity yoyote zaidi ya biashara ndogondogo na viwanda. Ombi langu la kwanza, nimwombe kabisa Mheshimiwa Waziri hebu apange, tukae siku kama tatu hivi pale Musoma maana tulikuwa tunasaidiwa na Kiwanda cha Mutex, Kiwanda cha Nguo, nacho hivi leo ninavyozungumza kinaenda kwa kusuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, viko viwanda kama vinne vya samaki, kwa bahati mbaya sana sasa hivi tunacho kiwanda kimoja tu nacho kinasuasua. Kwa hiyo, kwa maneno mengine, watu wa Musoma Mjini leo hawana ajira, vijana hawana kazi za kufanya, matokeo yake sasa ni kuongeza vibaka lakini na uchumi wa mji unaendelea kudorora. Kwa hiyo, hilo ni ombi langu la kwanza ambalo naomba kwamba hebu tufike kule ili tuweze kusaidiana tuone tutafanyaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Mutex kilipobinafsishwa, kuna mafao ya watumishi ambayo nimeyapigia kelele katika Bunge hili toka mwaka 2005 hadi leo, wale waliokuwa wanadai wengi wao wamepoteza maisha, lakini hata watoto wao wanaendelea kudai. Kwa hiyo, nimwombe kabisa Mheshimiwa Waziri tutakapofika pale, tupate nafasi ya kuzungumza nao na Serikali sasa itoe majibu yao ya mwisho ili wajue kama hayo mafao yao wanayapata au la kama hawayapati basi waweze kufahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili zoezi la kuendeleza viwanda, tunavyo viwanda vya ngozi hapa nchini. Hivi viwanda vinaonekana vimekufa kwa sababu mpaka leo ukiangalia kwa wafanyabiashara au wachinjaji ngozi zao wanatupa bure. Kwa sababu leo anauza kilo ya ngozi kwa bei isiyozidi sh. 200, tafsiri yake ni kwamba, hakuna wanachokipata. Kwa hiyo, tunadhani na hili nalo Mheshimiwa Waziri ajaribu kutuambia, hivi viwanda vilivyopo mkakati wake ni nini katika kuwasaidia wananchi wetu wa Tanzania maana vinginevyo tutajikuta wale Watanzania tulionao ambao wanafanya biashara hizo basi wanaendelea kufilisika siku baada ya siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo na kwa ufupi hili suala ambalo Serikali imezungumza kwamba tunahitaji kukuza viwanda. Mchango wangu ni kwamba, kama leo tunakubaliana kwamba Tanzania tunahitaji iwe ya viwanda, lazima tukubaliane hivi viwanda tunavyovihitaji ni viwanda vya aina gani. Leo ungeniuliza mimi vile viwanda vikubwa vyote vinavyokuja, kwanza vingi ni automation, utakuta kiwanda ni kikubwa lakini watu kinaowaajiri ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu la kwanza pamoja na kuanzisha viwanda na kwa kuwa lengo letu ni ajira tungeiangalia vizuri sana SIDO, tuangalie namna ya kuiwezesha kwani kule vijana na akinamama wanapata mafunzo mbalimbali. Ni imani yangu kwamba yale mafunzo wanayoyapata, ukiangalia wanaweza kuzalisha bidhaa nzuri sana, zile bidhaa zinaweza zika-compete katika masoko mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuendelea sasa ni vizuri Mheshimiwa Waziri akawa na mkakati maalum, kwanza kuhakikisha kwamba wataalam wanaendelea kuwepo SIDO na mafunzo yanaendelea kutolewa. Bahati nzuri SIDO ipo karibu katika kila mkoa, kama ni vijana pamoja na akinamama tayari wameshajifunza, wamepata mafunzo sasa tuna nafasi ya kuwapa mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi ni kwamba hata vile viwanda ambavyo tunaona vinaleta bidhaa nyingi, maana Mheshimiwa Waziri leo amejibu hapa kuhusiana na suala la toothpick, amesema kwamba kile kiwanda kinagharimu siyo zaidi ya dola 28,000, wako Watanzania wengi tena wenye uwezo wa kawaida wanazo hizi fedha, lakini tatizo letu sasa ni kwamba hawa Watanzania wengi hawana exposure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbe kinachotakiwa sasa, tukishatoa haya mafunzo, wakati mwingine Mheshimiwa Waziri hawa Watanzania hebu waulizwe, naamini watakuwa tayari kupata exposure kwa fedha zao, waende kwenye nchi za wenzetu kama India, China na hizi nchi Asia, viko viwanda vidogo vidogo huko ambapo wakirudi watavianzisha hapa kwa fedha zao na kwa kusaidiwa na benki na vingi viwe vile ambavyo vinaweza kuzalisha bidhaa zinazoweza kutumika humu nchini. Kwa hiyo, tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo tunaweza kusaidia Watanzania wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja ambalo mimi binafsi nalifahamu na hizo ni hisia zangu, ni kwamba, Serikali yetu haijawa tayari kuhakikisha kwamba inawasaidia hawa Watanzania ambao wanaibukia kwa kuwajengea uwezo ili na wao waweze kufanya biashara. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba tukienda kwa utaratibu huo hii SIDO itafanya kazi nzuri. Hebu tuzalishe zile bidhaa ambazo tunaweza kuziuza humu humu nchini na kwenye hizi nchi za jirani kuliko kuanza kupambana na yale masoko ya wenzetu, masoko ya Ulaya ambayo ushindani ni mkubwa kwa hali yetu kusema ukweli siyo rahisi sana tukaweza kuingia huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye nchi za wenzetu mfano kama Syria, kila mwaka kuna bidhaa ambazo wanaleta hapa nchini. Zile bidhaa zote zinatengenezwa na viwanda vidogo vidogo kama SIDO. Ukienda kwenye nchi jirani ya Kenya, kuna hivi viwanda wao wanaita Juakali, Juakali ina mchango mkubwa sana Kenya na inatengeneza bidhaa nyingi, nzuri na ambazo zinaweza zikashindanishwa katika masoko mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu ni hilo kwamba hebu tuangalie namna ya kuweza kuisaidia SIDO, watu wakapata mafunzo na baada ya kupata mafunzo tuone namna ya kuwasaidia, lakini namna wanavyoweza kupata exposure na wakaja kufanya biashara zao mbalimbali na tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo basi tutakuwa tumewasaidia sana Watanzania wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mchango wangu kwa leo, lakini niendelee tu kumwomba Mheshimiwa Waziri kwamba, kusema ukweli wale watu wetu wa Musoma kule wanahitaji msaada mkubwa wa Serikali ili waweze kuendelea. Nina uhakika vijana na akinamama wakisaidiwa wanaweza kujikwamua. Maana hayo mengine nazungumza kutokana na uzoefu wangu kwamba pale tulipojaribu kuwasaidia vijana, pale tulipojaribu kuwasaidia akinamama wanaweza kwenda, lakini tatizo kubwa ni kwamba vijana hawana ramani.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.