Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima kuwepo katika Bunge lako hili Tukufu. Pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Elimu imekuwa na falsafa nyingi wakati wa miaka nenda rudi. Kulikuwa na suala la Elimu ni Ufunguo wa Maisha, Elimu ni Bahari, Elimu haina Mwisho. Hayo yote ilikuwa ni kuhakikisha tunahamasisha elimu katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI kwa jinsi ambavyo wanajitahidi kuhakikisha kwamba elimu katika nchi yetu inasonga mbele. Kama tunavyofahamu elimu ndiyo imefanya Taifa hili likafika mahali hapa. Kuna mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema anaitwa J.K. Chesterton alisema: “Education is simply the soul of a society as it passes from one generation to another.”
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yote ni mwelekeo wa kuhakikisha kwamba Taifa letu linakwenda kuwa salama kwa sababu wananchi wetu wanapata elimu. Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru TAMISEMI kwa jinsi ambavyo wametuletea fedha za mabweni, madarasa na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo nitajikita katika maeneo manne kuhusu vikwazo vya elimu. Vikwazo vya elimu vipo vingi lakini leo nitajikita katika vinne. Kwanza, suala la lugha, lugha ya kufundishia katika shule za msingi kuanzia chekechea mpaka darasa la saba ni Kiswahili, lakini mtoto huyo anapofundishwa Kiswahili masomo kumi na moja, mara moja anatoka kuingia form one, anafundishwa masomo yote Kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto hawa wanateseka kwa sababu hawajui lugha ya Kiingereza wanapoingia form one. Hii inatuleta utata mkubwa, watoto wanachukia shule, hawapendi shule kwa sababu hawaelewi wanapofundishwa darasani form one mpaka form four na wakati huo huo wanapewa mtihani huo kwa Kiingereza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiombe Wizara ya Elimu hebu suala hili liangaliwe kwa sababu ukiangalia shule za private kuanzia chekechea mpaka darasa la saba ni Kiingereza, lakini mtoto wa shule ya Serikali anakwenda form one akiwa anajua Kiswahili tu, ushindani huu hauko sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waziri wa Elimu atakapokuja hapa atuambie utafiti huu unasema nini kuhusu mtoto wa darasa la kwanza wa Serikali mpaka darasa la saba, akaja akaingia form one kwenda four inakuwaje? Hapo kuna usawa au tunawatesa watoto kisaikolojia. Naomba tupate maelezo kwamba Serikali inafikiria nini kuhusu hili jambo, kwa sababu hata ukiangalia ufaulu katika za Serikali watoto wanapata zero nyingi. Tunasema tupunguze zero, tutapunguza zero wakati tunawatesa watoto kwa lugha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia shule za private wanafaulu sana kwa kiwango cha juu, kwa sababu wao wametoka Kiingereza shule za msingi, wameingia shule za sekondari lugha ni ile ile ya Kiingereza. Suala hili naomba baadaye Waziri atakapokuja aweze kutueleza vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikwazo kingine ni chakula shuleni. Watoto wanateseka, kule shuleni wanasema, Serikali imetoa elimu bure au elimu bila malipo, wazazi wanasema hatuwezi kuchangia maana Serikali imetoa fedha. Sasa ni vizuri Wizara ya Elimu na TAMISEMI itoe tamko kwamba kila mzazi ana wajibu wa kuhakikisha kwamba mtoto wake anapata chakula au Serikali itoe chakula mashuleni, kwa sababu tunatengeneza Taifa ambalo tunadhani tuna usawa lakini hatuna usawa. Tutatenga watu walionacho na wasionacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wanaosoma private wanakula chakula kizuri mpaka wanamaliza shule, lakini watoto wanaosoma shule zetu za Serikali wanateseka, wanakataa shule, wanaingia makorongoni, wengine wanapata mimba na kadhalika. Ni kwa nini sehemu hiyo Wizara isitoe tamko, imekaa kimya, naomba atakapokuja pia aweze kutujibu kuhusiana na hiyo suala la chakula shuleni watoto wanateseka na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la upungufu wa walimu. Hili ni tatizo, mtoto anakwenda shuleni lakini katika masomo ya physics, chemistry, biology hakuna Mwalimu, lakini mwisho wa siku anapewa mtihani, kuna usawa gani hapo? Naomba Serikali ijitahidi kwa kadri iwezavyo kuwaajiri Walimu hasa wa sayansi ili kuleta usawa katika shule za Serikali na private, vinginevyo tutatengeneza Taifa la wenye nacho na wasio nacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala la Walimu liangaliwe, waajiriwe walimu wa kutosha. Nilikuwa nasoma taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema hadi kufikia 2030 inahitajika Walimu milioni 69 kukidhi. Je, Tanzania sisi tumejiandaaje na suala hilo la kuhakikisha kwamba tumekuwa na Walimu wa kutosha. Pia, naomba Waziri atakapokuja atuambie pamoja na kwamba kuna ajira 6,000 za Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan amesema waajiriwe, lakini bado kuna haja ya kuongeza jitihada za kuhakikisha kwamba Walimu wanatosheleza ili kuleta usawa katika shule zetu za private na shule za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba suala la elimu ujuzi, wenzangu wamezungumza sana. Tuhakikishe kwamba katika Taifa letu mtu akimaliza, sio anazunguka na vyeti kutafuta kazi, anazunguka na vyeti huku na huku, kazi, kazi, lazima Wizara ya Elimu itengeneze Elimu Ujuzi. Iangalie namna gani itatengeza hiyo sera ili iweze kuhakikisha kwamba watu wetu wanakwenda kusoma lakini wawe na ujuzi wa kutosha kujiajiri na hata kuajiriwa ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)