Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kwa kupata nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza kwenye maeneo mawili; kwenye Bodi ya Mkopo pamoja na Shule yetu pedwa ya St. Jude ambayo ipo pale Mkoani Arusha. Hii ni shule ambayo inasomesha watoto 1,800 bure. Wanatoa chakula bure, usafiri bure, wanalala kwenye mabweni bure na masuala mengine yote. Watoto hawachangii hata shilingi moja. Pia wanasomesha watoto 350 Chuo Kikuu kwa gharama zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, pia wameajiri watu 295. Kati yao, Watanzania ni 286 na wageni wako saba. Cha kushangaza mwaka 2020, mwezi Oktoba, TRA walikwenda kuifunga akaunti ya shule hiyo ambayo ipo kwenye Benki ya NCBA na tarehe 03, Novemba, 2020, walikwenda kuchukua fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kutoka kwenye akaunti ya shule hiyo huku wakiwa wamewapa assessment ya shilingi bilioni 5.43.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unajiuliza, hii shule haifanyi biashara, wanaunga mkono juhudi za Serikali za kusomesha bure watoto wa Kitanzania. Mazingira ya shule ni mazuri, lakini bado TRA wanakwenda wanawagawia assessment ya 5.4 billion na wanafunga akaunti yao na wanachukua fedha kiasi cha milioni 500, fedha ambayo ingetumika kwa ajili ya chakula cha watoto, kwa ajili ya uniform za watoto na masuala mazima ya uendeshaji.
Mheshimiwa Spika, nadhani Wizara ya Elimu, mama yangu, Mheshimiwa Prof. Ndalichako, ana kazi kubwa ya kuliangalia suala hili kwa kushirikiana na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Katika hili nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Elimu kwa sababu yeye alimtuma Katibu Mkuu wake akaenda kutembelea shule hii akaona changamoto hizo na wakaahidi kwamba wataongea na Wizara ya Fedha ili changamoto iondoke kwenye shule hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwenye eneo hili, kwa sababu shule hii haifanyi biashara, nina mapendekezo mawili. Pendekezo la kwanza shule hii ipate msamaha wa kodi. Pendekezo la pili, kwa sababu tumepata taarifa maana kuna wadau wanasaidia kwenye shule hii na tunaambiwa zaidi ya asilimia 92 ambao wanasaidia shule hii wanatoka Australia na wako wageni ambao wanafanya kazi ya kusaidia kwenye fundraising na wanasaidia kwenye masuala ya marketing, wameomba vibali vya kazi kupitia Idara ya Kazi, wamekosa. Sasa hivi wamekata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana, mama yangu, Mheshimiwa Mhagama, mtu ambaye ni mchapakazi, ni mtu ambaye anaendana na falsafa ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu kwamba Mheshimiwa Mhagama atakwenda kulipa kipaumbele jambo hili, tuwasaidie watu hawa wawili wapate vibali vya kazi na vibali vya ukaazi ili mwisho wa siku wasaidie kutafuta fedha kwa ajili ya shule ile na watoto wa Kitanzania waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ni kuhusu Bodi ya Mikopo. Katika hili kwa kweli…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gambo, hebu tusaidie jambo moja; katika hiyo shule, umetaja hiyo idadi kubwa ya wanafunzi.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Ndiyo.
NAIBU SPIKA: Hiyo shule ina wanafunzi wanaosomeshwa bure tu au inao na wengine ambao wanasomeshwa kwa kulipa fedha?
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wote pale wanasoma bure ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa kike 600 na pia wameanzisha na shule ya sayansi, wana masomo ya PCB na PCM ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na changamoto ya sayansi na teknolojia. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Haya, endelea na hoja yako.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusiana na Bodi ya Mkopo. Kwanza kabisa nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali Sikivu ya Awamu ya Sita chini ya mama yetu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Nampongeza pia Waziri wa Elimu kwa sababu nina imani ameshauriana na Mheshimiwa Rais na mwisho wa siku akaweza kufanya maamuzi haya yenye tija kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata taarifa kwanza siku ya Mei Mosi, Mheshimiwa Rais alitutangazia kwamba asilimia sita ya kulinda thamani ya fedha imeondolewa. Jana pia tumepata taarifa kuwa asilimia 10 ambayo ilikuwa imewekwa kwa wale ambao wanachelewa kulipwa kama penalty na yenyewe pia imeondolewa. Hayo ni mambo makubwa na kama Wabunge tumekuwa tunayapigia kelele kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna changamoto moja kubwa. Tunafahamu kwamba mwaka 2016 Bunge hili lilitunga sheria, lilifanya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo kutoka asilimia nane kwenda asilimia 15. Changamoto ambayo naiona kwenye hiyo sheria ni kwamba badala ya sheria kuanza kutumika mwaka 2016, imerudi toka watoto walivyaonza kukopeshwa hizo fedha. Matokeo yake, ukiangalia ripoti ya CAG ya mwaka 2016/2017, kwa sababu wao wanafanya sampling, hawakwenda kwa wahusika wote ambao wanatakiwa kulipa. Wanafunzi au wafanyakazi 4,830 wanalipwa mshahara chini ya moja ya tatu, kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Na. 7 ya mwaka 1970 inasema ni lazima mtumishi yeyote ambaye anafanya kazi, lazima makato yake yasizidi mbili ya tatu ya malipo au pato ghafi ambalo analipwa. Kitendo cha Wizara ya Elimu kushirikiana na Serikali yote kwa ujumla kurudi nyuma zaidi mwaka 2016 imekwenda kuwaathiri wafanyakazi wengi sana. Wapo ambao walikopa kwa sababu wanajua wao wanakatwa asilimia nane, unavyomkata asilimia 15 maana yake ni kwamba unakwenda kuathiri kipato chake na mpango wake mzima wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia waraka wa Serikali wa Novemba, 28, 2012, wenye Kumbukumbu Na. CE26/46/01/66 unaelekeza makato ya watumishi yasizidi mbili ya tatu ya mishahara yao ghafi. Kitendo cha Serikali kwenda kuwakata watumishi zaidi ya mwaka ambao sheria imetungwa, kwanza ni kukiuka sheria na kutumia mabavu, kitu ambacho tunadhani siyo sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Rais wetu ni mtu msikivu, ni imani yangu jambo hili litakwenda kupewa kipaumbele na pendekezo langu kwenye jambo hili ni kwamba asilimia 15 ianze kukatwa kuanzia mwaka 2016 na isirudi nyuma ili kuwapa ahueni wafanyakazi wetu. Ahsante sana. (Makofi)