Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri iliyojitosheleza. Namfahamu sana Mheshimiwa Mwijage, nilijua na niliamini ataleta hotuba nzuri ambayo imejitosheleza kama alivyoisoma hapa. Pia Waziri huyu ni msikivu na ni mfuatiliaji sana na Wizara hii inamfaa kwa sababu amekuwa akitushauri, amekuwa akitufuatilia kwenye mikoa yetu kuona kipi kinafaa ili tuweze kufanikiwa. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa azma yake ya kufanya Awamu ya Tano kuwa ya viwanda. Hii analenga kutubadilishia uchumi tulionao wa chini na kutupeleka kwenye uchumi wa kati. Hivyo tuungane sisi Waheshimiwa Wabunge kumwombea Mheshimiwa Rais na Serikali yetu ili tufikie hapo tunapokwenda na tusiwe watu wa kukatisha tamaa, tuwe watu wa kuwapongeza na kuwashauri ili tuweze kufikia pale tulipokuwa tumejipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu niliongelea kuhusu suala la tumbaku lakini kwa umakini wa suala hili, naomba niongee tena. Nimkumbushe pia Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Tabora tunalima tumbaku kwa asilimia 60 lakini Serikali imewekeza pesa nyingi sana kwenye reli na barabara, hii pia inasaidia sisi Mkoa wa Tabora kupata viwanda kwa sababu sasa tutakuwa na reli na barabara nzuri, tumbaku tunalima asilimia 60, sioni sababu gani inayoweza kufanya sisi Tabora tusiwe na viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepiga kelele sana kuhusu viwanda vya tumbaku Tabora, lakini hata kiwanda cha ku-process hatuna. Wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu niliongea, namshukuru sana Mheshimiwa Mwijage, alinifuata na akaniambia kwamba amepata mwekezaji wa Kichina na atakuja hapa sisi Wabunge wa Mkoa wa Tabora tutaongozana naye kwenda Tabora. Nimwombe sana Mheshimiwa Mwijage atutimizie hilo neno alilotuambia ili sisi Wabunge wa Tabora angalau tuonekane sasa tunajali wananchi wetu maana hawatuelewi na wana Wabunge humu ndani zaidi ya 12. (Makofi)
Wabunge wa Tabora sasa tuna mkakati mkubwa wa kuhakikisha Tabora tunapata kiwanda cha tumbaku, wote tumekubaliana tuhakikishe Serikali inatupa kiwanda cha tumbaku au hata cha ku-process tumbaku. Nimshukuru Waziri Mwijage ametuahidi kwamba atatuletea Mchina. Mheshimiwa Waziri hali ya ajira Tabora ni mbaya, vijana wetu hawana ajira wakati sisi ni wakulima wakubwa wa tumbaku, naomba tupate kiwanda. Sijui nani alitoa wazo nchi hii la kupeleka kiwanda cha tumbaku Morogoro wakati tumbaku inalimwa Tabora!
Kwa kweli huwa najiuliza hata sipati jibu, sioni sababu. Kibaya zaidi juzi tena kimejengwa kiwanda kingine cha sigara Morogoro, kwa kweli hii inatuumiza sana kama wananchi wa Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kuhusu Kiwanda cha Nyuzi. Pale Tabora kuna Kiwanda cha Nyuzi cha muda mrefu, lakini kiwanda hiki kimekufa muda mrefu. Naiomba Serikali yangu, kama kweli inaheshimu wakulima wa pamba, wahakikishe kiwanda hiki kinafufuliwa na kinaanza kufanya kazi. Naomba sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie, nini hatima ya kiwanda hiki? Kiwanda hiki kimeanza kupigiwa kelele na Wabunge wengi waliotutangulia ambao leo hii hawamo humu; nasi pia toka mwaka 2011 mpaka leo tunakipigia kelele, lakini hatupati hatima yake ni nini, hakitengenezwi, hakifunguliwi!
Mheshimiwa Naibu Spika, leo namwomba Mheshimiwa Waziri wakati ana-windup atuambie ana mkakati gani kuhusu Kiwanda cha Nyuzi cha Mkoa wa Tabora? Nasi pia vijana wetu wanahitaji ajira, hawana ajira, hali ya uchumi inakuwa mbaya kila siku, mpaka kuna baadhi ya watu wanatucheka kwamba Tabora hakuna maendeleo. Ni Serikali haijatuletea hayo maendeleo, tunalima tumbaku lakini hatuna viwanda, lakini pia tuna Kiwanda cha Nyuzi ambacho kimefungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba tena Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara ageuze sasa zao la asali liwe zao la biashara. Watanzania wengi humu ndani ya nchi yetu wameshajua nini maana ya kutumia asali na naamini watu wengi sasa hivi wanatumia asali. Pia zao hili lina soko kubwa nje ya nchi yetu. Namwomba sasa Mheshimiwa Waziri aliboreshe zao hili, awe na mkakati maalum wa kuboresha zao la asali ili liwe zao la kibiashara; lakini pia tupate viwanda vya ku-process asali ili vijana wetu wafaidike na zao la asali na pia wapate ajira ili na sisi kama watu wa Tabora tupunguze huo umaskini. Naomba sana Mheshimiwa Waziri akija ku-windup atuambie pia mkakati wake alionao katika kiwanda cha ku-process asali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutuletea EPZ ndani ya Mkoa wa Tabora. Sisi kama watu wa Tabora tumeipa Serikali heka 200 ili kujenga viwanda vinavyotokana na mazao ya kilimo, ikiwemo tumbaku, asali pamoja na viwanda vya ufugaji. Naiomba sana Serikali, ile ardhi tumewapa bila kulipa fidia, bila gharama yoyote ile ili waweze kutusaidia kutafuta wawekezaji tupate viwanda. Nia yetu ni kupata viwanda ili tuweze kupata ajira za vijana wetu na hatimaye na sisi tuweze kuondoa umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukipiga kelele sana Wabunge wa Mkoa wa Tabora, kwa kweli Mkoa ule ni wa siku nyingi, lakini cha kushangaza na cha kutia masikitiko makubwa, Mkoa ule hauna kiwanda hata kimoja. Malighafi zinazopatikana, Tabora zinapelekwa mikoa mingine kuwekewa viwanda na watu wa kule ndio wanaofaidika. Kitu hiki kinatuumiza sana sisi Wabunge wa Mkoa wa Tabora na kuonekana kama vile hatuji kuwasemea na kuwasaidia waliotuweka madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusema kwamba tumtie moyo Mheshimiwa Waziri, tuitie moyo Serikali yetu ya Awamu ya Tano, iendelee na mkakati wake wa kuhakikisha Awamu ya Tano inakuwa Awamu ya Viwanda, hatimaye tutoke kwenye uchumi wa chini na kuingia kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wale wenzetu wanaosema kwamba huu Mpango hauna maana yoyote, hatuko kwenye dhana ya viwanda…
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Washindwe na walegee. Naunga mkono hoja.